RAIS
Kikwete amezindua mradi mkubwa wa maji wa Uwanja mpya wa Ndege wa Swaya
mkoani Mbeya, huku akivirushia madongo kwa vyama vya upinzani kuwa
vinafikiria kuanzisha ugomvi kila siku badala ya kuhamasisha maendeleo.
Rais Kikwete alisema atahakikisha
anatekeleza ahadi zake zote alizoahidi wakati wa kampeni mwaka 2010 na
kuhoji vyama vya upinzani vitawaeleza nini wananchi wakati wa uchaguzi
mkuu mwaka 2015.
Akizungumza na wananchi wa Mbeya kwenye
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uzinduzi wa mradi mkubwa wa Maji
Safi na Usafi wa Mazingira uliopo Swaya, Rais Kikwete alisema kuna
vyama vya siasa vya upinzani vinafikiria kuanzisha ugomvi.
Ingawa Rais Kikwete hakutaja jina la
chama, lakini ni dhahiri kwamba alikuwa akikilenga chama kikuu cha
upinzani nchini cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho ndani na
nje ya Bunge kimejikuta kwenye mvutano na serikali kwenye masuala
kadhaa yanayohusu maslahi ya taifa.
“Wengine wanatafuta ugomvi kila siku
badala ya kuhamasisha maendeleo tuone mwaka 2015 watawaeleza nini
wananchi, sisi chama chetu kinawahudumia wananchi wakati wengine
wanawazuia wasiende kwenye miradi ya maendeleo, ikifanikiwa wao
wanakuwa wa kwanza kuhitaji huduma wakati hawakushiriki kuhamasisha,”
alisema Rais.
Akizungumzia mradi huo mkubwa wa maji
uliogharimu sh bilioni 79.5, Rais Kikwete alisema umejengwa kwa
ufadhili kutoka nchi za Jumuiya ya Ulaya iliyotoa sh bilioni 36.9,
Ujerumani sh bilioni 13.5 na serikali sh bilioni 29.1 kupitia programmu
yake ya maji.
Pia aliwaonya wananchi kuacha tabia ya
kuharibu vyanzo vya maji na kuagiza kuwa wanapaswa kuvilinda na
kuhifadhi miundombinu ya maji na kuvitaka vyombo vya dola kuwachukulia
hatua wananchi watakaoshikwa wakiiba vifaa vya maji ambavyo
vimenunuliwa kwa gharama kubwa.
Katika uzinduzi huo ulioshuhudiwa na
Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Klaus Brandes, alisema kuwa nchi yake
imekuwa ikishirikiana na serikali tangu mwaka 1973 katika miradi
mbalimbali ya maendeleo na itaendelea kufanya hivyo kutokana na
ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Naye Kamishina wa Maendeleo ya Jumuiya
ya Ulaya, Andris Piebalgs, alisema kiasi hicho cha fedha kilichotolewa
na jumuiya hiyo, kimesaidia kukamilisha mradi huo.
Uwanja wa Ndege wa Songwe
Kwa mara ya kwanza, Rais Kikwete jana
alitua rasmi kwenye Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Songwe mkoani Mbeya
akiwa kwenye ndege aina ya Forker 28 akiongoza msafara wa watu 31.
Kitendo cha Rais Kikwete kutua kwenye
uwanja huo uliokamilika asilimia 95, kulimuongezea furaha zaidi katika
ziara yake ya kuzindua mradi wa maji.
Baada ya kutua kwenye uwanja huo majira
ya saa 5.15 jana, rubani wa ndege hiyo, Kapteni Dominick Boman,
akiongozwa na Meneja wa Uwanja wa ndege wa Mbeya ilipotua, Valentine
Kadeha, aliusifia kuwa una sifa zote za kurusha ndege kubwa zinazobeba
abiria na kuhoji kwa nini haujaanza kutumika.
“Uwanja ni mzuri sana, sehemu ya kurukia
ndege ni pana na uwanja ni mrefu hakika wananchi wana kila sababu ya
kuufurahia, sijui kipi kinakwamisha kuanza kutumika kwa abiria labda
vituo vya mafuta havijajengwa, suala la sehemu ya kushukia abiria si
tatizo; marubani tunahitaji uwanja mzuri,” alisema Bomani.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege, Suleiman Suleiman, alisema uwanja huo utaanza kutumika rasmi Novemba Mosi.
No comments:
Post a Comment