Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, October 15, 2013

KINYOGOLI: MTAMBO WA 'KUTENGENEZA' MABONDIA TANZANIA ANAE MKUMBUKA MWALIMU NYERERE


Habibu Kinyogoli kulia aliyeshika kikombe akiwa na Mfaume Kawawa Simba wa Yuda baada ya kutoka katika mashindano ya All African Game 1973. Picha zote kwa hisani ya   www.superdboxingcoach.blogspot.com.


Kinyogoli akimnoa Rashid Matumla

Kinyogoli akimwelekeza bondia Ibrahim Class
 

Habibu Kinyogoli akimfundisha bondia chipukizi wa kike, Lulu Kayege jijini Dar es Salaam.

Habibu Kinyogoli kulia aliyeshika kikombe akiwa na Mfaume Kawawa Simba wa Yuda baada ya kutoka katika mashindano ya All African Game 1973. Picha zote kwa hisani ya   www.superdboxingcoach.blogspot.com.


Na Daniel Mbega

UNAPOLITAJA jina la Habibu 'Master' Kinyogoli unakuwa kama umetaja jina la 'Chuo Kikuu kinachotoa Shahada ya Juu ya Ndondi nchini Tanzania'. Ni sawa na unapotaja timu ya soka ya Pamba ya Mwanza, ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikijulikana kama 'Chuo Kikuu cha Soka Tanzania' kutokana na kutoa wanasoka wengi mahiri waliotamba katika klabu mbalimbali zikiwemo Simba na Yanga pamoja na timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars.
Katika Afrika, ukitaja jina la Zaiko Langa Langa moja kwa moja unakuwa unazungumzia Shule ya Muziki barani humu, ambayo ndiyo iliyotoa wanamuziki wengi wa Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo), ambao mpaka sasa ndio wanaotamba na kujulikana sana ulimwenguni. Kama hawakujifunza muziki moja kwa moja ndani ya Zaiko, basi waliibukia katika bendi zinazomilikiwa na watu walioanzia Zaiko!
Ndivyo ilivyo kwa Habibu Ally Maulid Kinyogoli 'Master', ambaye yupo ulingoni kwa zaidi ya miaka 40 sasa na hivyo kujiwekea historia ndefu na ya pekee, pengine kuliko bondia yeyote wa enzi zake.
Kwa zaidi ya miaka 10 Kinyogoli alicheza ndondi za ridhaa, baadaye akawa mmoja wa waasisi wa ndondi za kulipwa. Cha kujivunia zaidi ni kwamba, bondia huyo mkongwe, kwa zaidi ya miaka 20 amekuwa akifundisha ndondi na siyo siri, wengi wa mabondia wanaotamba sasa katika ndondi za kimataifa ni matunda yake mwenyewe!
Ndiye aliyekuwa bondia wa pili wa Tanzania kuleta medali ya mashindano yanayoshirikisha nchi kutoka nje ya Afrika Mashariki wakati alipopata medali ya fedha katika Michezo ya Pili ya Afrika (2nd All African Games) iliyofanyika mjini Lagos, Nigeria mwaka 1973.
Hadi wakati huo mwanamasumbwi aliyekuwa ameleta medali kutoka nje ya mipaka ya Afrika Mashariki alikuwa marehemu Titus Simba, ambaye alipata medali ya kwanza ya fedha kwa Tanzania katika Michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka 1970 huko Scotland.
Kinyogoli anakiri kwamba, Simba ni mmoja wa mabondia mahiri waliojitoa mhanga kwa kutetea heshima ya Tanzania, lakini serikali haikuwajali kabisa hata pale alipofariki. Chama cha Ndondi za Ridhaa (TABA) kilitoa mchango wa shilingi 4,000 tu kuchangia mazishi ya bondia huyo mkongwe!
"Mimi binafsi serikali imenisahau kabisa na haithamini mchango wangu katika mchezo huu, ingawa ni mimi nilianza kuwafundisha vijana kadhaa waliolitangaza jina la nchi katika ndondi za ridhaa na kulipwa," analalamika.
Miongoni mwa mabondia ambao ni matunda yake ni Majuto Mchevu, aliyemfundisha mwaka sitini na tisa katika klabu ya Magomeni Community Centre, Zakaria Yombayomba, Habibu Mzungu, Bakari Selemani, Kweli Msigili, Abbas Pazi, Francis na nduguye Benedict Kakokele aliowafundisha mwaka 1971.
