Na Anna Nkinda – Perth, Australia
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ni mmoja wa wake wa viongozi wa nchi wanachama wa Jumuia ya madola waliohudhuria mkutano wa siku tatu wa jumuia hiyo unaofanyika mjini Perth nchini Australia.
Wake hao wa viongozi walishiriki ufunguzi wa mkutano huo uliofunguliwa na Malkia Elizabeth wa pili na baada ya ufunguzi waliweza kuendelea na ratiba yao ya kujifunza na kujadili mambo mbalimbali yanayaikabili jamii inayowazunguka ikiwa ni pamoja na afya, elimu, utamaduni, mila na michezo.
Baada ya kumalizika kwa ufunguzi huo walianza ratiba yao kwa kusikiliza mada kuhusu afya ya binadamu ilitolewa na Kanali Dk. Robert Walters ambaye ni Balozi wa Serikali wa afya ya binadamu na Julian Krieg Afisa mtendaji na mwalimu wa jamii katika mpango wa mkoa wa Afya ya binadamu.
Mme wa Waziri Mkuu wa Australia Tim Mathieson aliweza kuwatembeza wake hao wa viongozi maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na makumbusho ya Australia’s Aboriginal and Torres Strait Islander ambako waliweza kujifunza historia ya nchi hiyo pamoja na utunzaji wa mila na utamaduni wao.
“Asili ya wenyeji wa nchi hii ni watu weusi ambao kwa sasa kizazi chao kinatishia kumalizika kutokana na uchache wao lakini miaka ya nyuma Waingereza walihamia hapa na kuzaliana na hivyo idadi yao kuwa kubwa kuliko wenyeji hivi sasa asilimia kubwa ya waustralia ni watu weupe.
Nchi hii inaongozwa na waziri mkuu Julia Gillard’s huku mtalawala wa nchi akiwa ni Malkia wa Uingereza Elizabeth wa pili”, alisema Mathieson.
Katika makumbusho hayo pia walijifunza mila za watu wa Magharibi ya Australia ambao wanaishi kandokando ya Bahari ya Hindi hivyo walifahamu utawala wao, faida wanazozipata hususani za kibiashara na utalii kutokana na matumizi ya bahari na bandari ambayo ni lango kuu la meli.
Waliweza kutembelea bahari ya Hindi na kujionea shughuli za biashara na utalii zinavyofanyika katika ukanda wa pwani, meli kubwa za mizigo zinavyotia nanga, kupakua na kupakia mizigo na kuona jinsi maaandalizi ya mashindano ya kimataifa ya mchezo wa mashua (Sailing World Championships) yanayotarajia kufanyika katika mji huo mwishoni mwa mwaka huu yanavyoendelea.
No comments:
Post a Comment