Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, December 25, 2013

UMEME BEI JUU JANUARI MOSI


Taarifa ya EWURA YA bei mpya za umeme zitakazoanza kutumika Januari, Mosi,2013

Tarehe 11 Oktoba 2013, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) liliwasilisha maombi ya kurekebisha bei ya umeme kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA). TANESCO ilipendekeza kuongeza bei kwa asilimia 67.87 kuanzia tarehe 1 Oktoba 2013, asilimia 12.74 kuanzia tarehe 1 Januari 2014 na asilimia 9.17 kuanzia tarehe 1 Januari 2015.

Vilevile TANESCO waliomba kuidhinishwa kwa kanuni ya kurekebisha bei ya umeme kulingana na mabadiliko ya bei za mafuta, mfumuko wa bei na mabadiliko ya thamani ya shilingi ya kitanzania. Aidha, TANESCO iliomba kuidhinishwa viwango vya gharama za kuunganisha umeme vinavyozingatia ruzuku inaliyotolewa na Serikali, na kuidhinishwa tozo mbalimbali kwa huduma zitolewazo na TANESCO.

Kwa mujibu wa TANESCO, kupitishwa kwa maombi haya kutaliwezesha Shirika (a) kupata fedha za uendeshaji na uwekezaji wa miundombinu, (b) kulifanya Shirika liweze kukopesheka na hivyo kuwezesha kupata mikopo yenye masharti nafuu, (c) kuliwezesha Shirika kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya umeme kwenye Gridi ya Taifa, na (d) kuongeza uwezo wa 
kufanya matengenezo ya mara kwa mara ya miundombinu iliyopo ili kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa huduma za umeme wa uhakika kwa wateja.

Itakumbukwa kwamba bei za umeme zinazotumika hivi sasa ziliidhinishwa mwezi Januari 2012. Bei hizo zilipanda kwa asilimia 40.29 ikilinganishwa na maombi ya TANESCO ambapo ilipendekeza bei zipande kwa wastani wa asilimia 155. Sababu ilikuwa ni kuongezeka kwa gharama za uendeshaji kulikosababishwa na hali ya ukame katika maeneo yanayotiririsha maji katika mabwawa ya kuzalishia umeme, toka mwaka 2011. 

Hali hiyo ilipelekea TANESCO kulazimika kununua umeme kwa gharama kutoka kwa wazalishaji wa dharura (Emergency Power Producers). Hali ya maji katika mabwawa ya kuzalishia umeme bado sio nzuri na hivyo TANESCO itaendelea kununua umeme kutoka kwa wazalishaji wa dharura (Emergency Power Producers).

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...