Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Saturday, October 5, 2013

TUZO ZA WANAMICHEZO BORA WA TASWA SASA KUTOLEWA DESEMA 20 MWAKA HUU


Katibu Mkuu wa Taswa Tanzania, Amir Mhando (katikati) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo mchana kuhusu sherehe za utoaji wa tuzo kwa wanamichezo bora wa mwaka 2012, zinazotarajia kufanyika hivi karibuni. Kushoto ni Mwenyekiti wa tuzo hizo, Haji Manara (kulia) ni mjumbe wa tuzo hizo, Salum Jaba.
******************************************
CHAMA cha Waandishi wa Habari  za Michezo Tanzania (TASWA), kimekuwa na utaratibu wa kila mwaka kutoa tuzo kwa wanamichezo wanaofanya vizuri na sherehe za utoaji wa tuzo hizo zimekuwa zikifanyika kati ya miezi ya Mei na Juni.

Hata hivyo mwaka huu tuzo hizo zimechelewa kufanyika kutokana na sababu mbalimbali, ambazo zipo nje ya uwezo wa Kamati ya Tuzo, Kamati ya Utendaji ya TASWA, wanachama wa TASWA, wanamichezo husika na wandishi wa habari za michezo kwa ujumla wao.

Ndugu zangu ninyi ni mashahidi wa tuzo za miaka miwili iliyopita, zilivyofana na zikabaki kupigiwa mfano kwa ubora wake.

Lakini mwaka huu, mambo kidogo yalikuwa magumu kutokana na kampuni ambayo sitaitaja jina, ambayo awali ilituhakikishia ingedhamini kwa asilimia 100 lakini ilipata matatizo ya kiuchumi wiki tatu kabla ya tarehe tuliyokuwa tumepanga kufanya tuzo, hivyo wakatuomba tusogeze mbele huenda mambo yangeimarika.

Kuanzia hapo kila mara wakawa wanatuhakikishia mambo yatakuwa mazuri, lakini mwezi Agosti mwishoni wakatupa taarifa rasmi kuwa hawatamudu kudhamini tuzo zetu, hali ambayo ilituchanganya kwa kiasi kikubwa kwani ingekuwa vigumu sana kupata wadhamini wa ghafla kwa wakati huo.

Hata hivyo kutokana na heshima ambayo TASWA imejijengea na kuaminika mbele ya jamii kwa kushirikiana na Kamati ya Tuzo, tukaanza mazungumzo na kampuni mbalimbali na tayari tumepata kampuni mbili za kutusaidia, huku tukiendelea na juhudi zetu za kupata wadhamini wa kutosha kulingana na bajeti yetu.

Leo ninayo furaha kuwatangazia kuwa Desemba 20 mwaka huu, tutafanya Tuzo ya Wanamichezo Bora wa mwaka 2012 katika ukumbi ambao tutautangaza hivi karibuni na maandalizi yamefikia hatua nzuri sana.

Tumefanya vikao kadhaa cha mwisho kikiwa jana kati ya Kamati ya Utendaji ya TASWA na Kamati ya Tuzo, tumetafakari athari za kuchelewa kufanya na zile za kuacha kufanya, tukajiridhisha ni bora tufanye ingawa tumechelewa, lakini lazima tuwaenzi wanamichezo waliofanya vizuri mwaka uliopita.

Tunaomba radhi wanamichezo wanaowania tuzo hizo, vyama mbalimbali vya michezo na wote ambao kwa namna moja au nyingine kuchelewa kwetu kuliwakwaza, lakini hatukuwa na jinsi yote ni katika kuhakikisha tuzo zetu zinakuwa bora kama miaka iliyopita.

Tayari majina ya awali ya wanaowania tuzo kwa michezo mbalimbali tulishayatangaza, ni jukumu sasa la Kamati ya Tuzo kuendelea na mchakato ili kuhakikisha zinakuwa nzuri zaidi.

Ahsanteni
Haji Manara
Mwenyekiti Kamati ya Tuzo
3/10/2013

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...