Na Mwandishi Maalum, Abuja.
Wake
wa Marais wa Afrika wametakiwa kuwajengea uwezo wanawake na watoto wa
kike kwa kuhakikisha kuwa wanapata elimu ya kutosha ambayo itawawezesha
kushika nafasi za juu katika uongozi na hivyo kupunguza ukatilia wa
kijinsia dhidi yao.
Wito
huo umetolewa jana na Rais wa Malawi Joyce Banda wakati akifungua
mkutano wa saba wa wake wa marais wa Afrika uliozungumzia masuala ya
amani barani Afrika uliofanyika mjini Abuja nchini Nigeria.
Rais Banda alisema kuwa ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto ni
matokeo ya kukosekana kwa elimu na amani katika nchi, jambo la muhimu
ni kuwajengea uwezo wa kielimu na kiuchumi ili waweze kutambua haki zao
za msingi.
“Kila mmoja wenu katika nchi yake anafanya kazi ya kuhakikisha kuwa
watoto wa kike wanapata elimu lakini hiyo pekee haitoshi bali mnatakiwa
kuweka nguvu zaidi katika kuimarisha amani ndani ya nchi zenu kwani bila
nchi kuwa na amani ukatili wa kijinsia utazidi kuendelea”, alisema
Banda.
Rais Banda aliendelea kusema kuwa wanawake wapewe nafasi katika
usuluhishi na utatuzi wa migogoro wasiachwe wanaume peke yao kufanya
kazi hiyo kwani nchi ikikosa amani waathirika wakuu ni wanawake na
watoto ambao wengi wao wanauawa na wengine wanafanyiwa ukatili wa
kijinsia ikiwemo kubakwa.
Kwa upande wake Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan alisema kuwa nchi za
Afrika lazima zifanye jitihada kubwa za kuondoa vikwazo ambavyo
vinawazuia wanawake na watoto wa kike kushindwa kutimiza ndoto zao.
Wanawake wanatakiwa kutobaguliwa bali kupewa fursa sawa ya kushiriki
katika elimu, siasa na uchumi.
Aliendelea kusema kuwa usawa wa kijinsia unatakiwa kuwepo barani Afrika
kwa kuunga mkono na kutengeneza mazingira ya kuwainua wanawake kiuchumi
na kuhakikisha kuwa wanawake hao wanaishi mazingira salama.
No comments:
Post a Comment