Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Msama Promotions, imemkamata mmoja wa watuhumiwa wa mtandao wa kundi la wanyonyaji wa kazi za wasanii wa muziki wa injili, Seleman Mtupwa.
Mtuhumiwa huyo aliyekamatwa juzi kwa kurudufu kanda ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam, alipelekwa Kituo cha Polisi Magomeni.
Kukamatwa kwa Mtupwa kumetokea baada ya kiongozi wao, Francis Kamalamu, aliyekuwa akifanya biashara hiyo katika eneo la Ubungo Maziwa, Dar es Salaam, naye kutiwa mbaroni, akiwamo Mwakwi Yahya.
Baadhi ya wanyonyaji waliokwishakamatwa ni Fred Jumbe, Martin Mkinga, Abdallah Kijemi, Abdallah Salum, Yahya Salum, Lazaro John, Amir Kassim, Faraj Amir, Rashid Juma na Mustafa Rashid.
Harakati za kuwakamata wanyonyaji hao zilianza mwishoni mwa mwaka jana, ambapo maofisa usambazaji wa Kampuni ya Msama Promotions, walianza harakati za kuwasaka wanyonyaji hao na kufanikiwa kuwanasa vijana kadhaa wakiziuza CD za muziki wa Injili.
Wanapozikuta, maofisa hao wamekuwa wakiweka mtego kwa kujifanya ni wateja wa CD hizo kisha wanawakamata wahusika.
Imeelezwa kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akiiuza CD moja kwa sh. 1,700, na alikamatwa na mali zenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 1.2 huku wenzake wakikimbia.
Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akijikusanyia zaidi ya sh. milioni 2.1 kutokana na kurudufu kanda hizo.
Mtuhumiwa bado anaendelea kushikiliwa kwenye Kituo cha Polisi Magomeni, Dar es Salaam, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi Kinondoni, ACP Charles Kenyela, alisema uchunguzi zaidi unaendelea.
Msama alisema vijana wake wa kikosi kazi wanaendelea na msako dhidi ya maharamia hao Dar es Salaam na hivi karibuni watahamia mikoani.
No comments:
Post a Comment