Na Zitto kabwe
Katika
mkutano wa Kumi wa Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Spika wa Bunge ndugu Anna Makinda alitangaza mabadiliko kadhaa ya muundo
wa Bunge katika Kamati mbalimbali za Bunge. Moja ya maamuzi ya Spika
yalikuwa ni kufutwa kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma
ambayo inajulikana kifupi kama POAC. Maamuzi haya yameleta sintofahamu
kwa wananchi wengi na wafuatiliaji wa masuala ya Bunge na Uwajibikaji
katika nchi yetu.
Ni
muhimu tufahamu uundwaji wa POAC ulitokana na misingi gani na kwamba
Uamuzi wa Spika unarudisha nyuma maendeleo makubwa ya kujenga Bunge
imara na lenye meno. Maamuzi ya Spika ni kinyume cha kanuni za Bunge,
sheria ya Ukaguzi na Katiba ya nchi. Maamuzi ya Spika yanavuruga
Bunge,ni ya hovyo na yanapaswa kupingwa na kila mdau wa Uwajibikaji
nchini.
Baada
ya Tanzania kuingia kwenye zoezi la Ubinafsishaji, mashirika mengi ya
Umma yaliuzwa na mengine kufa kabisa. Wakati huo kulikuwa na chombo
kinaitwa SCOPO (Standing Committee on Parastatal Organisations) kwa
madhumuni ya kusimamia uendeshaji wa Mashirika ya Umma. Bunge lilikuwa
na Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma na kamati hiyo ilifutwa mwaka
1997 kufuatia hatua za ubanifsishaji na ukweli kwamba Mashirika ya Umma
hayatakuwapo na hivyo hapakuwa na haja ya kuwapo kwa kamati hiyo.
Mwenyekiti wa mwisho wa Kamati hiyo alikuwa ni Mzee William Shellukindo
wakati huo akiwa Mbunge wa Jimbo la Bumbuli wilayani Lushoto mkoani
Tanga.
Mwaka
2007, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alifanya mkutano
wa Uwajibikaji na kueleza Taifa kuwa kimsingi Mashirika ya Umma bado
yapo na mahesabu yao, kwa kuwa hayaangaliwi, ni mabaya sana nafedha za
umma zinapotea. Pia alieleza kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ibara ya 143(5) inamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali kutoa taarifa za Ukaguzi za Mashirika ya Umma (Public
Authorities and Other Bodies).
Hivyo
aliomba Bunge liunde Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma ili liweze
kupokea, kujadili na kutoa maelekezo kuhusu mahesabu ya Mashirika ya
Umma na kusimamia ufanisi wa Mashirika ya Umma.
Vile
vile alishauri Kamati hiyo isimamie sera ya Ubinafsishaji wa Mashirika
ya Umma. Spika wa Bunge wa wakati huo, kupitia Kamati aliyoiunda chini
ya Job Ndugai (wajumbe wengine walikuwa dkt Willibrod Slaa, Beatrice
Shelukindo, Hamad Rashid Mohammed na Nimrod Mkono) wakaunda Kamati ya
Bunge ya Mashirika ya Umma kwa mujibu wa Kanuni za Bunge za Mwaka 2007.
Kamati
ya POAC iliundwa rasmi mwaka 2008 mwezi Februari. Nilipewa dhamana ya
kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Kamati hii. Sababu za kuanzishwa kwa kamati
ya POAC bado zipo na kimsingi sababu hizo ni za maana sana sasa kuliko
ilivyokuwa kabla.
Majukumu
ya POAC yaliainishwa na sehemu ya tatu ya nyongeza ya nane ya Kanuni za
Bunge toleo la mwaka 2007, kanuni ya 115 (13)(a-e). Majukumu hayo ni
pamoja na kushughulikia mahesabu yaliyokaguliwa ya Mashirika ya Umma,
kuainisha maeneo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za Umma, kutathmini
ufanisi wa Mashirika ya Umma na kufuatilia utekelezwaji wa sera ya
ubinafsishaji wa mashirika ya Umma.
Kuanzia
mwaka 2008 Mdhibiti na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali
amekuwa akitoa taarifa za mahesabu ya mashirika kama Katiba ya nchi
inavyomtaka na sheria ya ukaguzi ya mwaka 2008. Sheria hii imeitaja
kamati ya POAC kama moja ya kamati zenye majukumu ya kuwasilisha Bungeni
taarifa ya mwaka ya mahesabu ya Mashirika ya Umma.
