Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Sunday, January 26, 2014

Logarusic katika mtihani wa kwanza Ligi Kuu Bara


Logarusic kocha wa Simba

BAADA ya kutua kwa mbwembwe na kuiwezesha Simba kunyakua taji la Nani Mtani Jembe kisha kulikosa kiduchu Kombe la Mapinduzi, Kocha Logarusic Zdravko ataanza rasmi kibarua chake katika  Ligi Kuu Tanzania Bara leo wakati vijana wake watakapovaana na Rhino Rangers.
Kocha huyo kutoka Croatia, aliajiriwa Simba kwa mkataba wa miezi sita kuchukua nafasi ya Abdallah Kibadeni 'King' aliyeiwezesha timu hiyo kushika nafasi ya nne kwenye hatua ya duru la kwanza la ligi hiyo iliyokuwa imesimama na kuanza rasmi jana kwa mechi kadhaa.
Hivyo pambano la Simba na Rhino litakalochezwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni mtihani wa kwanza kwa kocha huyo ambaye mechi zake mbili zilizopita alishuhudia vijana wake wakigaragazwa.
Baada ya kushinda mfululizo, Simba ilisimamishwa na KCCA ya Uganda kwa kufungwa bao 1-0 kwenye pambano la fainali za Kombe la Mapinduzi lililochezwa mjini Zanzibar kabla ya wiki iliyopita kulazwa tena 1-0 na Mtibwa Sugar katika pambano la kirafiki lililochezwa jijini Dar.
Lugarusic aliingia Msimbazi kwa kismati kwa kuitandika KMKM ya Zanzibar kwa mabao 3-1 kabla ya kupata ushindi kama huo kwa Yanga na baadaye kwenda Zenji na kufanya vema kabla ya kufungwa na KCCA.
Simba itaikaribisha Rhino waliotoshana nao nguvu kwa kutoka sare ya 2-2 mjini Tabora katika mechi yao ya awali, ikiwa na nyota wapya watano, Donald Musoti wa Kenya, Ivo Mapunda, Ali Badru aliyekuwa Misri, Awadh Juma wa Mtibwa na kipa Yew Berko wa Ghana.
Pia itakuwa na kiungo wake wa zamani, Uhuru Suleiman aliyekuwa akiichezea Coastal Union kwa mkopo kwenye duru la kwanza ambaye ataungana na wakali wengine kuanza mbio za kuufukia ubingwa wa ligi hiyo unaoshirikiliwa na watani wao Yanga.
Mbali na mechi hiyo ambayo mashabiki wana hamu ya kutaka kuona Simba chini ya kocha Logarusic wataanza vipi, pia leo kuna pambano jingine ambalo litazikutanisha timu za maafande wa JKT Ruvu itakayoikaribisha Mgambo JKT ya Tanga kwenye uwanja wa Chamazi.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena siku ya Jumatano kwa mechi tano ambazo zitazikutanisha timu 10 ambapo moja ya mechi hizo ni Kagera Sugar itakuwa nyumbani kwao mjini Bukoba kuikaribisha 'ndugu' zao Mtibwa Sugar.
Michezo mingine ya siku hiyo ni ile ya Azam Fc dhidi ya Rhino Rangers, Ruvu Shooting kuialika Mbeya City kwenye uwanja wa Mabatini huku watetezi Yanga 'Wazee wa Uturuki' watawafuata Coastal Union iliyokea Oman katika jiji la Tanga.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...