Rais
Kikwete akiendesha kikao cha baraza la Mawaziri siku za hivi karibuni.
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake Rais
Jakaya Kikwete, imeanza kuwahoji mawaziri waliotajwa ni ‘mzigo’ kwa
Serikali. Picha na Maktaba.
………………………………………………………………
Dodoma. Kamati
Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya
Kikwete, imeanza kuwahoji mawaziri waliotajwa ni ‘mzigo’ kwa Serikali.
Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, jana alilithibitishia gazeti
dada la Mwananchi, The Citizen juu ya kuanza kwa kikao cha Kamati Kuu
(CC), lakini hakuwa tayari kuingia kwa undani kuhusu ajenda.
Hata
hivyo, habari za ndani zilieleza kwamba miongoni mwa ajenda kuu za CC
ni kuwahoji mawaziri wanaolalamikiwa na wananchi, kwamba wameshindwa
kutekeleza majukumu yao.
Wakiwa
Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Nape aliwatupia lawama mawaziri
wakati akielezea changamoto zinazowakabili wakulima ambao ni asilimia 80
ya Watanzania, huku mawaziri husika wakikaa kimya.
Mawaziri
waliotajwa mzigo ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru
Kawambwa; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza na
Naibu wake, Adam Malima, kwamba wameshindwa kazi na alipendekeza
wang’olewe.
Hata
hivyo, gazeti hili jana lilishuhudia mawaziri kadhaa wakifika na
kuingia kwenye mkutano wa CC, taarifa zingine zilisema mawaziri
waliofika kwenye kikao hicho walihojiwa na wajumbe wa CC.
Kuhojiwa na CC
Mawaziri
waliohojiwa na CC hadi kufikia saa 8:00 mchana jana walitajwa kuwa ni
Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Christopher Chiza. Mkuya ndiye ambaye kwa sasa anaisimamia
Wizara Fedha kutokana na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa kulazwa
nchini Afrika Kusini akisumbuliwa na maradhi ambayo hayajatajwa.
Waandishi
wa gazeti hili jana waliwashuhudia takriban mawaziri 10 wakiingia
katika ofisi za makao makuu ya CCM, Dodoma, maarufu White House, huku
baadhi wakiwa si wajumbe wa CC.
Habari
zilizotufikia jioni ziliwataja wengine kuwa ni Dk David Mathayo David
(Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi), Hawa Ghasia (Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-Tamisemi), Dk
Kawambwa, Celina Kombani (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma).
Dk
Kawambwa wakati akitoka kwenye kikao cha CC aliulizwa na waandishi wa
habari kilichotokea na yeye alijibu kwa kifupi; “Mawaziri mizigo ndiyo
tunatoka.”
Mawaziri
ambao si wajumbe wa CC ni Mkuya, Chiza, Dk Kawambwa, Hawa Ghasia na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Utawala Bora, George
Mkuchika ambaye naye taarifa zilidai alihojiwa.
Tayari
Bunge limepitisha azimio la kumtaka Ghasia pamoja na naibu mawaziri
wake wawili, Aggrey Mwanry na Majaliwa Kassim Majaliwa, kupima na
kutafakari kama bado wanatosha kusimamia wizara hiyo.
Kiini
cha Bunge kupitisha azimio hilo ni taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu
za Serikali kubainisha kuwapo wizi, ubadhirifu na mtandao wa ufisadi
ndani ya Tamisemi, Halmashauri na Hazina.
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda ambaye baadhi ya wabunge wamemtaja kama waziri
mzigo namba moja, amesema yuko tayari kuachia ngazi kama Rais ataamua
kumwondoa katika wadhifa huo.
Pinda
alitoa kauli hiyo juzi bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la
papo kwa hapo kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Ahmed (Cuf)
aliyetaka aeleze anajisikiaje kuitwa mzigo namba moja.
Akijibu
swali hilo, Pinda alisema yeye anasimamia wizara 20, hivyo kama wapo
watakaomhukumu kwa sababu ya wizara moja ama mbili kutofanya vizuri basi
watu hao watakuwa hawamtendei haki.
Alisema
kama Rais atamwona ameshindwa kuwajibika yuko tayari kuachia ngazi na
endapo Rais hatafanya hivyo na wabunge bado wakaona ipo haja hiyo,
wampigie kura ya kutokuwa na imani naye.
Kauli ya CCM
Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, mbele ya Katibu Mkuu wa chama
hicho, Abdulrahman Kinana, alisema kuwa mawaziri hao wameshindwa
kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia Watanzania.
Alisema
kuwa Waziri Chiza na Malima wamebaki wakifunga tai na kuvaa suti mjini
wakati wakulima wa Ruvuma na mikoa mingine ya Tanzania wakiteseka.
