Wachezaji wa Simba na Yanga wakisalimiana katika moja ya mechi baina yao
DAR ES SALAAM, Tanzania
WAKATI
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF chini ya
Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa ikitarajiwa kukutana kesho Jumapili
Septemba 2 kupitia pingamizi za usajili kwa wachezaji msimu wa 2012/13,
klabu ya Yanga imeiwekea Simba pingamizi mbili.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini
Dar es Salaam leo, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kuwa,
Yanga inapinga Simba kuwaacha wachezaji Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu
Mbiyavanga na Lino Masombo.
“Pingamizi la Yanga kwa Simba kuhusu nyota
hao ni kuwa, walishapatiwa leseni za kucheza Ligi ya Tanzania
walizozitumia kwenye mashindano ya Kombe la Kagame wakiwa na Simba. Pia
inapinga Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kujiunga Simba kwa vile ana leseni ya
kuchezea Azam kwa msimu wa 2012/13,” alisema Wambura.
Pingamizi lingine la Yanga kwa Simba ni
kuwa, imezidisha idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kusajiliwa,
kwa maelezo inao nyot wanane wakati wanaoruhusiwa ni watano, ambapo
imewataja wachezaji hao kuwa ni Lino Masombo, Felix Sunzu, Emmanuel
Okwi, Mussa Mude, Kanu Mbiyavanga, Pascal Ochieng, Komalmbil Keita na
Daniel Akuffor.
Wakati yenyewe ikiweka pingamizi hizo kwa
Simba, Yanga imewekewa pingamizi mbili Kagera Sugar inayopinga usajili
wa beki David Charles Luhende kwa vile ada ya uhamisho haijalipwa, huku
Simba nayo ikipinga usajili wa Kelvin Yondani kwa madai ina mkataba naye
uliosainiwa Desemba 23, 2011.
Kwa mujibu wa Wambura, jumla ya wachezaji
17 wamewekewa pingamizi za usajili wao kwa klabu za Ligi Kuu, ambapo
Simba licha ya kupinga usajili wa Yondani, yenyewe inapingwa kuwasajili
Edward Christopher Shija na Samir Said Luhava wa Falcon ya Chakechake,
Pemba kwa madai ya kutofuatwa kwa taratibu za uhamisho wao
Azam FC kwa upande wake inapinga usajili wa
Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwenda Simba kwa maelezo bado ina mkataba
naye unaomalizika Juni 11 mwakani, wakati Simba imewasilisha malalamiko
ya mchezo usio wa kiungwana katika usajili wa Mbuyu Twite aliyeko Yanga.
Katika madai yao hayo, Simba inasema Twite
alisaini mkataba na klabu yao Agosti 1 mwaka huu mbele ya viongozi wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA) klabu ya APR, akilipwa
dola za Kimarekani 30,000 na nyingine 2,000 ikiwa ni fedha ya kujikimu
na nauli yake ya kujiunga na klabu hiyo.
Toto Africans ya Mwanza imewawekea
pingamizi wachezaji Enyinna Darlinton aliyeombewa usajili na Kagera
Sugar na Mohamed Soud anayekwenda Coastal Union kwa maelezo kuwa bado
ina mikataba na wachezaji hao, huku Rollingstone Multipurpose Ateclass
Foundation ya Arusha inapinga usajili wa Kigi Makassy.
Rollingstone inataka kulipwa fidia ya
kumlea Makassy aliyejiunga Simba akitokea Yanga, kwa kuwa mchezaji huyo
bado hajafikisha umri wa miaka 23, kama taratibu za uhamisho na matunzo
ya mchezaji zinavyoelekeza.
Aidha, Wambura aliongeza kuwa, Shirikisho
la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA), limetuma Hati ya Uhamisho wa
Kimataifa (ITC) kwa ajili ya mchezaji Ayoub Hassan Isiko aliyejiunga na
Mtibwa Sugar akitokea timu ya Bull FC ya nchini humo.
ITC hiyo ilitumwa juzi Agosti 30, hivyo
kufanya wachezaji ambao ITC hazijapatikana hadi sasa kubaki wawili tu,
huku zikiwa zimesalia siku tatu kufungwa kwa dirisha la usajili wa
wachezaji hapo Septemba 4.
Wachezaji ambao ITC zao bado hazijapatikana ni Salum Kinje na Pascal Ochieng kutoka AFC Leopards ya Kenya waliojiunga na Simba.
ITC hizo zinatarajiwa kupatikana wakati
wowote kwani tayari TFF limeshaziomba kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Kenya (FKF) baada ya nyaraka zote zilizokuwa zikitakiwa kupatikana.
No comments:
Post a Comment