Katika klabu ya Urafiki mwaka 1973 aliwafundisha akina Charles Mhilu 'Spinks', Lazaro Makali, Salum Temianga, Herbert Sempoli na Mmasi, ambao walikuwa wakifanyia mazoezi Peninsula Hotel.
Baada ya kustaafu ndondi za ridhaa mwaka 1978 na kuanza kufundisha watoto ndipo alipopata nafasi ya kuwafundisha mabondia wengi zaidi. Mara tu baada ya kustaafu ndondi mwaka huo alianzisha klabu ya ndondi ya Simba na kwa kuanzia akawachukua watoto wa mzee Ally Matumla Namwera; akina Matumla, Haji, Rashid na Hassan, ambao hivi sasa wamekuwa maarufu katika mchezo huo duniani kote.
Baadaye akawachukua akina Mbwana, Karim na Mazimbo Matumla, Iraq Hudu, Joseph Marwa, Adeli Mkajanga, Oscar Manyuka, marehemu Steven Bicco, Patrick Kibona, Shabani Mhamila 'Star Boy' , Adam Abdulrahman, Maneno Oswald, Rajab Mhamila 'Super D' ambaye kwa sasa ni kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi na ni msaidizi wake katika kuwanowa vijana chipkizi kwa sasa, Abdallah Nyuni, Nassor Kondo, Rehema Matumla, Theresia Kapinga, na wengineo wengi.
Anasema, pamoja na kuichezea timu ya ndondi ya taifa kwa miaka 12, pamoja na kuendeleza vipaji vya vijana wengi katika mchezo huo, lakini hakuna chochote alichoambulia kutoka serikalini.
"Msaada pekee niliowahi kuupata ni mfuko wa mazoezi (punching bag) na jozi mbili tu za gloves ambazo nilipewa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Michezo, Victor Mkodo," anasema kwa mamsikitiko.
Kinyogoli alizaliwa Oktoba 20, 1948 huko Maneromango, wilayani Kisarawe, akiwa mtoto wa tano katika familia ya mzee Ally Maulid Kinyogoli iliyokuwa na watoto nane; wanne wanaume na wanne wanawake. Alipata elimu yake ya kati huko Maneromango Middle School mwaka elfu mia tisa na sitini na tano.
Alianza kucheza ngumi mwaka 1958 wakati akiwa darasa la pili. "Kulikuwa na kaka yangu katika familia aliyeitwa Saidi Uliza 'Sheni' ambaye alikuwa anacheza ngumi katika klabu ya Anartouglou, jijini Dar es Salaam. Kila alipokuja likizo alikuwa akinifundisha. Pia mimi mwenyewe nilipokuwa nikija mjini alinichukua na kunipeleka pale klabuni kwao kuangalia mazoezi, kwa kweli nikavutiwa sana na mchezo huo," amaeleza.
Baada ya kumaliza shule aliamua kuja Dar es Salaam na kujiunga na klabu ya ndondi ya Magomeni, ambapo walimu wao walikuwa Kassim Saidi na Joseph Okalla. Mabondia wengine aliokuwa nao walikuwa Ayoub Zicco, Hamisi Nassoro, marehemu Michael Nchimbi, marehemu Hemedi Selemani (kaka yake Bakari Selemani) na wengineo.
Pambano lake la kwanza lilikuwa dhidi ya Ally Kanduru wa JKT katika uzani wa light welter, ambalo lilikuwa la kirafiki na lilifanyika mwaka sitini na sita. Kinyogoli alishinda pambono hilo kwa knock out ya raundi ya pili.
Mwaka uliofuata alitwaa ubingwa wa taifa wa uzani wa light baada ya kumchapa Jack Laimon wa klabu ya Anartouglou. "Wakati huo uzito ulikuwa ni wa kubuni tu. Unaweza kucheza uzito mkubwa, kesho ukacheza uzito mdogo. Mara nyingi mabondia walikuwa wakipinishwa kwa kuangalia maumbo yao. Wakati Baraza la Michezo la Taifa (BMT) lilipoundwa mwaka sitini na saba ndipo sheria zilipoanza kufundishwa. Wakati huo Katibu Mkuu wa TABA alikuwa Nizar Walji," anafafanua.
Katika mashindano ya mikoa, anasema, mabondia wa Morogoro na Tanga walikuwa hatari na walimpa wakati mgumu sana.
