Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Sunday, July 10, 2011

Tamko La Mbunge Wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, Kwa Waandishi Wa Habari Kuhusu Kushikiliwa Kwake Na Polisi

|

Mbunge wa Mbeya Mjini-Chadema Mheshimiwa Joseph Mbilinyi
------
Jana tarehe 8 Julai 2011 Polisi walinikamata kwa kile walichokiita kuwa ni kufanya mkutano bila kibali.Hata
hivyo, mtiririko wa matukio unaonyesha kwamba polisi walisukumwa na sababu nyingine kwa kuwa suala la
taarifa kupelekwa polisi kama sheria zinavyohitaji lilishashughulikiwa na viongozi wa CHADEMA mkoa na
wilaya ya Mbeya Mjini.


Leo tarehe 9 Julai 2011 pamoja na kutolewa kwa dhamana polisi wameonyesha nia ya kutaka kuzuia tamasha la wazi la bure ( ‘Burudani Nyumbani’) ambalo wasanii mbalimbali walikuwa walifanye kwa mwito wangu kwa ajili ya kutoa burudani na kuhamasisha maendeleo. Polisi wameonyesha vitendo vya kutaka leo kufanyike tamasha la fiesta pekee wakati ambapo matamasha haya yote mawili yameandaliwa na wadau tofauti katika maeneo tofauti.

Mpaka wakati huu ninapotoa taarifa hii wananchi wengi wamejikusanya katika uwanja wa Ruanda Nzovwe ambao ni maarufu kama Uwanja wa Dr Slaa wakisubiri tamasha hilo lakini polisi wameonyesha dhamira ya kutaka kuwatawanya.

Maneno na vitendo vya Jeshi la Polisi vinaelekea kuwa na uhusiano na kauli ambayo niliitoa hivi karibuni kupitia mtandao wa Facebook ya kutohitaji tamasha la Fiesta kufanyika Mbeya.Katika mazingira haya ni muhimu nikaeleza tu kuwa kauli yangu kuhusu Fiesta ilikuwa na madhumuni ya kuanzisha mjadala kuhusiana na suala zima la wizi na unyonyaji uliopo kwenye Sanaa, ambao sio tu unawanyima haki Wasanii, bali pia kukosesha mapato kwa Serikali ambayo yangetokana na kodi kupitia Sanaaikiwemo muziki.

Nilifanya hivyo baada ya tamasha hilo kutangazwa kufanyika katika eneo ambalo wananchi wamenipa wajibu
wa uongozi wa kuwatumikia na kuwawakilisha. Hivyo kwa niaba ya wananchi wa Mbeya Mjini wanaokosa mapato katika sanaa na wasanii wa Mbeya wanaokosa fursa kutokana na vikwazo nilichukua uamuzi wa kuwakilisha kupaza sauti kama ambavyo nimekuwa nikipaza sauti katika masuala mengine yanayogusa umma kama viwanda, kilimo, barabara za Mbeya Mjini na Haki zawanafunzi wa Elimu ya Juu pamoja na makundi mengine katika jamii.

Niliamua kupaza sauti katika hili kupitia Fiesta, kwa kuwa waandaji wake kimsingi ni sehemu ya vyanzo vya maovu kwenye maendeleo ya muziki hapa nchini. Fiesta ikiwa kitovu cha uonezi kwani hata Wasanii wanaoshiriki halipwi ipasavyo au hawalipwi kabisa. Na hii ni kutokana na wao kutumia njia haramu kuhodhi (monopolise) biashara ya muziki hapa nchini, huku wakiwanyima nafasiwatanzania wengi kutumia vipaji na ubunifu wao kwenye biashara ya muziki.Waandaji wa Fiesta ndio wenye redio ya Clouds, Kampuni ya promotion ya Primetime, na pia wanahusika na N.G.O ya THT, waandaji wa matamasha ya injili, ikiwemo kuwa na ushirika katika Tamasha la Pasaka.

Huku wakiwa na ushawishi wa hila kwenye Kili Music Awards (One Call Promotion) na mambo mengine
yote muhimu yanayohusu Sanaa. Ikiwemo ujumbe wa bodi kwenye Tamasha la majahazi, Zanzibar. Lisingekuwa jambo baya kama wangetumia nafasi hizo kwa haki na maendeleo ya sanaa.

Kutokana na haya, kwa miaka mingi himaya (“empire”) hiiimetumia nafasi yake dhalimu kukandamiza watu wengine hasa Wasanii. Kwa mfano kama Msanii hayupo kwenye hiyo “himaya” yao basi hana nafasi ya kutimiza ndoto yake. Na iwapo Msanii hakubaliani na taratibu zao au malipo finyu wanayowalipa Wasanii, basi watahakikisha wanampiga vita na hatimaye kuhujumu usanii wake ili atoweke, kwa kuwa tu hakubaliani nao.

