Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, May 10, 2011

MAKAMU WA RAIS DKT BILAL AUNGURUMA ISTANBUL


Na Mwandishi Maalum, Instabul

Tanzania imetoa wito kwa nchi tajiri kutambua nafasi yao katika kuzikwamua nchi maskini ili ziweze kukuza uchumi wake na kuwasaidia wananchi waliomo katika nchi hizo.


Kauli hiyo imetolewa jana na Makamu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal wakati akihutubia mkutano wa nne wa Umoja wa Mataifa unaojadili maendeleo ya nchi maskini unaofanyika nchini Uturuki.


Dk Bilal alisema mataifa maskini yametekeleza mambo mbalimbali ambayo yameshauliwa na mataifa makubwa sambamba na mashirika ya kimataifa, lakini kikwazo kimebakia katika nafasi za mataifa makubwa kutimiza ahadi zao ili kuzikwamua nchi maskini kutoka katika hali zilizomo.

“Kama ambayo ripoti mbalimbali zinavyoonyesha utekelezaji wa malengo yaliyowekwa kwa muongo wa mwaka 2001 -2010, nchi maskini zimemudu kutimiza malengo yao mengi, kama sio makubaliano yote yaliyotolewa na nchi tajiri kwa nchi maskini. Jambo linalokatisha tamaa ni hali ya nchi tajiri kutotimiza ahadi wanazotoa,” Dk Bilal alisema.


Akichukulia mfano wa Tanzania, Dk Bilal alizielezea nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuwa tangu kupitishwa kwa Azimio la Brussels mwaka 2001, Tanzania ilibadili sera zake nyingi zikiwemo zile zilizolenga kupunguza umaskini nchini kama MKUKUTA, ikaweka vyombo vya kusimamia ukuzaji wa uchumi, ikaongeza nafasi za wanawake katika vyombo vya maamuzi, ikaanisha chombo cha kupambana na rushwa huku pia ikitoa uhuru mkubwa kwa vyombo vya habari.


Dk Bilal aliendelea kufafanua kuwa, Tanzania katika kipindi hicho imeongeza uwazi katika mambo mbalimbali yanayofanywa na serikali, imefanikiwa kupitia upya mikataba ya madini na imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kwa kutumia uwezo wake wa ndani kutanua wigo wa demokrasia nchini.


Mifano mbalimbali ya Dk Bilal aliyokuwa akiitoa katika hotuba yake ililenga kuonyesha nafasi ya nchi maskini katika kujikwamua lakini akasisitiza kuwa jitihada hizo peke yake hazitoshi kwa kuwa nchi tajiri ndizo zinazodhibiti uchumi wa dunia, huku pia zikiwa na fursa nyingi katika ushindani kuliko nchi maskini.

“Bado ipo haja kwa nchi maskini kupewa fursa zaidi katika soko ambalo halina masharti magumu. Kama hoja hii ikitekelezwa vema ni wazi nchi hizi zitamudu ushindani katika biashara za ndani na zile za kimataifa. Hali iliyopo sasa haitoi fursa hizo,” alisema na kuongeza.


“Ili nchi maskini zimudu kuondoka katika kundi hili ndani ya kipindi cha miaka kumi ijayo, jukumu lililo mbele yetu ni moja ambalo ni kuweka mikakati ya wazi na kila upande kutimiza wajibu wake kama ambavyo Tanzania imedhamiria kufanya.”


Dk Bilal yuko jijini Instabul akiongoza ujumbe wa Tanzania unaohusisha pia wabunge, wawakilishi wa asasi za kiraia sambamba na wafanyabiashara. Hii ni mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kuhusisha wabunge, wawakilishi wa asasi za kiraia na wafanyabiashara katika mkutano wake wa kujadili maendeleo ya nchi maskini tangu kuanza kwa mikutano hii miaka 30 iliyopita.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohamed Gharib Bilal, akiteta jambo na Balozi mdogo wa Tanzania nchini Italia, Salvator Mbilinyi, wakati wakiwa nje ya ukumbi wa mkutano wa Istanbul, Uturuki walipohudhuria katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo ya nchi Maskini, ulioanza jana na kumalizika Mei 13 mwaka huu. Kulia ni Katibu wa Makamu wa Rais , Zahor Haji.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohamed Gharib Bilal, akizungumza na Naibu Msaidizi wa Shirika la Misaada la watu wa Marekani (USAID), Donald K Steinberg (wapili kulia) na ujumbe wake wakati walipokutana kwa ajili ya mazungumzo kwenye Ukumbi wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa uliofsnyika jijini Istanbul Uturuki kuhusu maendeleo ya Nchi Maskini Duniani. Mkutano huo ulianza jana na unatarajia kumalizika Mei 13 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...