Mkurugenzi wa Lindi Soccer Academy (LSA), Hafidh Karongo (nyuma), akiwa
katika picha ya pamoja na wachezaji wa kikosi chake cha LSA
kilichoichapa Kingstone ya Kineng'ene, nje kidogo ya Manispaa ya Lindi
kwa mabao 3-2, ikiwa sehemu ya maandalizi ya Kombe la Muungano 2012.
LINDI, Tanzania
LSA inatarajia kushuka
tena kwenye Uwanja wa Mapinduzi Jumapili ijayo Novemba 18, kuumana na wenyeji
wengine wa kijiji hicho, Kineng’ene Stars, huku akisema watahakikisha
wanawafunga na kuendeleza wimbi la ushindi
KATIKA kujiandaa na michuano ya Muungano Cup 2012
itakayofanyika Desemba huko visiwani Zanzibar,
timu ya Lindi Soccer Academy (LSA) ya Lindi Mjini, juzi imeichapa Kingstone ya
Kineng’ene nje kidogo ya Manispaa hiyo kwa mabao 3-2.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu jana, Mkurugenzi wa
LSA, Hafidh Karongo, alisema kuwa mechi hiyo ilikuwa ni mfululizo wa maandalizi
ya kikosi chake, kilichoalikwa kushiriki Kombe la Muungano katikati ya mwezi
ujao huko Zanzibar.
Pambano hilo
la kirafiki, lilipigwa juzi kwenye Uwanja wa Mapinduzi ulioko katika kijiji cha
Kineng’ene, ambapo mabao ya washindi yaliwekwa nyavuni na Mohammed Omari dakika
ya tano, Haji Saidi dakika ya 60 na Maximilian Peter dakika ya 63.
Mabao ya wenyeji Kingstone iliyokera mashabiki wake kwa kukubali
kichapo hicho kwenye uwanja wa nyumbani, yalifungwa na Fabian Saidi dakika ya
tatu na Juma Nungo dakika ya 29 katika pambano kali lililojaa ufundi na
ushindani miongoni mwa nyota wa timu hizo.
Karongo aliongeza kuwa, LSA inatarajia kushuka tena kwenye Uwanja
wa Mapinduzi Jumapili ijayo Novemba 18, kuumana na wenyeji wengine wa kijiji
hicho, Kineng’ene Stars, huku akisema watahakikisha wanawafunga na kuendeleza
wimbi la ushindi.
LSA inatarajia kuondoka mjini Lindi mapema mwezi ujao,
kupitia jijini Dar es Salaam, ambako watacheza
mechi kadhaa za kirafiki – kabla ya kwenda kushiriki Kombe la Muungano huko Zanzibar linalojumuisha
timu za bara na visiwani.
No comments:
Post a Comment