Katika
kipindi cha miaka mitano POAC imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa
umahiri na kwa kweli kwa uwazi sana kuliko kamati nyingine zote za
Bunge. Taarifa ya mwisho ya POAC katika Bunge iliyowasilishwa katika
mkutano wa saba wa Bunge, mwezi Aprili mwaka 2012 ulipelekea kutolewa
kwa hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu ambayo ilisababisha
mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri.
Hatua
hii ilikuwa ni hatua muhimu sana katika kuweka mizizi ya utamaduni wa
uwajibikaji nchini kwetu. Wakati Kamati inajiandaa na Taarifa yake ya
Mwaka 2012 kwenye Mkutano wa Kumi na Moja, Spika ameivunja. Ikumbukwe
maagizo ya mwisho ya Kamati ya POAC yalikuwa ni kuzuia mifuko ya hifadhi
ya jamii kutoa mikopo kwa Serikali bila ya kuwapo kwa mikataba.
Hivi
sasa Serikali imekopa zaidi ya shilingi 1.2 trilioni kutoka mifuko ya
Hifadhi ya Jamii kwa ajili ya miradi mbalimbali, mikopo hiyo ya fedha za
wafanyakazi haina mikataba yeyote na POAC iliona hatari ya fedha za
wafanyakazi kupotea na kuleta madhara makubwa kwa wastaafu nchini.
Katika
maelezo yake Spika amesema nchi nyingine duniani hazina kamati kama ya
POAC. Nadhani waliomshauri Spika waliamua kumdanganya na yeye
akadanganyika. Nchi zote za Afrika Mashariki zina Kamati ya kusimamia
Mashirika ya Umma. Kenya inaitwa Public Investments Committee, Uganda
inaitwa State Corporations Committee na hata nchi nyingine kama India
ambazo zinafuata utamaduni wa kibunge kama wetu wanayo na wanaita Public
undertakings Committee.
Nchini
Afrika Kusini sio tu kuna Kamati ya Mashirika ya Umma bali pia kuna
Wizara inayosimamia Mashirika ya Umma (Ministry of Public Entreprises).
Kimsingi Kamati ya POAC ilipaswa kuongezewa nguvu zaidi ili kufikia
uwezekaji wa Serikali kwenye makampuni binafsi badala ya kuifuta.
Uwezekaji wa Serikali kwenye makampuni kama BP, AirTel, Kilombero Sugar,
SonGas nk hauna uangalizi wowote.
Uamuzi
wa Spika wa Bunge kuifuta Kamati ya POAC ni uamuzi unaorudisha nyuma
juhudi za nchi kujenga asasi za uwajibikaji, ni kinyume cha sheria ya
ukaguzi wa umma inayotaja Kamati tatu za Bunge za kusimamia fedha za
Umma na ni kinyume cha Katiba ya nchi.
Spika
wa Bunge anasema kazi za Kamati ya POAC zitafanywa na Kamati ya PAC;
Tanzania ina jumla ya Mashirika ya Umma 258 yenye thamani ya shilingi
trilioni 10.2 mpaka mwezi Juni mwaka 2012, hata kamati ya POAC ilikuwa
haiwezi kushughulikia Mashirika yote ya Umma katika mwaka mmoja, PAC
itawezaje kusimamia Wizara za Serikali, Mikoa na wakala za Serikali na
wakati huo huo Mashirika ya Umma 258? Kwa vyovyote vile Taifa linarudi
miaka ya kabla ya 2008 ambapo Mashirika ya Umma yalikuwa kichaka cha
kuiba fedha za Umma. Hivi karibuni Kamati ya POAC iligundua mtindo wa
Wizara za Serikali kupeleka fedha Serikali kwenye Mashirika na kutumia
kifisadi ili kukwepa ukaguzi kwenye Wizara (Wizara ya Utalii ilipeleka
zaidi ya shilingi 600 milioni Bodi ya Utalii mwaka 2010/2011).
Ikumbukwe
pia wizi wa EPA, MEREMETA na hata uuzaji holela wa baadhi ya mali za
Serikali kupitia ubinafsishaji ulifanyika nyakati ambazo Bunge halina
kamati inayosimamia Mashirika ya Umma.
Kwa
vyovyote vile Spika wa Bunge amedhihirisha namna ambavyo anafanya
maamuzi bila kuzingatia maslahi ya nchi wala kuzingatia historia ya
uwajibikaji katika nchi. Namna mijadala ya Bunge inavyoendeshwa, namna
anavyobeba ajenda za Serikali katika kujenga Bunge kibogoyo na namna
anavyofanya maamuzi kwa kukurupuka, inahitaji hatua za kuokoa misingi ya
uwajibikaji wa nchi.
No comments:
Post a Comment