Kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima akimtoka mchezaji wa Ruvu Shooting,
Said Dulunga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara
uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Yanga
imeshinda 3-2
Golikipa wa Ruvu Shooting, Benjamin Haule akiokoa moja ya hatari zilizoelekezwa langoni mwake
Kiungo wa Yanga Haruna Niyonzima akiwatoka wachezaji wa Ruvu Shooting
katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara uliofanyika kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo. Yanga imeshinda 3-2. (Picha na
Habari Mseto Blog)
Beki wa Ruvu Shooting, George Otei akichuana na mshambuliaji wa Yanga, Didier Kavumbagu
DAR ES SALAAM, Tanzania
MABINGWA wa soka Afrika
Mashariki na Kati, jana ilibidi wapigane kufa au kupona ili kutoka na pointi tatu
muhimu katika mfululizo wa Ligi Kuu Bara, ilipovaana na maafande wa Ruvu
Shooting ya Pwani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.
Ikitoka nyuma kwa mabao
mawili, Yanga ilipigana kiume na kufanikiwa kuwalaza maafande hao kwa mabao 3-2
na kujikusanyia pointi zilizowasogeza hadi nafasi ya tatu katika msimamo ikiwa
na pointi 14, ikitanguliwa na Azam FC pointi 17 na vinara Simba pointi 18.
Katika mechi hiyo ambayo
Yanga ilicheza ikiwa na jezi za Vodacom zenye nembo ya rangi nyeusi, Ruvu
ilianza kwa kasi na kujipatia bao la kwanza dakika ya tatu, likifungwa na Seif
Abdallah kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu ndogo, baada ya mabeki wa
Yanga kushindwa kuruka naye hewani.
Wakati ngome ya Yanga
iliyokuwa chini ya Mbuyu Twite na Nadir Haraoub ‘Cannavaro’ ikionekana na
kutoelewana, walijikuta wakipachikwa bao la pili mfungaji akiwa huyo huyo
dakika ya tisa.
Ni bao lililotokana na mpira
mrefu wa mlinda mlango Benjamini Haule, aliyepiga kutokea langoni kwake, baada
ya mwamuzi Amon Paul kuamuru ipigwe, akikataa katakata kudanganywa na
mshambuliaji Jeryson Tegete, aliyejiangusha kwenye boksi na na kupewa kadi ya
njano.
Baada ya mabao hayo, Yanga
iliyonekana kukosa uelewano katika safu ya ulinzi, ilijipapatua kusaka mabao na
juhudi zao zikazaa matunda dakika ya 20, baada ya mpira wa adhabu ndogo wa beki
Mbuyu Twite, kwenda moja kwa moja nyavuni.
Tegete ambaye alipoteza
nafasi mbili za wazi za kuisawazishia Yanga dakika ya 30 na 32, alikuja
kusawazisha makosa na kuipa Yanga bao la pili dakika ya 35.
Hadi mapumziko, timu zote
zilikuwa sare ya mabao 2-2, huku Ruvu Shooting wakionekana kutawala mchezo na
kuipa wakati mgumu Yanga.
Dakika ya 63, Didier
Kavumbagu aliipatia Yanga bao la ushindi, akimalizia uokoaji mbovu wa Haule.
Ruvu ikacharuka dakika za
mwisho na kukosa mabao mawili kunako dakika ya 88 na 90, ambapo piga nikupige
langoni mwa Yanga iliishia kugonga mwamba na mpira kuokolewa na kufanya hadi
filimbi ya mwisho matokeo kubaki Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 3-2.
Yanga iliwakilishwa na Yaw
Berko, Juma Abdul/Juma Seif ‘Kijiko’, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’,
Mbuyu Twite, Rashid Gumbo/Shamte Ally, Nurdin Bakar, Haruna Niyonzima, Jeryson
Tegete/Hamisi Kiiza, Didier Kavumbagu na David Luhende.
Ruvu Shooting; Benjamin
Haule, Michael Aidan, Baraka Jaffari, George Otei/Mangasini Mangasini, Ibrahim
Shaaban, Ernest Ernest, Raphael Kyala/Ayoub Kitala, Hassan Dilunga, Seif
Abdallah, Abrahman Mussa na Said Dilunga/Kulwa Mobi.
Huko Tanga, Coastal
Union ‘Wagosi wa Kaya’ waliutumia vema Uwanja wa nyumbani, Mkwakwani kwa
kuwalaza Mtibwa Sugar kwa mabao 3-1.
Coastal ilijipatia bao la
kwanza dakika ya 9, baada ya mpira wa adhabu uliopigwa na Juma Jabu kugonga
besela la kushoto na kujaa nyavuni huku kipa Shabani Kado akiwa hana la kufanya,
kabla ya dakika ya 38, Danny Lyanga kupachika la pili kwa shuti kali la
takribani mita 40.
Mtibwa ilijibu mapigo na
kujipatia bao lake
pekee la kufutia machozi
dakika ya 40, likifungwa na Salum Swedi na dakika ya 82, Lameck Dayton
aliipatia Coastal bao la tatu. Hadi mwamuzi Israel Nkongo anamaliza mpira,
Wagosi waliibuka kidedea kwa mabao hayo 3-1.
Ligi hiyo itaendelea leo, kwa
vinara wa ligi, Simba kupepetana na maafande wa Mgambo JKT, Uwanja wa
Mkwakwani, JKT Ruvu na Oljoro Chamazi Complex wakati maafande wa Tanzania
Prisons watawakaribisha Toto Africans ta Mwanza kwenye Uwanja wa Sokoine
No comments:
Post a Comment