Asema Simba ina historia Afrika
Aitambia TP Mazembe
MBUNGE wa Singida Mjini Mohamed Dewji (MO), ametamba kuwa ni lazima Simba, itoke na ushindi mnono dhidi ya mabingwa wa Afrika, TP Mazembe ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC).
Pia, ametangaza dau la sh. milioni 50 kwa Simba iwapo itafanikiwa kuibuka na ushindi mnono, utakaoivua ubingwa TP Mazembe na yenyewe kusonga mbele.
Miamba hiyo inatarajiwa kuminyana (kesho) kwenye mchezo mkali wa kuwania kusonga mbele, ambapo katika mchezo wa kwanza Simba ililala kwa mabao 3-1, mjini Lubumbashi .
Dewji, ambaye alipata kuwa mfadhili wa Simba kwa miaka kadhaa, aliwatambia viongozi na wana habari waliotua na msafara wa TP Mazembe, akiwaeleza watarajie kipigo cha mbwa mwizi.
Alikuwa akizungumza na msafara huo katika hoteli ya Kilimanjaro Kempinski, mjini Dar es Salaam , jana usiku ikiwa ni muda mfupi baada ya kutua nchini.
Alisema Simba ni timu kubwa na ina historia nzuri katika michuano ya klabu bingwa Afrika hivyo, wana kila sababu ya kutoka na ushindi katika mchezo huo na kuiondosha TP Mazembe kwenye mashindano.
“Jiandaeni kwa kipigo kesho, tuna historia nzuri na michuano hii hivyo mstarajie kutoka salama, wapo wenzenu waliumia kama itakavyokuwa kwenu” alisema Dewji, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya kusaidia Taifa Stars ishinde.
Dewji aliwapasha wageni hao kuwa watarajie kupata kile kilichowapata Zamalek ya Misri, waliondoshwa na Simba kwenye hatua ya awali ya michuano hiyo.
Zamalek ndiyo walikuwa mabingwa watetezi kama ilivyo kwa TP Mazembe kwa sasa, na kipigo hicho kiliwavua ubingwa huo baada ya kuaga mashindano.
Dewji aliongeza kuwa katika mchezo wa (kesho) leo Simba ina nafasi kubwa ya kufanya vizuri hasa ikizingatiwa kuwa inacheza nyumbani na mashabiki watakuwa wakiipa nguvu uwanjani.
No comments:
Post a Comment