Msanii hana haki ya kufanya majadiliano ya kibiashara mbele yao. “Empire” hii imehodhi mpaka makampuni ya udhamini hapa nchini, ambapo makampuni haya yamekuwa magumu kutoa udhamini kwa wadau wengine kwa kuwa tu wao ni washirika wa “Empire” hii. Walifikia hatua ya kuhodhi mpaka biashara ya usambazaji kwa “Wadosi” ambapo bila ya wao kuruhusu basi Msanii yeyote kazi yake haipewi nafasi ya kusambazwa wala kusikika.

Hata kama nyimbo au album yake ni nzuri kwa kiasi gani.Kibaya zaidi wamehodhi mpaka nia njema ya Rais Kikwete katika kusaidia Sanaa na Wasanii. Mfano ni Studio ambayo Rais kupitia Bunge Tukufu la Jamhuri ya
Muungano alitangaza kuwa amewapa Wasanii wa Tanzania, lakini baadaye tukashangaa kusikia ipo
mkononi! Pia Rais aliahidi na kutoa nyumba ya Serikali kwa Wasanii ambayo ingetumika kuendeshea Studio
husika, lakini nyumba hiyo ya Serikali iliyotolewa na Rais sasa iko chini yao na ndio makao ya THT! Wamefanikiwa kumhadaa Rais kuwa wao ndio “Care takers” wa Sanaa ya Tanzania akawaamini na wao wanaitumia vibaya imani njema ya Rais kwao kufanya dhuluma.

Yote niliyoyataja juu, japokuwa hayo ni kwa uchache tu! Yanalalamikiwa sana na wasanii wengi na wadau hapa nchini, japokuwa wengi wameshindwa kujitokeza waziwazi kutoka na vitisho vya watu hawa. Vitendo hivyo wanavyofanya vimeleta madhara katika tasnia ya sanaa na matokeo yake ni kudumaa kwa maendeleo ya muziki hapa nchini. Vijana wengi wanaojihusisha na sanaa wamepoteza matumaini. Wengi walipata tegemeo la ajira kupitia muziki, lakini hali haipo hivyo tena. Vijana wengi wasanii wamekata tamaa kwa ajili ya ukandamizaji wa “empire” hii.

Na sio tu wasanii na wadau wengine wanawapoteza katika hili. Kwa watu hawa kuhodhi na kuvuruga kabisa biashara ya muziki, hata Serikali inapoteza fedha nyingi kupitia kodi. Kwa mujibu wa utafiti wa Dr. Jehovaness Aikaeli ambaye ni mchumi wa UDSM, hata katika hali hii mbaya ya biashara ya muziki, Serikali imepoteza Tsh. Milioni 18,kwa kutokusanya kodi kupitia muziki tu, ukiachilia mbali filamu na sanaa nyingine.

Na iwapo hali itaboreshwa basikodi hiyo itapanda mpaka wastani wa Tshs. Bilioni 50 kwa mwaka! Hizi sio pesa kidogo kwaserikali, hasa ukizingatia bajeti ya Wizara inayohusika na Utamadnuni ni Tsh bilioni 14, kwa mwaka, fedha ambazo mara nyingi hawapewi zote kutokana na Serikali kutokuwa na fedha ya kutosha! Lakini hapa utaona kukwa kodi ya mwaka peke yake ingetosha kwa bajeti ya Wizara na ziada kubwa
ingebaki kwa miradi ya maendeleo kama kujenga Art Theatres n.k Napenda ieleweke wazi kwamba mimi binafsi ni “Mhanga” au “victim” wa uharamia wa “himaya” hii kwa miaka

mingi, tukupitia migogoro kadhaa ya kibiashara lakini kilichonisikuma kuchukua hatua hii; sio nafsi yangu pekee bali wajibu nilionao hivi sasa kama mwakilishi umma.Izingatiwe kuwa baada ya mimi kuchaguliwa kuwa Mbunge na wananchi wa Mbeya tena kwa kishindo, Serikali kupitia Wizara inayohusika na utamaduni na pia Baraza la Sanaa (BASATA), walinipongeza kwa barua huku wakinitaka niendelee na harakati za kupigania sanaa na wasanii kwa kutumia nafsi au jukwaa langu jipya Bungeni na nje ya Bunge. Jukumu ambalo nililikubali kwa mikono miwili kwani harakati za muziki huu si kitu kipya kwangu, ulianza kabla ya Ubunge na ndio ninachokifanya na hasa ukizingatia mimi pia sasa ni Waziri Kivuli

(Shadow Minister) wa Wizara ya Habari, Vijana na Michezo.

Kwa lugha nyingine ujumbe nilioutoa wa kukataa Fiesta ni ishara ya mgomo wenye nia ya kutuma ujumbe wa madai ya msingi. Na historia inaonyesha kuwa, Wasanii wa Nigeria walianza kulipwa vizuri kama wanavyolipwa sasa baada ya kuanzisha migomo dhidi ya mapromota wanyonyaji wa nchini kwao.Na kama ni suala la kukuzauchumi na ajira, Ni nini mchango wa Fiesta na matamasha mengine kwa halmashauri za mji na majiji wanayopita na kuvuna mamilioni ya fedha kila siku?

Wenu katika kutaka haki,
Joseph Mbilinyi (Mb)
9/7/2011-Mbeya Mjini
http://mjengwa.blogspot.com/

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...