Mhando kulia akiwa na Mwenyekiti wake, Pinto |
Na Princess Asia
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA)
kimeamua kulipeleka kwa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania
(MOAT), suala la kuzuiwa kwa vituo vya Televisheni na Redio nchini kutangaza
moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara pamoja na wapiga
picha za Televisheni kuchukua picha kwa ajili ya kutumia kwenye habari.
Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando ameiambia BIN
ZUBEIRY leo kwamba, hatua hiyo ina lengo la kuomba mwongozo kwa chama
hicho ambacho ndio kinachomiliki vyombo vya habari kuhusiana na suala hili
ambalo limekuwa likilalamikiwa kwa kiasi kikubwa na wanachama wake.
Tayari TASWA imefanya mazungumzo ya awali na MOAT, ambayo
imeridhia iandikiwe barua rasmi ili jambo hilo lijadiliwe kwenye vikao vyake na
baada ya hapo TASWA itapewa mwongozo ambao itautoa kwa waandishi wa habari za
michezo.
“Kwa kuwa Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto pia ni mjumbe wa
MOAT, basi suala hilo tunaamini litafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo, hivyo
tunawaomba waandishi wa habari za michezo waendelee kuwa watulivu na wavumilivu
kipindi hiki na wafanye majukumu yao kama kawaida,”alisema Mhando.
“Siku zote chama chetu kimekuwa na uhusiano mzuri na
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wadau wengine wote na TASWA haitaki ifike
mahali iwe na mgogoro na chama chochote cha michezo, lakini pia haitakuwa
tayari kuona wanachama wake wakishindwa kutekeleza majukumu yao,”aliongeza.
Wiki iliyopita kulifanyika kikao cha Kamati ya Ligi na baadhi
ya klabu zinazoshiriki ligi hiyo na kuzuia Televisheni na Redio kutangaza moja
kwa moja michezo ya Ligi Kuu pamoja na wapiga picha za Televisheni kuchukua
picha kwa ajili ya kutumia kwenye habari.
Katika kikao hicho ambacho Mwenyekiti wa TASWA, Juma
Pinto alihudhuria kulitoka maelezo
mbalimbali ambayo baadhi ya Wana Habari hawakubaliani nayo na wamekuwa wakitaka
TASWA ichukue hatua uamuzi mgumu.
Mhando amesema sekreterieti ya TASWA imeona si vizuri
kukurupuka kuchukua uamuzi wowote ule kwa sasa kwani yenyewe haina chombo cha
habari, lakini wanaofanya kazi kwenye vyombo vya habari ndiyo wanachama wake,
hivyo amesema itawasilisha MOAT maazimio ya kikao cha Kamati ya Ligi kuhusiana
na jambo hili, tuna hakika tutalimaliza.
Kuhusu Mkutano Mkuu wa TASWA, Mhando amesema Jumatano ya Novemba
16, mwaka huu Kamati ya Utendaji ya TASWA itakutana Dar es Salaam kupitia
ajenda za Mkutano huo na Novemba 18 Mwenyekiti wa TASWA, Juma Abbas Pinto atakutana
na Waandishi Habari kutangaza mdhamini wa mkutano huo pamoja na tarehe rasmi na
mahali utakapofanyika.
“Kutokana na kuandaliwa kwa ajenda mpya ya kuboresha chama na
maslahi ya wanachama wake, TASWA inaendelea kutafuta wadhamini zaidi ili
kuufanya mkutano huo uwe wa siku mbili,”alisema Mhando. Chanzo; Bin Zubeiry Blog
No comments:
Post a Comment