Akiwa katika timu ya Taifa, Kinyogoli aliweza kuzuru nchi nyingi kama Kenya, Uganda, Zambia, New Zealand, Shelisheli, Nigeria, Ethiopia, Scotland, Mexico na nyinginezo nyingi.
Anakumbuka kwamba, mwaka sitini na nae alishindwa kwenda Zambia kuwania ubingwa wa Afrika kutokana na kuugua, nafasi yake ikachukuliwa na James Jonathan.
Mapambano ambayo yapo kwenye kumbukumbu yake ni lile la mtoano dhidi ya Adeyemi wa Nigeria kuwania ubingwa wa Jumuiya ya Madola katika uzani wa light huko Edinburgh, Scotland mwaka 1970, ambapo alishindwa kwa pointi. Mnigeria huyo alinyakua medali ya dhahabu baada ya kuwatoa mabindia wengine kwa KO. Ni katika michezo hiyo ambapo Titus Simba alitwaa medali ya fedha baada ya kupigwa na John Conteh wa England.
Pambano jingine lililopo kwenye kumbukumbu zake ni lile la kuwania ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati katika uzani wa unyoya (feather weight), ambapo alipambana na Musoke wa Uganda mjini Nairobi, Kenya katika pambano la nusu fainali mwaka 1971.
"Pambano hilo nilipigana kwa jihadi kama mtu mwenye wazimu. Nilikuwa tayari kufa lakini nishinde. Hii ilitokana na ukweli kwamba, bondia wa Tanzania nilikuwa nimebakia peke yangu katika michuano hiyo baada ya akina Patrick Mtagalo, Said Tambwe na Frevitus Bitegeko kutolewa. Wengi walinidharau na kujua kwamba na mimi ningebondwa kama wenzangu. Hivyo, nilipanda ulingoni nikiwa na dhamira moja tu ya kushinda na kuiondolea aibu Tanznaia, na kwa kweli nilishinda kwa pointi na kuingia fainali," anasema.
Katika fainali alikumbana na John Ndelu wa Kenya na akapigwa kwa pointi hivyo kufanikiwa kurejea na medali ya fedha katika mashindano hayo ya kwanza kabisa katika ukanda huo.
Mwaka huo 1971 alikwenda kushiriki katika sherehe za kuadhimisha uhuru wa Madagascar na akasanikiwa kushinda mapambano yote mawili. Baada ya hapo timu yote ya taifa ilikwenda Ujerumani kushiriki michezo ya nusu-Olimpiki kujiandaa na ile ya Olimpiki ya mwaka 1972. Nchi nyingine zilizoshiriki zilikuwa Romania, Cuba, Nigeria, Libya na wenyeji Ujerumani Mashariki. Kinyogoli alipoteza pambano lake la kwanza tu kwa pointi dhidi ya Peter Garth, Mjerumani, mtoto wa kocha aliyekuwa akiwafundisha. Mjerumani huyo, hata hivyo, alidundwa na Eddy Nduku wa Nigeria kwa KO ya raundi ya pili.
Mwaka 1972 alikwenda na timu ya Taifa Munich, Ujerumani Magharibi katika michezo ya Olimpiki. Katika hatua ya kwanza alimdunda bondia kutoka Cambodia, lakini akashindwa mchezo wa pili dhidi ya Robert wa Puerto Rico, ambaye alimpiga kwa pointi. Anasema alishindwa kwa sababu mkono wake uliteguka.
Mwaka 1973, aliweka historia nyingine kwa Tanzania baada ya kushiriki Michezo ya Pili ya Afrika nchini Nigeria. Katika robo fainali alimpiga bondia kutoka Madagascar na katika nusu fainali akamtwanga bondia kutoka Mali na kusonga mbele kwenye fainali kuwania ubingwa wa uzani wa Bantam, ambapo alikumbana na Omollo wa Uganda aliyemshinda Kinyogoli kwa pointi na hivyo Mtanzania huyo kuambulia medali ya fedha.
"Uamuzi wa pambano hilo ulilalamikiwa na majaji karibu wote isipokuwa wale waliokuwa kwenye meza ya uamuzi. Matokeo yake Omollo hakuchaguliwa kwenye timu ya ndondi ya Afrika na badala yake mimi ndiye niliyechaguliwa na kupewa unahodha kwenye ndondi. Baada ya kufanya mazoezi nchini Senegal nililiwakilisha Bara la Afrika mjini Mexico City, Mexico katika Michezo ya Dunia ya Mabara," anaeleza.
Kinyogoli, akiwa nahodha wa Tanzania, alifanikiwa kuingia fainali na kutwaa ushindi wa pili wa dunia wa uzito wa Bantam baada ya kushindwa na Alfred Gomez wa Puerto Rico. Akarejea na medali ya fedha.
Watanzania wengine waliokuwa wamechaguliwa kuunda timu ya Afrika ni mwanariadha Filbert Bayi, aliyekuwa kipa wa Simba marehemu Omar Mahadh bin Jabir na mshambuliaji wa zamani wa Young Africans, Maulid Bakari Dilunga, ambaye alikuwa nahodha wa timu hiyo ya Afrika.
Kinyogoli aliongozana pia na mabondia James Oduor wa Uganda (uzito wa light), George Oduor wa Kenya (light welter), Dulla wa Kenya (middle), na Obisia wa Nigeria (super welter). Wanamichezo wengine walikuwa Ben Gibson wa Kenya aliyekuwa akikimbia katika mita 1,500 na wengineo.
Mwaka 1974 alishiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola huko Christchurch, New Zealand na kurudia robo fainali baada ya kudundwa kwa pointi na Ally Rojo wa Uganda. Katika michezo hiyo mwanariadha wa Tanzania Filbert Bayi alivunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 1,500.
Mwaka 1975, Kinyogoli alishiriki mashindano ya Afrika Mashariki na Kati mjini Lusaka, Zambia na kutwaa medali ya shaba baada ya kupigwa na Mzambia katika nusu fainali. Mwaka uliofuata alikuwa katika timu ya Taifa iliyoshiriki sherehe za uhuru wa Shelisheli, ambazo zilishirikisha pia nchi za Kenya, Uganda na wenyeji, na akashinda mechi zote mbili.
Mwaka 1977 alitwaa medali ya fedha baada ya kupigwa na bondia wa Ethiopia katika fainali ya michuano ya Afrika Mashariki na Kati mjini Addis Ababa, Ethiopia. Mwaka 1978 akaamua kustaafu kuichezea timu ya taifa na kubakia kwenye klabu ya Bandari.
Mpaka anastaafu ndondi za ridhaa alikuwa amecheza mapambano 110 na kushinda 95 na kupoteza 15. Alipata medali saba, moja ya dhahabu, tano za fedha na moja ya shaba.
Akizungumzia kuhusu makocha, Kinyogoli anasema kwamba, kocha Bajwala alikuwa haeleweki kabisa, lakini akaongeza kwamba, alipata mchango mkubwa kwa kocha Ogan Kodbas aliyekuwa kocha wa Afrika. Pia anamkumbuka kocha wa timu ya Taifa, Calvin Cobb, aliyefukuzwa nchini kwa sababu za kiusalama.
Vifaa, anasema, ndilo tatizo kubwa kwa sasa. "Mifuko ya mazoezi, gloves na vifaa vingine ni vingi sana madukani tofauti na enzi zetu, lakini tatizo kubwa ni fedha. Tukipata vifaa hivyo, pamoja na ulingo tutaweza kufanya vizuri. Lakini ni vyema mabondia wa zamani wakafungua klabu nyingi za mazoezi na wachezaji wajiunge kwenye klabu za kudumu ili kuuinua mchezo. Lengo langu ni kuhakikisha nafungua klabu nyingi za mitaani kila wilaya," anasema Kinyogoli ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Ngumi za Kulipwa Mkoani Dar es Salaam (DPBU) chenye azma ya kuhamasisha klabu za mitaani tu.
Ameitaka serikali kuhamasisha mchezo wa ndondi mikoani kote, na ikibidi kuanzia mashuleni kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma. "Uanzishaji wa klabu za mitaani kila pembe ndilo chimbuko la mabondia wazuri," anasema.
Amewataka wafanyabiashara na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kuudhamini mchezo huo na akasifu jitihada zinazofanywa na majeshi, hususan Jeshi la Ulinzi la Wananchi, kuwa hao pekee ndio mapromota wanaoufanya mchezo huo uendelee kudumu Tanzania.
Jina lake bado liko kwenye chati kama vile bado anacheza, na wale aliowafundisha bado wanalitangaza. Mwaka 1998 Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kilimuenzi kwa kumpa tuzo ya Bondia Bora wa zamani.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...