Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Saturday, December 14, 2013

Airtel Tanzania kumleta Andy Cole Dar es Salaam kushiriki promosheni ya Mimi ni Bingwa


Andy Cole akionyesha umahiri wake katika kulisakata kabumbu alipokuwa akitoa somo kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Makongo ya jijini Dar es salaam mara ya mwisho alipotembelea Tanzania.
 Na Mwandishi Wetu
MCHEZAJI wa zamani wa klabu ya Manchester United Andy Cole anatarajia kutua jijini Dar es Salaam Ijumaa hii, imethibishwa.
Ziara ya Cole nchini inalenga kuwapatia uzoefu washindi wa tiketi za promosheni ya Airtel ya 'Mimi ni Bingwa' ambao watasafiri kwenda kuangalia mechi za klabu ya Manchester United moja kwa moja (live) katika uwanja wa Old Trafford pamoja na kukabidhi vifaa vya mazoezi  kwa wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania ya chini ya umri wa miaka 17.
Hii ni ziara ya pili Tanzania kwa mchezaji Cole baada ya kutembelea Tanzania mwaka 2011 alipozindua mpango wa kutafuta vipaji wa Airtel Rising Star.
Akizungumza na waandishi wa habari juu ya ziara hiyo, Meneja Uhusiano wa kampuni ya mawasiliano ya Airtel Tanzania, Bw Jackson Mmbando alisema kuwa mchezaji huyo mkubwa wa zamani wa Man U atakuwa na wakati wa kuzungumza na kushiriki mazoezi na wachezaji wa timu ya Tanzania chini ya miaka 17, timu ambayo wengi wao ni matunda ya mpango wa kuvumbua vipaji wa Airtel Rising Star.
"Andy Cole ataongea na nyota hao wanaochipukia, na kuwashawishi kuongeza jitihada zaidi katika michezo pamoja na kuwapatia mbinu za jinsi gani ya kufikia mafanikio katika fani yao ya michezo.
"Mbali na kuwaonyesha wachezaji hao njia ya mafanikio, mchezaji huyo mkubwa wa zamani wa Manchester United pia atakabidhi vifaa vya mazoezi kwa timu hiyo," alisema Mmbando.
Alisema kuwa Cole pia atahudhuria droo ya moja kwa moja (live) ya kuwatafuta na kuwatangaza washindi wa tiketi tatu za kwenda Old Trafford, kabla ya kuungana na washabiki wa Man U kuangalia mechi moja kwa moja (live) itakayoonyeshwa Coco beach kati ya Manchester United na Aston Villa itakayochezwa jumapili.
Rashid Jacob Kagomola na Dickson Lyatuu ni washindi wa kwanza wawili wa promosheni ya Mimi ni Bingwa waliojishindia tiketi za kwenda Old Trafford, ambapo zawadi zaidi ya shilingi milioni 40 tayari imetolewa kwa ajili ya washindi wa kila siku na kila wiki.
Mmbando alisema kuwa bado kuna zawadi nyingi zaidi kushindaniwa katika promosheni, na kuongeza kuwa ili mteja kushiriki anatakiwa kutuma ujumbe mfupi (SMS) wa neno "BINGWA" kwenda namba 15656.
Aidha, alisema Airtel imeweka vituo mbali mbali ambavyo washabiki wa Man U wataweza kuangalia mechi za Manchester United moja kwa moja (live) kupitia luninga kubwa, na kutaja vituo hivyo kuwa ni Mbeya - Shaba Pub, Mwanza - Shooters Pub, Dodoma - Four ways, Dar es Salaam - Coco Beach, Morogoro - Nyumbani Lounge na Arusha - Empire Sports bar.
Mwaka 2011 kampuni ya mawasiliano ya Airtel Tanzania ilizindua mpango wa kuvumbua vipaji katika soka kwa ushirikiano na klabu ya Manchester United, uliolenga kuvumbua vipaji na kuviendeleza katika mpira wa miguu Tanzania.
Cole amekuwa na dhamira ya kuonyesha uzoefu wake kwa wachezaji nyota wanaochipukia ikiwa ni kama njia ya kuunga mkono maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu duniani.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...