Marquee
tangazo
Thursday, October 7, 2010
CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI ZA MICHEZO (TASWA) CHATOA TAMKO KUUSU KUNYANYAPALIWA KWA WANA HABARI
CHAMA Cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kimesikitishwa na hatua ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza itatoa tiketi kwenye mechi ya Taifa Stars na Morocco badala ya kadi ambazo zimekuwa zikitumika karibu kila mechi kubwa.
Hatua hii ya TFF tunaiona kama ni ubaguzi na pia kutaka kuwagawa waandishi wa habari za michezo maana walio wengi watakosa kwenda kushuhudia mchezo huu, licha ya juhudi kubwa walizofanya katika kuutangaza kwa umma.
TASWA hailazimishi waandishi wa habari waingie wote, lakini inasikitishwa na namna wanavyonyanyaswa hasa linapokuja suala la mechi kubwa zinazofanyika Uwanja Taifa Dar es Salaam.
Sote tunakumbuka tukio la Juni mwaka huu wakati wa mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Taifa Stars na Brazil ambayo waandishi walio wengi walishindwa kuingia uwanjani kutokana na utaratibu ambao haukuwa mzuri, na ulioleta malalamiko kwa wanachama wetu.
Kwa kutambua hili uongozi mpya wa TASWA ulipoingia madarakani Agosti 15 mwaka huu, siku mbili baadaye yaani Agosti 17 Siku ya Jumanne saa tano asubuhi, ujumbe wa viongozi watatu wa juu wa TASWA ulienda ofisi za TFF Uwanja wa Karume Dar es Salaam kujitambulisha na pia kuzungumza masuala mbalimbali yahusiyo waandishi wa michezo na namna ya kuingia uwanjani.
Upande wa TASWA waliohudhuria walikuwa ni Mwenyekiti, Juma Pinto, Makamu Mwenyekiti, Maulid Kitenge na Katibu Mkuu, Amir Mhando, wakati upande wa TFF uliwakilishwa na
Makamu wa Kwanza wa Rais, Athumani Nyamlani, Kaimu Katibu Mkuu, Sunday Kayuni, Ofisa Habari wa TFF, Florian Kaijage na Wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji, Eliud Mvella na Muhsin Said.
Ikumbukwe kikao hiki kilifanyika siku moja kabla ya mchezo wa Ngao ya Hisani kati ya Simba na Yanga, hivyo tulijadiliana kwa kirefu namna ya waandishi kuingia uwanjani hasa tukirejea tukio la mechi ya Stars na Brazil.
Kwenye mjadala huo tulikubaliana kwamba wakati utaratibu mwingine ukiandaliwa ambao utaridhiwa na pande zote mbili yaani TASWA kama wawakilishi wa waandishi wa habari za michezo na TFF kama wasimamizi wa mpira nchini, zitumike kadi ambazo TFF ilizitoa miaka miwili iliyopita kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, ili kuepusha usumbufu kwani zinatumika kwenye ligi.
Tulifikia uamuzi huo wa kutumia kadi kwa kuwa TFF ndiyo iliyozitoa na si nyingi kama wengi wanavyofikiria, mjadala ulikuwa mbona mechi nyingine huwa zinatumika? Hivyo kikao kikaazimia kwamba zitumike kadi hizo na hilo likafanyika na limekuwa likifanyika.
Mambo mengine ikiwemo suala la ukaaji wa waandishi wa habari uwanjani lilizungumzwa lakini ikaonekana kwa Uwanja wa Uhuru TFF wakasema hawana mamlaka nalo, lakini tukapeana muda wa kulitafutia ufumbuzi.
Hili la namna ya ukaaji uwanjani napenda tuseme wakati TASWA mpya ilipoenda kujitambulisha kwa Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo na aliahidi kwamba kwa kushirikiana na TFF watalifanyia kazi.Hivyo hatuna wasiwasi nalo.
Lakini TASWA imesikitishwa sana na kauli iliyotolewa na uongozi wa TFF kwamba watatoa tiketi badala ya zile kadi zao ambazo ndizo waandishi wanatumia iwe mechi ya Stars au timu nyingine yoyote maana kwetu tuliona ndizo 'ACCREDITATION' za TFF viwanjani.
Tunashangaa kwamba TFF kwa makusudi imeamua kuyaweka kapuni yale tuliyozungumza kwenye kikao cha Agosti 17 na kwa kweli hili ni jambo ambalo halipaswi kufanywa na watu wanaofanya kazi kwa pamoja, sisi tukiwa wadau wakubwa wa TFF.
Tunachokiona hapa TFF ina huruma ya mamba, ambaye anakutafuna huku anatoa machozi ukidhani kwamba anakuonea huruma kumbe ndiyo staili yake ya kukumaliza.
Kwa msingi huo Taswa haipo tayari na haikubaliani na utaratibu wa utoaji kadi uliotangazwa na TFF badala yake tunasisitiza umuhimu wa kutumika zile kadi ambazo zinatumika kwenye mechi mbalimbali.
Tunajiuliza maswali kwa nini Morocco? Kwa nini waandishi waelezwe mabadiliko sasa? TFF ina nini? Mbona haikutujulisha kwamba siku tunajadili kwenye kikao ilikuwa tunapoteza muda?
Kwa misingi hiyo tunaandaa mkutano wa pamoja kati ya Taswa na wahariri wa michezo wa vyombo mbalimbali vya habari kesho ili tutoke na msimamo wa pamoja kuhusu TFF na hatua gani tuchukue kutokana na mambo haya ya waandishi wa michezo kutothaminiwa.
Tunawasisitiza wanachama wa Taswa waendelee kuwa watulivu kipindi hiki wakati tukitafuta ufumbuzi wa jambo hilo, lakini kwa kuanzia TASWA haikubaliani na utaratibu huu, hivyo TFF waufanye wenyewe kwa sababu wao ndio wenye mamlaka ya mpira na wanaona hatuna la kufanya na mawazo yetu huwa yanapuuzwa, kwani wametuomba tushirikiane nao kuandaa uataratibu wa tiketi hizo lakini hatutajiingiza huko maana kama hawakuheshimu kikao cha Agosti 17 itakuwa leo?
Hata kama TASWA itatoa mawazo mazuri namna gani, TFF haiwezi kuyafanyia kazi.Waendelee wenyewe na utaratibu wao maana kusudi haina pole.
Chama kimekuwa kikipokea shutuma nyingi kwa uamuzi unaotolewa na TFF sisi hatutaki tuwe kama yale mambo ya msafara wa ng’ombe, ambaye anayechelewesha yuko mbele,lakini viboko anapigwa wa nyuma ambaye ni TASWA. Hilo hatutalikubali hata kidogo.
Tunaishauri TFF iwe makini na jambo hili, vinginevyo heshima ya shirikisho hilo itaingia matundu bila sababu za msingi ni kama watu waliojificha mvua kwenye mpapai.
Tunamalizia kwa kusema kuwa kama TFF wenzetu wanajua mbio, sisi tunaelewa njia
Ahsanteni
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment