Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, October 30, 2012

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo,kupokea ripoti mikataba ya gesi Novemba 30


Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo
--
Na
Gedius Rwiza
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo atapokea ripoti mikataba ya gesi Novemba 30, akizungumza na Wajumbe wa TPDC Waziri Muhoongo Alisema:

“Nawaombeni wajumbe wote wa TPDC, kuweni makini na mikataba ya utafutaji wa mafuta na gesi, pia naomba mpitie mkataba mmoja baada ya mwingine kwa umakini zaidi na ile yenye utata naomba taarifa kuhusu utata huo,”alisema Profesa Muhongo.

MIKATABA  26  ya utafutaji na uchimbaji wa gesi ambayo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzani (TPDC)kuipitia upya na kutoa ripoti ,ripoti hiyo inatarajiwa kutolewa Novemba 30 mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es salaam jana, Mwenyekiti wa Bodi ya (TPDC), Michael Mwanda alisema kazi inaendelea vizuri na kwamba wanatarajia kutoa ripoti hiyo mwishoni mwa mwezi ujao.

Profesa Muhongo alitaka mikataba  hiyo ipitiwe upya ili kuona kama kuna ambayo ilifanyika kinyume na sheria ili waliohusika waweze kuchukuliwa hatua.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Profesa Muhongo  kuiagiza TPDC kupitia upya mikataba yote iliyokuwa imefanyika na kutoa taarifa ya mikataba yote mibovu.

Akizungumza na gazeti hili  jana, Mwanda alisema kwa sasa zoezi hilo linakwenda vizuri na timu yake inaendelea kuipitia mikataba hiyo 26 na kwamba ana matumaini ifikapo mwishoni mwa Novemba  watakabidhi ripoti kwa Waziri wa Nishati na Madini.

Alisema kamati hiyo ambayo ilipewa kazi hiyo, inafanya kazi kwa makini kama ilivyoagizwa na Waziri, na kwamba wanazingatia muda waliopewa ukifika wawe wamemaliza suala hilo.

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, alifanya mkutano na wajumbe wa bodi ya TPDC, Septemba 15 mwaka huu  na kuwaagiza kupitia upya mikataba ambayo tayari ilishaingiwa na kuwakataza kusaini mikataba mipya hadi pale watakapokuwa wametoa ripoti ya mikataba hiyo.

Waziri alisema kuna mikataba mingi yenye utata katika mikataba hiyo 26 na kuwaomba wajumbe hao kuhakikisha wanaipitia kwa umakini na kwamba ile ambayo itakuwa na makosa wahusika watatakiwa kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria.

“Nawaombeni wajumbe wote wa TPDC, kuweni makini na mikataba ya utafutaji wa mafuta na gesi, pia naomba mpitie mkataba mmoja baada ya mwingine kwa umakini zaidi na ile yenye utata naomba taarifa kuhusu utata huo,”alisema Profesa Muhongo.

Alisema kwa sasa mtu yeyote atakayejihusisha na vitendo vya mikataba ya kifisadi katika wizara yake na mashirika ambayo yapo chini ya wizara watafukuzwa kazi na kufunguliwa mashitaka.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...