Wachezaji wa Zanzibar Heroes wakisujudu wakati wakishangilia goli lao la kwanza lililofungwa wakati wa mechi yao ya Kundi C la Kombe la Chalenji kwenye Uwanja wa Mandela, Kampala leo. |
Nyota
wa klabu ya Azam FC ya Dar es Salaam, Khamis Mcha 'Viali' alifunga mara
mbili na kuifanya Zanzibar ifikishe pointi 4 baada ya mechi mbili na
sasa ina uhakika wa kutinga hatua ya 8-Bora hata kwa nafasi ya ‘best
looser’ kulingana na matokeo ya mechi za mwisho.
Rwanda
inayoshika nafasi ya pili ya msimamo wa Kundi C kwa kuwa pointi 3 na
Malawi iliyo katika nafasi ya tatu kwa pointi 3 pia baada ya jana
kushinda 3-2 dhidi ya Eritrea inayoburuza mkia, zinaweza kufikisha
pointi 6 zikishinda mechi zao za mwisho Jumamosi. Hata hivyo, matokeo
hayo hayataizuia Z’bar kutinga robo fainali kama ‘best looser’, endapo
itapoteza mechi yake ya mwisho Jumamosi dhidi ya Malawi.
Hali
mbaya ya uwanja iliwagharimu pia Malawi na Eritrea, ambapo katika
matukio mawili -- moja kwa kila timu -- mpira uliokuwa ikiserereka
kuingia wavuni ulikwama kwenye dimbwi la maji kabla ya kuokolewa na
mabeki wa timu hizo.
Katika
tukio la kwanza wakati Malawi wakiongoza kwa magoli 2-0 wangeweza
kufunga goli la tatu baada ya mpira kumpita kipa na mchezaji mchezaji wa
malawi kupiga shuti dogo katika lango tupu akidhani amefunga lakini
mpira ulikwama kwenye dimbwi kabla ya beki kufika na kuokoa mpira.
Tukio
jingine lilikuja wakati Eritrea wakiwa nyuma kwa magoli 2-1 na
wangeweza kufanya matokeo yawe 2-2 lakini mpira uliokuwa ukienda wavuni
ulinasa kwenye dimbwi na kuwapa nafasi Malawi kuokoa.
Zanzibar
ilipata goli la kuongoza katika dakika ya 9, shukrani kwa madimbwi ya
maji yaliyouzuia mpira usimfikie kipa wa Rwanda, Jean Claude Ndoli,
aliyekuwa katika nafasi nzuri ya kuuokoa jirani na ukingo wa boksi na
kumpa mwanya Mcha kufunga katika nyavu tupu.
Mcha alifunga goli la pili katika dakika ya 62 kufuatia pasi ndefu kutoka kulia.
Rwanda
walicharuka na kupata goli kupitia kwa Dady Birori aliyefunga kwa
kichwa katika dakika ya 80 kufuatia krosi ‘matata’ ya nahodha Haruna
Niyonzima.
Kocha
wa Rwanda, Milutin Sredjovich ‘Micho’ alisema baada ya mechi hiyo
kwamba hawezi kusingizia uwanja kwa kipigo chao kwa sababu hata
wapinzani wao walicheza katika uwanja huo huo lakini alisema mazingira
yalikuwa hayafai kuendelea kuchezewa mechi.
Michuano
hiyo inaendelea kesho kwa mechi za Kundi A ambapo Kenya itacheza dhidi
ya Ethiopia saa 10:00 jioni kabla ya wenyeji Uganda ambao tayari
wametinga robo fainali watawakaribisha Sudani Kusini saa12:00 jioni.
No comments:
Post a Comment