WAANDISHI wa habari 1,500 wanatarajiwa kushiriki kwenye bonanza la vyombo mbalimbali vya habari litakalofanyika Jumamosi wiki hii ukumbi wa Msasani Beach Club, Dar es Salaam.
Bonanza hilo hufanyika kila mwaka likiandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) na linajulikana kama Media Day Bonanza.
Lengo la bonanza ni kuwaweka pamoja waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa, michezo, uchumi, afya na mambo mengine pamoja na wafanyakazi wa vyombo mbalimbali vya habari, ili kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja.
Maandalizi kuhusiana na bonanza hilo yapo hatua za mwisho, ambapo bendi ya FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’ watatumika kuburudisha washiriki, ambapo shughuli itaanza saa tatu asubuhi hadi saa mbili usiku.
Pia kutakuwepo na wasanii wa muziki wa kizazi kipya ambao tutawatangaza Alhamisi wiki hii, lengo ni kuwa na bonanza tofauti na la miaka ya nyuma.
Mgeni rasmi katika bonanza hili atakuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki na aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta.
Pamoja na mambo mengine, Sitta atakabidhi zawadi za vikombe na medali kwa washindi mbalimbali watakaoibuka siku hiyo, pia atapata fursa ya kuzungumza na washiriki wa bonanza hilo.
No comments:
Post a Comment