Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Saturday, July 16, 2011

Msama Auction Mart yaendelea kuwakamata wauza CD feki


NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya udalali ya Msama Auction Mart kwa kushirikiana na jeshi la Polisi, imeendelea kuuvuruga mtandao wa wanyonyaji wa kazi za wasanii wa muziki wa injili,ambapo hivi karibuni imemkamata kiongozi mwingine wa mtandao wa kufanya wizi huo wa kazi za wasanii.
Hiyo ni mara ya pili kwa kampuni hiyo kwa kushirikiana na Polisi kuwakatama wezi hao, ambapo ilifanikiwa kumkamata Mwaku Yahaya baada ya kukamilisha zoezi la kumkamata kiongozi wa juu wa mtandao huo Francis Kamalamu, aliyekuwa akifanya biashara hiyo katika eneo la Ubungo Maziwa, jijini Dar es Salaam.
Mwaku alikamatwa eneo la Ubungo River side akiwa anajiandaa na utaratibu wa kuusafirisha mzigo huo kwenda kwenye mikoa ya Mwanza, Dodoma na Morogoro, ambapo aliwekewa mtego na maofisa wa kampuni hiyo kwa kushirikiana na Polisi.
Alikamatwa akiwa na maboksi yenye CD zaidi ya 600 za wanamuziki tofauti tofauti, ambapo kati ya CD hizo 280 zinasimamiwa na kampuni ya Msama Promotions.
Watuhumiwa hao wamekutwa na CD zilizobeba albamu ya Haleluya Collection,Shengena Gospol Panorama,Mtu wa nne ya Kinondoni revival kwaya pamoja na CD za wanamuziki wa muziki wa kizazi kipya.
Imeelezwa kuwa kampuni hiyo imewasambaza maofisa wake katika mikoa mbalimbali ili kuhakikisha wanawakamata watu wote wanaotumia kazi za wanamuziki wa Injili kujinufaisha.
Imewekwa wazi kuwa mikoa ambayo imeonekana kuwa na wezi sugu kazi za wasanii ni Arusha,Kilimanjaro, Mbeya, Morogoro,Dar es Salaam,Iringa, Tanga,Mwanza, Pwani na Dodoma.
Mtuhumiwa huyo anatarajia kufikishwa Mahakamani leo, mara baada ya uchunguzi wa kina juu ya wizi huo kukamilika, ambapo imewekwa wazi kuwa msako huo utaendelea.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...