Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, January 14, 2014

WANANCHI UKONGA WAGOMEA FIDIA KIDUCHU BOMBA LA GESI


Mwenyekiti wa Kamati ya kufatilia malalamiko ya wananchi wa mji mpya relini Bw. Omari Msusa kushoto akihojiwa na vyombo vya habari kuhusu fidia wanayotakiwa kulipwa huku Mbunge wa Jimbo la Ukonga Dar es Salaam, Bi,Eugen Mwaiposa akimsikiliza kwa makini (Picha na Mpiga Picha Wetu)

mbunge wa jimbo la Ukonga Dar es salaam, Bi,Eugen Mwaiposa (kulia) akisikiliza malalamiko ya wananchi wea eneo la Mji Mpya Relini jimboni kwake jana wakilalamika kutaka kulipwa fidia ndogo ambazo hazilingani na thamani ya nyumba zao (Picha na Mpiga Picha Wetu)

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mjipya Relini,Ilala Dar es Salaam Bw. Geofrey Chacha (aliyesimama) akitoa malalamiko ya wananchi mbele ya mbunge wa Jimbo la Ukonga, Bi. Eugen Mwaiposa wa pili kushoto wanaolalamikia kuhusu tahmini ya fidia ndogo inayopitishwa ili kupisha upanuzi wa bomba la gesi linalotoka Mtwara. (Picha na Mpiga Picha Wetu)
Na Mwandishi wetu
WANANCHI wa Mji mpya Relini wilaya ya Ilala waliopitiwa na mradi ya bomba la gesi ya Mtwara wamemuomba Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Bi. Eugen Mwaiposa awasilishe bungeni hoja ya kukataa mradi huo kutokana na kupunjwa fidia ya nyumba na mali zao wanayotakiwa kulipwa.
Wakizungumza na kutoa maazimio hayo katika mkutano wa dharura walioitisha na kuhudhuriwa na mbunge wao, wananchi hao walisema awali walikubali mradi huo kwa manufaa ya taifa lakini baada ya kuletewa dodoso la kutathmini mali na nyumba zao wamegundua kuna ujanja unatumika kuwanyima haki na kuwafanya kuwa masikini maisha yao yote.
Waliendelea kudai kuwa mpaka sasa hawajui serikali imemkabidhi nani jukumu la kuthamini nyumba zao kwani kampuni nyingi za ujanja ujanja zimejitokeza kutaka kuwathamini lakini kwa kiwango cha chini ambacho hakiwezi kumpatia makazi mengine.

Bw. Josephat Haule alisema waathirika wenzao katika Kata za Kivule, Pugu Kwalala na Mbande wao wamethaminiwa vizuri na wanatarajia kupata fedha za kujenga nyumba nyingine kutokana na gharama kuwa juu lakini wao nyumba iliyojengwa kwa sh. mil 57 anathaminiwa alipwe sh. mil. 11 na nyumba zenye thamani ya sh. mil. 10 wanataka alipwe sh, mil 3.
Bw. Robert Pius alisema kutoka taarifa ya Serikali itolewe ya kutangaza kupitisha bomba la gesi eneo hilo waathirika wote walisimamisha uendelezaji wa makazi hayo na kusubiri kupewa haki zao lakini ni mwaka wa pili sasa hakuna taarifa zenye ukweli zinazowafikia hivyo kuwafanya waishi kama wanya aina ya digidigi porini,
Mbunge Mwaiposa akizungumza na wananchi hao aliahidi kushirikiana nao kujua ukweli wa kampuni gani iliyopewa jukumu la kuthamini nyumba na mali zao kwani anachofahamu ni kuwa Kampuni ya Kilwa Energy iliyopewa jukumu hilo awali hakiwa na uwezo wa kifedha kuwalipa wananchi kwa wakati.
Aliahidi kushirikiana na Kamati ya wananchi hao kushughulikia madai yao kwenda Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwenda kumuona Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwenda kumuona Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na ikishindikana wanakwenda kumlalamikia Rais Jakaya Kikwete.
Alisema wananchi wanateseka kwa vile kuhamisha makazi kutoka sehemu moja kwenda nyingine kunarudisha maendeleo nyuma na kama anavyofahamu Serikali ya Rais Kikwete ni sikivu na yenye kufanya kazi kwa ufasaha hajui sababu za wananchi wake kushindwa kutimiziwa ahadi zao katika kiwango kinachostahili.
"Wananchi wangu wanadhiki, wanashida ya fedha lakini si kwa malipo kidogo kiasi hicho, tunapiga picha tuoneshe umma thamani ya nyumba na kiasi wanachotakiwa kulipwa ili wakaendelee na maisha yao sehemu nyingine" alisema Bi. Mwaiposa.

Bi. Mwaiposa alikiri kuona nyumba zilizothaminiwa kwa fedha kidogo ambazo haziwezi kununua kiwanja kingine ambavyo kwa sasa katika maeneo hayo vinauzwa kati ya sh. mil. 10 mpaka sh. mil. 15 kwa kiwanja cha nusu hekari.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...