Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lina imani kuwa mazungumzo kati yake,
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) yatamaliza tatizo la kushikiliwa akaunti ya TFF kutokana
na malipo ya kodi ya mishahara ya makocha wa kigeni.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga alizungumza na waandishi wa habari jana juu
ya uamuzi wa TRA kushikilia akaunti ya TFF ikiielekeza Benki ya NMB
kukata sh. 157,407,968 ikiwa ni malipo ya Kodi ya Mapato ya Mshahara wa
Mfanyakazi (P.A.Y.E) ya makocha Marcio Maximo na wasaidizi wake.
Katika
mzozo huo wa muda mrefu, TFF imejitetea kuwa haiwezi kulipa kodi hiyo
kwa kuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ndiyo mlipaji wa
mishahara ya makocha hao, ikiwa ni ahadi ya Rais wa Tanzania, Jakaya
Kikwete ya kulipia makocha wa michezo tofauti, ukiwemo mpira wa miguu.
“Hili
ni suala nyeti ambalo linahitaji kumalizwa kwa mazungumzo baina ya
pande zote. Ninataka kuwahakikishia kuwa suala hili linazungumzwa na
tayari nimeshafanya mazungumzo na maofisa wa Wizara na tumekubaliana
kukutana na pande zote wakati wowote; iwe leo jioni au kesho.
“Ni
matumaini yangu kuwa suala hili litakwisha na jana nimetoka Kampala
(Uganda kwenye Kombe la Chalenji) moja kwa moja na kwenda kuzungumza na
viongozi wa Wizara na wamekubali kwamba tuongee pande zote kulimaliza
suala hili.
“Nimezungumza
na wenzetu wa Serikali kwa sababu najua unyeti wa suala hili. Fedha
zilizokamatwa si zetu; ni fedha za klabu na zimetolewa na mdhamini
ambaye tumekubaliana namna ya kuzitumia. Fedha hizi hazikutolewa kwa
ajili ya kulipia kodi. Lakini TRA wanazishikilia kwa sababu Premier
League iko chini ya TFF,” amesema Rais Tenga.
Tenga
amesema TRA wanafanya kazi kwa kufuata sheria zao za ukataji kodi na
hivyo wana haki ya kufuatilia kwa kuwa kwa mujibu wa sheria, mwajiri
ndiye anayetakiwa kukata kodi kutoka kwenye mshahara wa mfanyakazi.
“Hivyo
hatuwezi kuilaumu TRA kwa sababu ndivyo sheria inavyosema, lakini pia
hatuna uwezo huo wa kulipa fedha hizo kwa sababu, kwanza hatuna na pili
sio sisi tunaolipa mishahara ya hawa makocha,” amesisitiza Rais Tenga.
Akizungumzia
historia ya suala hilo, Tenga aliishukuru Serikali kwa msaada ambao
imekuwa ikiutoa katika mpira na kwamba ahadi ya Rais Kikwete ya kusaidia
kulipa makocha wa timu za taifa imeusogeza mpira wa miguu karibu na
Serikali na karibu na Rais.
“Rais
Kikwete alisema wakati alipoingia madarakani (mwaka 2005) anajua kuwa
kuna tatizo kwenye mpira na akatoa ahadi ya kulipa walimu wa mpira.
Ahadi hiyo imefanya ukaribu uliopo sasa kati ya mpira na Serikali; kati
ya mpira na Rais sasa kuwa mkubwa. Serikali imechangia kwa kiasi kikubwa
kwenye mpira, yaani kulipa walimu.
“Sasa
sisi ni administrators wa hawa walimu. Tunachofanya ni kuandaa mikataba
ambayo ni standard duniani kote kwa mujibu wa taratibu za FIFA
(Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu). Kwa kawaida makocha wa
kigeni huwa wanatayarishiwa mikataba ambayo ni tax free (isiyo na kodi).
Baada ya kuingia nao mikataba, huwa tunaipeleka wizarani ambao ndio
wanawalipa makocha moja kwa moja kwenye akaunti zao,” amesema Rais
Tenga.
Katika
mkutano huo na waandishi, Rais Tenga pia aliipongeza timu ya taifa ya
Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kwa kuanza vizuri mashindano ya Kombe
la Chalenji, akisema ushindi huo ni ishara nzuri hasa kutokana na ukweli
kuwa kikosi hicho kinaundwa na wachezaji wengi chipukizi na akataka
Watanzania waendelee kuiunga mkono.
Tenga
pia alisema kumekuwepo na malalamiko kuhusu makato ya mechi na kwamba
suala hilo ni la muda mrefu na kwamba TFF imepiga hatua kubwa tangu
ilipoanza kulishughulikia.
No comments:
Post a Comment