Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Saturday, October 5, 2013

MRADI WA MAJI YA ZIWA VIKTORIA UNA UWEZO WA KUSAMBAZA MAJI MIKOA MITANO


 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe.Rufunga akipanda tanki la maji linalosambaza maji ya Ziwa Viktoria katika miji ya Shinyanga na Kahama,mbele yake akiongozwa na Mkurugenzi wa KASHWASA Ndg.Kivegaro.
 Mkurugenzi wa Mamlaka ya kusambaza maji Kahama na Shinyanga(KASHWASA), Ndg.Clement Kivegaro akiwaonesha wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Shinyanga chanzo cha Maji kilichopo ziwani ambacho ni "Open channel" kutoka ziwa Viktoria.kamati hiyo ilitembelea chanzo hicho Jumatatu hii huko Ihelele wilayani Misungwi mkoa wa Mwanza.
 Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na usalama wakiendelea kuona kazi zinazofanyika ili kuhakikisha wananchi wanaopata maji kutoka chanzo hicho yanakuwa salama kwa matumizi.
Na Magdalena Nkulu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Shinyanga

MAMLAKA ya kusambaza Maji katika miji ya Shinyanga na Kahama (KASHWASA) inayoendesha mradi mkubwa wa maji ambayo chanzo chake ni Ziwa Viktoria,ina uwezo wa kusambaza na kusafirisha maji kwa mikoa mitano kutokana na uwezo mkubwa wa mashine za kusukuma maji pamoja na wingi wa maji.

Hali hiyo imebainika baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Shinyanga ambayo Mwenyekiti wake ni Mkuu wa Mkoa Mhe.Ally N.Rufunga, kutembelea Ofisi kuu za mamlaka hiyo zilizopo Ihelele wilaya ya Misungwi na Jumatatu ya wiki hii,kuona shughuli za uzalishaji na usafirishaji wa maji kutoka kwenye chanzo cha Ziwa Viktoria. 

Changamoto kubwa iliyobainishwa na Mkurugenzi wa KASHWASA Ndg.Clement Kivegaro wakati akisoma taarifa ya mamlaka ni uchache wa watumiaji wa maji ambapo alisema kwa sasa mamlaka inasambaza maji kwa asilimia 13 tu ya uwezo wake hivyo inalazimika kuwasha pampu moja tu ya kusukuma maji, kati ya pampu tatu zilizopo.

Kamati iliweza kutembelea mradi huo kwa muda wa zaidi ya saa 2 na kupata maelezo ya kina juu ya uendeshaji na usambazaji wa maji,ambapo mradi una uwezo wa kuzalisha maji kwa kiwango cha "cubic metres" 120,000 kwa siku.

Mradi unauza maji kwenye mamlaka ya maji Shinyanga( SHUWASA), mamlaka ya maji Kahama (KUWASA) na jumla kamati 45 za maji vijijini.

Mhe.Rufunga wakati akizungumza na wafanyakazi wa mamlaka hiyo amesema, lazima serikali ihakikishe wilaya ya Kishapu nayo inapata maji  ili kupanua wigo wa watumiaji wa maji, na kuhamasisha mikoa mingine kununua maji kutoka chanzo hicho kwa sababu pamoja na uwezo mkubwa wa mradi huo,bado haujatumika ipasavyo kulingana na uwezo wake unaokadiriwa kulisha mikoa zaidi ya mitano.  

Amesema pia kazi ya serikali ni kutafuta fedha ili kushughulikia matatizo yaliyo ndani ya uwezo wa Mkoa kama kuweka mazingira mazuri kwa watumishi wa Mamlaka hiyo kwani chanzo hicho kipo mbali na huduma muhimu kama hospitali, shule na maeneo ya biashara.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...