Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Oliver Mhaiki (kulia) akimkabidhi Mwenyekiti wa Sauti ya Wanawake Walemavu Tanzania (SWAUTA) Bi. Modesta Mpelembwa sehemu ya nakala 1,500 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 zenye thamani ya Tshs 32 milioni zilizoandikwa katika maandishi ya nukta nundu ili kuwawezesha walemavu wasioona kuisoma Katiba hiyo. Hafla fupi ya makabidhiano hayo imefanyika Wizarani hapo leo Jumanne, Septemba 27, 2011.
Na Mwandishi Wetu
Katika kuhakikisha kuwa elimu ya Katiba inawafikia wananchi wengi zaidi, leo (Jumanne, Septemba 27, 2011), Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeikabidhi asasi isiyo ya kiserikali ya ‘Sauti ya Wanawake Wenye Ulemavu (SWAUTA)’ nakala 1,500 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika maandishi ya nukta nundu zenye thamani ya zaidi ya Tshs 32 milioni.
Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi nakala hizo iliyofanyika katika Ofisi za Wizara ya Katiba na Sheria jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Oliver Mhaiki alisema ni nia ya Serikali kuona kuwa makundi yote ya wananchi wanapata elimu ya Katiba hususan katika kipindi hiki cha mchakato kuandikwa kwa Katiba mpya ya nchi.
“Upatikanaji wa Katiba kwa makundi yote hasa katika kipindi hiki kuelekea kuandikwa kwa Katiba mpya ni muhimu sana,” alisema na kuongeza kuwa umuhimu huo unatokana ukweli kuwa Katiba ndiyo sheria mama na hivyo wananchi wa makundi yote hawana budi kuifahamu na kuielewa ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato muhimu wa kihistoria wa kuandika Katiba nyingine baada ya miaka 50 ya Uhuru.
Bw. Mhaiki aliongeza kuwa kutokana na umuhimu huo, ndiyo maana Serikali kupitia Wizara yake ilipopokea ombi la SWAUTA la kutengenezewa nakala za Katiba katika maandishi ya nukta nundu mwezi Mei mwaka huu haikusita kulifanyia kazi uamuzi uliopelekea kutengenezwa kwa Katiba hizo.
“Tulivyopokea ombi lao (SWAUTA) mwezi Mei mwaka huu tukaanza taratibu za kutafuta fedha na manunuzi ambapo hatimaye Kampuni ya Edpar Coporation Ltd ya jijini Dar es Salaam ilishinda zabuni hiyo baada ya taratibu zote za kisheria kuzingatia,” alifafanua Bw. Mhaiki.
Katibu Mkuu huyo aliwaagiza viongozi wa SWAUTA kuhakikisha kuwa Katiba hizo zinatunzwa ili zidumu na hivyo kutumika na walemavu wengi zaidi.
“Kama nilivyosema gharama ya kutengeneza nakala moja ya Katiba katika nukta nundu ni takribani Tshs 21,000/- wakati Katiba iliyopo katika maandishi ya kawaida ni kama Tshs 3,500/-. Hii ni gharama kubwa na ni lazima tuzitunze ili zinufaishe wenzetu wengi zaidi,” alisema katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo na wawakilishi wa walemavu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa SWAUTA Bi. Modesta Mpelembwa aliishukuru Serikali kwa msaada huo na kuahidi kuwa Katiba hizo zitatunzwa kama inavyotarajiwa na Serikali.
Akizungumzia usambazaji wake, Bi. Mpelembwa alisema Katiba hizo zitasambazwa katika mikoa yote kwa lengo la kuwafikia walemavu wakiwemo wanafunzi na wananchi walemavu wa kawaida
“Katiba hizi zitasambazwa katika asasi zote za walemavu bila ubaguzi wa jinsia, dini, umri wala jiografia ili walemavu waweze kupata elimu hii muhimu,” alisema.
SWAUTA ni asasi isio ya kiserikali ya wanawake yenye Makao Makuu yake jijini Dar es Salaam iliyoanzishwa mwaka 2007 kwa lengo la kuwawezesha na kutetea haki za wanawake hususan wenye ulemavu.
No comments:
Post a Comment