Nape
alisema Waziri Kawambwa naye anatakiwa kuchukuliwa hatua kwa kuingia
mkataba na kampuni ya ujenzi ya Progressive iliyopewa zabuni ya
kutengeneza barabara ya Namtumbo hadi Tunduru wakati mkandarasi huyo
hana uwezo wa kuijenga na matokeo yake amefukuzwa kazi.
Dk
Kawambwa ametupiwa lawama hizo kutokana na kuipa kazi kampuni hiyo
wakati akiwa Waziri wa Miundombinu pamoja na kushindwa kusimamia elimu.
“Katibu
Mkuu (Kinana), nilimuuliza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Chiza na Malima
wamefika lini kusikiliza matatizo ya wakulima wa tumbaku, korosho na
mahindi, alinijibu hakumbuki kama wamefika mkoani hapa. Nikafuatilia na
kubaini si yeye tu hata Waziri aliyetangulia Profesa Jumanne Maghembe
naye hakuwahi kufika. Najiuliza sababu nini, hakuna majibu,” alisema
Nape.
Alisema
anasikitishwa na kitendo cha mawaziri hao waliopewa dhamana kushindwa
kutambua wajibu wao na kwamba umefika wakati wa kuhojiwa na Kamati Kuu
(CC) ya CCM, ili wachukuliwe hatua kwani bila kufanya hivyo aibu itarudi
kwa chama chake.
Wabunge wajitosa
Kikao
hicho cha CC kinafanyika huku kikiwa na taarifa kwamba wabunge wa chama
hicho tawala wameanza kukusanya saini za wabunge, ili kushinikiza
kuitishwa kwa kikao cha wabunge hao au Party Cocas.
Uchunguzi
wa gazeti hili, uliofanywa kwa siku kadhaa mjini hapa, umebaini kuwa
wabunge wa CCM zaidi ya 160 wametia saini katika fomu hiyo wakiwamo
mawaziri zaidi ya 10.
Chanzo
kimoja cha kuaminika kilisema kuwa fomu hiyo iliwasilishwa katika ofisi
ya katibu wa wabunge wa CCM, ikiambatana na barua inayotaka kuitishwa
kwa kikao kitakachowakutanisha.
“Tuliwaomba
waitishe kikao cha wabunge wa CCM ili mawaziri ambao tunawaona
hawatimizi majukumu yao kikamilifu waweze kuhojiwa lakini wakawa
wanasuasua,”kilisema chanzo hicho.
“Lakini
mmoja wetu akasema kwa kuwa wamepiga chenga ya kukiitisha basi kuna
nafasi ya kikanuni ya kukusanya saini za wabunge zaidi ya nusu
kushinikiza kuitishwa kwa kikao,”alisema mbunge huyo.
Taarifa ya ziada na Habel Chidawali
Mbunge
mwingine wa CCM alisema katika kikao hicho wabunge walitaka
kukutanishwa kwa pamoja kati yao, mawaziri wanaoonekana kuwa mzigo na
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
“Kikao
hicho tulitaka kiwe Desemba 12 mwaka huu ili tuanze kuwahoji mawaziri
kabla ya CC lakini Mwenyekiti (Mizengo Pinda), amekuwa akipiga danadana
hadi leo (jana) inapokutana”alisema.
Habari
zaidi zilisema baadhi ya wabunge wa CCM walikutana faragha na Kinana
juzi jioni na kumtahadharisha kama mawaziri hao wasipowajibishwa, CCM
kitakuwa na wakati mgumu.
Vuguvugu
linaloendelea hivi sasa ndani ya wabunge wa CCM, liliwahi kujitokeza
Bunge la Aprili mwaka jana na kumlazimisha Rais Kikwete kupangua Baraza
lake Mawaziri Mei 4,2012.
Kung’olewa
kwa mawaziri sita waliokuwa wakishinikizwa na wabunge wajiuzulu
kulitokana na taarifa za kamati za kudumu za bunge na za Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Katika
baraza lake hilo jipya, Rais aliwatosa mawaziri waliokuwa
wakishinikizwa kujiuzulu akiwemo Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo na
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami.
Wengine
waliotoswa kwa shinikizo hilo lililoungwa mkono na kambi ya upinzani ni
wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, wa Nishati na Madini, William
Ngeleja na wa Uchukuzi, Omar Nundu.
Pia
Naibu Waziri wa Uchukuzi wa wakati huo, Dk Athuman Mfutakamba naye
alitoswa sambamba na Waziri wa Afya, Dk Haji Hussein Mponda na Naibu
wake, Dk Lucy Nkya.
CHANZO: MWANANCH
No comments:
Post a Comment