Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, December 20, 2013

George Foreman sasa akumbukia enzi


George Foreman sasa akumbukia enzi

GEORGE Edward Foreman au Big George ni jina kubwa katika ulimwengu wa michezo, hasa masumbwi.

Wengine hupenda kumwita ‘The Heywood Giant’ kwa sababu ya alikotokea na ukubwa wake wa umbo, ambapo ni Mmarekani ambaye kwa sasa amefikisha umri wa miaka 64.

Foreman anasema kwamba anakumbukia enzi zake, na kama kuna mambo ambayo hatasahau ni ngumi ya Joe Frazier anayosema ilimpata sikioni na kuwa kama radi.

Anasema akiikumbuka anachukia ndondi, lakini kwamba ngumi hiyo ya kijana aliyekuwa mdogo ndiyo ilimfanya akaongeza jitihada ili awe bondia mzuri na kweli alifanikiwa kuwa bora kama akina Muhammad Ali.

“Hakuwa mpiganaji mkubwa lakini ndiye pekee niliyekuwa namwogopa tukiwa ulingoni maana alijiamini sana, hata nilipompiga na kumdondosha, alinyanyuka haraka sana na kuwa kama mbogo aliyejeruhiwa,” anasema.

Anakumbuka alivyomwangusha mara sita lakini kila baada ya kufanya hivyo alinyanyuka na kuendelea na pambano mpaka watu wakamshauri mwamuzi asitishe pambano, lakini naye Foreman aliondoka na majeraha makubwa ya sikio na anasema aliogopa kwamba Frazier angemuua.

Hayo yalikuwa ya zamani lakini sasa Foreman ameanzisha kampuni yake inayoitwa ‘Foreman Boys Promotions’ ambayo inasimamia ndondi kwa kuandaa mapambano.

Kazi yao ya kwanza ilikuwa ni pigano la uzani wa Feather kati ya bondia wa Puerto Rico, Juan Manuel Lopez na Mmarekani ambaye hakupata kupigwa kabla ya hapo, Mikey Garcia.

Foreman aliwahi kupata medali za dhahabu kwenye michuano ya Olimpiki na alikuwa bingwa mara mbili wa uzani wa juu duniani.

Kwa sasa, tofauti na kufanya promosheni za ngumi, Foreman anaandika vitabu na kuendesha biashara mbalimbali.
Katika utoto wake alikuwa na matatizo makubwa lakini amekuja kufanikiwa kwenye masumbwi na maisha kwa ujumla.

Alipoteza pambano lake kwa Muhammad Ali mwaka 1974 katika kile kilichoitwa ‘The Rumble in the Jungle’. Alistaafu baada ya kupoteza pambano dhidi ya Jimmy Young 1977.

Alipata kustaafu lakini baadaye 1994 alirudi ulingoni akapigana akiwa na umri wa miaka 45 akichapana na Michael Moorer.

Kwa sasa anashikilia rekodi ya kuwa bingwa mwenye umri mkubwa zaidi wa uzani wa juu duniani ambapo ameshinda mapambano 76 kati ya hayo 68 yakiwa ni kwa ‘Knock Out’.

Anachukuliwa kuwa bondia namba nane kwa umaarufu duniani kwenye uzani wa juu, ambapo mwaka 2002 alitajwa kuwa miongoni mwa mabondia 25 bora katika miaka 80 iliyopita.

Hata hivyo, jarida la ‘The Ring’ lilimtaja kuwa bondia namba tisa kwa ubora.
Nje ya ulingo ni mjasiriamali aliyefanikiwa sana na maisha yake yanakwenda vyema na anasifika sana huko alikozaliwa, Marshall, Texas.

Alilelewa na J.D. Foreman aliyemwoa mama yake, lakini baba yake mzazi ni Leroy Moorehead.

Foreman alikuwa anapenda zaidi soka na si ajabu leo angekuwa mmoja wa wanasoka maarufu zaidi duniani, akifuata nyayo za Jim Brown, lakini aliamua kuachana na mchezo huo na kujiunga na masumbwi.

Vyombo vya habari havikumsema vizuri sana kwa sababu vilidai hakuwa na urafiki navyo hata alipotakiwa kuongea alikuwa mkinya akivikwepa.

Foreman alipata kwenda Afrika, ambapo alikuwa akifanya mazoezi nchini Zaire, ambapo katika mazoezi alijiumiza juu ya jicho na kulazimika kuahirisha mechi aliyokuwa nayo kwa mwezi mmoja.

Wakati huo, hata Ali mwenyewe alizuru Zaire kabla ya pambano lao, nchi iliyokuwa imechanua vyema kimazingira japokuwa iliharibiwa na wanasiasa.
Katika tawasifu yake, Foreman anasema kwamba lengo lake kubwa lilikuwa kutafuta fedha kwa ajili ya kituo cha vijana lakini pia kupambana na Mike Tyson.
.Chanzo gazeti la SPOTILEO
zaidi tembelea mtandao wa
http://superdboxingcoach.blogspot.com/
na kwa mahitaji mbali mbali ya dvd za mafunzo ya ngumi wasiliana na kocha kwa namba za simu

0713406938

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...