Niger wakishangilia ubingwa wa Airtel Rising Stars Afrika 2012
NAIROBI, Kenya
MASHINDANO ya Airtel Rising Stars Afrika
2012 yaliyoshirikisha mataifa 15 barani humu yamehitimisha juzi jijini
hapa, ambapo mgeni rasmi wa fainali na nyota wa zamani wa
ManchesterUnited, Peter Schmeichel, alikabidhi medali na zawadi kwa
washindi upande wa wavulana na wasichana.
Niger walifanikiwa kutwaa ubingwa wa kwanza
wa michuano ya kwa wavulana, katika fainali ya michuano hiyo, huku
Ghana wakitawazwa mabingwa upande wa wasichana katika mashindano hayo –
yaliyoanza na timu 18,000 na kujumuisha vijana walio chini ya miaka 17
wapatao 324,000 Afrika nzima.
Niger iliifunga Zambia kwa penati 5-4
kushinda ubingwa Airetl Rising Stars 2012 kwa wavulana, baada ya
kumaliza dakika 90 bila ya kufungana licha ya kosa kosa nyingi kwa kila
timu, ambapo pia dakika 30 za nyongeza pia hazikutoa mshindi na
kulazimika kupigiana penati.
Mamane Karibou, Issa Souleymane, Abubacar
Timbo, Idrissa Amadou na Issifou Garba wa Niger walifunga penati, kama
ilivyokuwa kwa Wazambia Timothy Sakala, Thomas Juma Mutale, Dennis
Chebuye na Albert Bwalya, huku Shadrack Chimanya akikosa mkwaju wake
muhimu.
Katika fainali ya wasichana, Ghana walitoka
nyuma na kuwafunga wenyeji Kenya waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya
kushinda na kuwachapa mabao 2-1.
Kenya walipata bao la uongozi lililowekwa
nyavuni na Vivian Odhiambo dakika ya 27, kabla ya Emelia Lokko
kuisawazishia Ghana 43 na pambano kuingia mapumziko kwa sare ya bao 1-1.
Ghana ikarejea kipindi cha pili ikiwa tishio zaidi, ambapo Patience
Narh aliifungia bao la ushindi 56 na kuwaduwaza Wakenya.
Wachezaji vijana 432 walishiriki fainali
hizi jijini Nairobi kwa wiki nzima, wakiwezeshwa katika kila mahitaji na
wadhamini, waratibu na waendeshaji wa michuano hiyo kampuni ya simu za
mkononi ya Airtel, huku vijana hao wakionyesha vipaji vya hali ya juu na
kutoa taswira njema ya soka la Afrika.
Mabingwa Niger na Ghana walizawadiwa fedha
taslimu dola za Kimarekani 10,000 kila moja, huku zikipata fursa kwa
wachezaji wake wote kushiriki Kliniki Maalum itakayofanyika hapa Nairobi
na Accra, Ghana, chini ya wakufunzi wa soka kutoka klabu za Arsenal na
Manchester United za England.
No comments:
Post a Comment