DAR ES SALAAM, Tanzania
MASHINDANO ya Taifa ya Riadha
yanayotarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Taifa kuanzia Septemba 7 hadi
9, yamelilazimisha Shirikisho la Soka nchini (TFF) kusogeza tena mbele
hadi Septemba 11 kwa mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Simba na Azam FC
itakayofanyika uwanjani hapo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo,
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kuwa, jaribio lao la
kukishawishi Chama cha Riadha (RT) kumaliza kwa wakati mashindano hayo
katika siku ya mwisho ili kupisha mechi hiyo hapo Jumapili lilishindwa.
Kutoka na hali hiyo, TFF ilikubali matokeoa
na kuamua kuisogeza mechi hiyo kwa mara nyingine hadi Jumanne alasiri,
ambapo pambano hilo la kuashiria ufunguzi wa Ligi Kuu ya Vodacom
linalohusisha bingwa wa ligi hiyo Simba dhidi ya mshindi wa pili ambayo
ni Azam.
“Ligi Kuu sasa itaanza rasmi hapo Septemba
15, siku nne baada ya pambano la Ngao ya Jamii. Kanuni zinataka wiki
moja kabla ya ufunguzi kupigwa kwa Ngao ya Jamii, lakini uwapo wa
mashindano ya riadha umetulazimisha kufanya hivi. Tuna imani siku nne
zitawatosha kujiweka tayari kwa ligi,” alisema Wambura.
Mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo utamalizika
Novemba 11, ambapo pambano gumzo baina ya mahasimu wa soka la Tanzania,
Yanga na Simba zitacheza mechi ya kwanza baina yao hapo Oktoba 3 kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Aliongea kuwa, katika mechi za pazia la
ufunguzi wa ligi, mabingwa watetezu Simba watacheza na African Lyon
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku Polisi Morogoro na Mtibwa
Sugar zikitoana ngao huko Jamhuri, Morogoro.
Ratiba hiyo inaonesha kuwa, Wajelajela
waliorejea Ligi Kuu msimu huu Tanzania Prisons ya Mbeya siku hiyo
itaoneshana ubabe na Yanga huko Sokoine, Mbeya, siku ambayo pia Mgambo
JKT na Coastal Union zote za Tanga ziachuana huko Mkwakwani.
Mechi nyingine katika ufunguzi huo ni ile
baina ya maafande wa JKT Ruvu na Ruvu Shooting watakaokipiga kwenye
dimba la Chamazi Dar es Salaam, Kagera Sugar dhidi ya Azam FC kwenye nyasi za Kaitaba, Bukoba, huku Toto Africans na Oljoro JKT wakioneshana kazi huko CCM Kirumba, Mwanza.
Ligi hiyo itamalizika Mei 18 mwakani kwa
timu zote kujitupa dimbani, ambapo Toto Africans itafunga na Ruvu
Shooting CCM Kirumba, Mgambo JKT dhidi ya African Lyon huko Mkwakwani,
wakati JKT Ruvu itamaliza na Mtibwa Sugar KWENYE Uwanja wa Chamazi.
Miamba na mahasimu wa soka nchini Simba na
Yanga watafunga msimu kwa pambano baina yao kwenye Uwanja wa Taifa, huku
Tanzania Prisons itaumana na na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Sokoine,
Oljoro JKT dhidi ya Azam huko Sheikh Amri Abeid na Polisi Morogoro dhidi
ya Coastal Union, Uwanja wa Jamhuri.
Aidha, Wambura aliongeza kuwa, endapo
wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya klabu barani Afrika, Simba na
Azam hazitafanikiwa kuvuka hatua mojawapo ya michuano ya Ligi ya
Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, ratiba hiyo itafanyiwa
marekebisho.
No comments:
Post a Comment