Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Monday, September 12, 2011

BENKI YA NBC YAKABIDHI MSAADA KWA WAHANGA WA TUKIO LA AJALI YA MELI ZANZIBAR, YAFUNGUA AKAUNTI MAALUMU.


Mshauri wa Mambo ya Habari wa Benki ya NBC, Redemptus Masanja (kushoto) akikabidhi sehemu ya misaada iliyotolewa na NBC kwa ajili ya wahanga wa ajali ya Meli ya MV Spice Islander kwa Waziri wa Afya wa Zanzibar Juma Haji Duni Mjini Zanzibar juzi. Kulia ni Meneja wa Tawi la NBC Zanzibar, Rajab Maalim.
Waziri wa Afya wa Zanzibar, Juma Haji Duni (kushoto) akipokea msaada wa vyakula, dawa, maji na misaada mingine ya kibinadamu iliyotolewa na Benki ya NBC kutoka kwa Meneja wa Tawi la benki hiyoVisiwani Zanzibar, Rajab Maalim kwa ajili ya wahanga wa ajali ya Meli ya MV Spice Islander iliyotokea usiku wa Septemba 10 visiwani humo.. Hafla ilifanyika Zanzibar juzi.
Ofisa Uhusiano wa NBC Tanzania, Eddie Mhina (wa pili kushoto) akisaidiana na baadhi ya wafanyakazi wa benki hiyo na wakazi wa Zanzibar kushusha baadhi ya vitu vilivyotolewa msaada na benki hiyo kwa ajili ya wahanga wa ajali ya Meli ya MV Spice Islander iliyotokea usiku wa Septemba 10 visiwani humo. Hafla ya makabidhiano ilifanyika Visiwani Zanzibar juzi.

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imekabidhi misaada mbalimbali ya kibinadamu kwa ajili ya tukio la ajali ya Meli ya abiria iitwayo MV Spice Islander iliyozama katika Bahari ya Hindi Visiwani Zanzibar na kupotea idadi ya watu na kuacha majeruhi wengi.

Akikabidhi misaada hiyo kwa Waziri Afya wa Zanzibar, Juma Duni Haji, Meneja wa Tawi la Benki ya NBC mjini Zanzibar, Rajabu Maalim alisema NBC imepokea taarifa za tukio hilo kwa masikitiko makubwa mno kwani baadhi ya waliopoteza maisha na majeruhi ni wateja wa NBC au ni ndugu na jamaa za wateja wetu au wafanyakazi wa NBC.

“Sisi kama Benki ya Taifa ya Biashara baada ya kupokea taarifa hizi tumeona ni vyema tukajitokeza kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali na taasisi nyingine zisizo za kiserikali ili kujaribu kuokoa maisha ya majeruhi wetu wa ajali hiyo ambayo imeitikisa nchini yetu.

Pamoja na kukabidhiwa kwa misaada hiyo ya madawa, vyakula, nguo , na maji yenye thamani ya shs milioni tano, Benki ya NBC pia imefungua akaunti maalumu katika Tawi la mjini Zanzibar iitwayo MV Spice Maafa Account yenye Namba 021206007793 ili kuwapa fursa wananchi kujitokeza kutoa michango yao ambayo itapelekwa moja kwa moja kwa chombo kinachoratibu tukio la ajali hiyo.

“NBC imeona tena ni vyema kuwapa nafasi nyingine kwa wateja wetu na hata wale ambao si wateja visiwani humo na nchini kote kutoa michango yao kupitia akaunti hii ili kuokoa roho za ndugu zetu waliojeruhiwa na pia kuwasaidia wale ambao walikuwa wakiwategemea waliopoteza maisha.

“Majeruhi wa ajali hii wanaohitaji msaada wa kimatibabu ni wengi lakini pia wako baadhi ndugu wa karibu wa maheremu walioachwa wakiwa na mahitaji mbalimbali hivyo tunatoa wito kwa wateja wetu, wafanyakazi na wote wenye mapenzi mema kujitokeza kutoa michango katika matawi yetu Tanzania kote kupitia akaunti hii,” alisema Meneja huyo wa Tawi la NBC mjini Zanzibar.

Meli ya Abiria ya MV Spice Islander ilipata hitilafu na kuzama katika Bahari ya Hindi katika eneo la pwani ya Nungwi wakati ikisafiri kutokea Unguja kuelekea Kisiwani Pemba usiku wa kuamkia tarehe 10 septemba 2011.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...