FIKIRIA mbio zozote kubwa
duniani kama vile London Marathon, Paris Marathon au yale mengine yenye
kupendwa na wengi zaidi duniani ya Berlin Marathon.
Mashindano yote haya ni ya
kutukuka kutokana na kushirikisha wanariadha wenye majina makubwa duniani, huku
kukiwa na ushindani mkubwa zaidi miongoni mwa washiriki.
Sasa Tanzania inaweza ikapata
kitu cha kujivunia zaidi kwa ujio wa mashindano ya mbio ndefu yaitwayo ‘Uhuru
Marathon’ ambayo yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi Desemba 5, mwaka huu jijini Dar
es Salaam.
Upekee wa shindano hilo la
Uhuru Marathon ni kutokana na aina ya washiriki wake, pamoja na kupewa tafu
kubwa na waandaaji wa mashindano ya Berlin Marathon, ambao wanataka kuiona
Tanzania inatangazwa zaidi.
Hivyo shindano la Uhuru
Marathon, ndilo ambalo lina uwezo mkubwa wa kuwabeba Watanzania kwa kutangazika
zaidi, hasa ukichukulia uzoefu mkubwa walionao waandaaji wa Berlin Marathon.
Hivi karibuni mjini Dodoma,
Spika wa Bunge, Anna Makinda alifanya uzinduzi wa awali wa mbio hizo kabla ya
uzinduzi wenyewe rasmi hapo Desemba 5. Mbio hizo ndefu zitakuwa zikiandaliwa na
kuratibiwa na Kampuni ya Intellectuals Communication.
Akithibitisha hilo, Mratibu wa
Uhuru Marathon, Innocent Melleck alisema lengo la mbio hizo ni kuwakumbusha Watanzania
umuhimu wa kukumbuka, kuzingatia na kuuenzi urithi waliaochiwa na viongozi waliopigania
uhuru wa nchi.
Alisema urithi huo ambao
utakuwa ukikumbukwa kila mwaka kupitia mbio hizo ni upendo, mshikamano, umoja
na amani iliyopo. Melleck aliisema mbio hizo zitakuwa zikifanyika kila mwaka na
zitaanza rasmi hapo mwakani.
Melleck alisema pamoja na
kwamba mbio hizo zimezinduliwa rasmi Bungeni pia wameandaa hafla ya uzinduzi
mwingine jijini Dar es Salaam Desemba 5 katika hoteli ya Delemonte iliyopo
Jengo la Benjamin Mkapa.
Mgeni rasmi katika uzinduzi
huo anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk.
Fenella Mukangara.
Mratibu huyo alisema ana imani
mbio hizo zitajizolea umaarufu mkubwa kutokana na jinsi zitakavyoweza kuteka
hisia za watu mbalimbali wakiwemo wanamichezo.
Katika mbio hizo
zitakazowashirikisha watu wa kada mbalimbali zitakuwepo pia mbio za kilomita 3,
kilomita 5, kilomita 21 ambayo ni ‘half marathon’ pamoja na marathon yenyewe
ambapo itakuwa na umbali wa kilomita 42.
Mratibu huyo alisema katika
mbio za kilomita tatu itakuwa ni maalumu kwa ajili ya viongozi wa kada
mbalimbali, wakiwemo pia wale wa dini na zile za kilomita 5 pia zitakuwa za kuchangia
kwa ajili ya watu wa mahitaji ya kila aina.
“Hapa tunachotaka kufanya
katika mbio za kilomita tatu ni kuwaomba kama vile viongozi maarufu wa dini
mbalimbali pamoja na viongozi wetu ili kushiriki, kwa kudumisha amani na
upendo.
“Pia tutahakikisha kama mbio
za kilomita tano zinakuwa kwa ajili ya kuchangia watu wenye mahitaji mbalimbali
na tayari tuna uhakika mkubwa wa wanariadha maarufu zaidi duniani watashiriki,”
alisema.
Mratibu huyo alifafanua kuwa,
wamejipanga mno katika hilo ili kuhakikisha wanafanya mambo makubwa zaidi na
ambayo yataleta tija kwa taifa.
Wakati Uhuru Marathon
ikitambulishwa bungeni, kiongozi aliyeonekana kufurahishwa zaidi na hilo na
Spika Makinda, ambaye hakuishia kulimwagia sifa tu, bali alitaka hata viongozi
wahakikishe wanalifanikisha.
“Ni wazo zuri hasa katika
kipindi hiki ambacho tunapigania amani na mshikamano miongoni mwetu, kuenzi
mashindano kama haya ili kutufanya tuwe wamoja zaidi,” alisema Spika Makinda.
Kwa nini Berlin Marathon?
Melleck alisema, wameanza
mazungumzo na waandaaji wa mashindano ya Berlin Marathon, kwani hilo ni moja
kati ya shindano kubwa zaidi duniani, likiwa linashirikisha wasanii mbalimbali
walio maarufu zaidi.
“Tuko katika hatua ya mwisho
ya kuingia mkataba wa ushirikiano na Berlin Marathon, naamini tutafika mbali
zaidi katika kile ambacho tumedhamiria,” alisema Melleck.
Shindano la Berlin Marathon
au maarufu zaidi kwa jina la BMW Berlin Marathon kutokana na kudhaminiwa na
Kampuni ya BMW ni maarufu zaidi ndani ya Ujerumani na duniani kwa ujumla.
Shindano hilo lina umbali wa
kilomita 42.195 na kushirikisha wanariadha wa kulipwa na wale wa ridhaa na
lilianza kwa mara ya kwanza mwaka 1974 na linafanyika kila wiki ya mwisho ya
mwezi Septemba ya kila mwaka.
Shindano hili kwa umaarufu
wake mwaka 2008 lilishirikisha wanariadha wapatao 40,827 kutoka mataifa 107,
huku waliomaliza mbio wakiwa 35,913 na lina zawadi kibao za kuvutia.
Uhuru Maratho watafaidikaje?
Melleck alisema ushirikiano
wa Berlin Marathon una maana kubwa kwani itasaidia kuitangaza zaidi Tanzania na
kuifanya dunia itambue umuhimu wa amani, upendo, umoja na mshikamano miongoni
mwetu.
“Wanariadha wengi watashiriki
katika mbio hizi wengi wakiwa maarufu zaidi duniani, pamoja na viongozi wa kada
mbalimbali na hivyo kutimiza lengo tulilojiwekea.”
Mratibu huyo alisema, kuna
kila haja kwa Watanzania kuyathamini mashanindano hayo, kwani yana lengo la
kuwafanya wawe wamoja zaidi hasa katika kipindi hiki kigumu ambacho kuna
majaribu ya kila aina.
“Waasisi wetu wa taifa na
wale waliopigania uhuru walikuwa na malengo mengi na tunatakiwa kuyadumisha
hayo, hilo ndilo Uhuru Marathon inalokwenda kupigania,” alisema.
Kwa Watanzania itakuwa faraja
zaidi hasa ukichukulia jinsi taifa hili linavyoweza kufaidika kwa kuzalisha pia
wanariadha wa aina mbalimba.
No comments:
Post a Comment