Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, akisalimiana na waislamu mbalimbali baada ya Swala ya Ijumaa huko msikiti wa Mtoro, mtaa wa Mahiwa, Kariakoo jijini Dar es Salaam leo.
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, akisalimiana
na Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi
Tuvako Manongi walipokutana katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam
leo kwa ajili ya kuagana. Kulia ni Naibu Mwakilishi wa kudumu wa
Tanzania Katika Umoja huo, Ramadhan Muombwa Mwinyi.
,
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad akizungumza na Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi na Naibu wake Ramadhan Muombwa Mwinyi (katikati), walipokutana katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam leo. (Picha zote na Salmin Said, OMKR)
Na Hassan Hamad, OMKR.
DAR ES SALAAM
24/08/2012.
MAKAMU
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema kazi
kubwa inayowakabili wawakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa ni
kutetea maslahi ya Tanzania katika Umoja huo.
Amesema
Tanzania pamoja na nchi nyengine zinazoendelea zinakabiliwa na
changamoto nyingi, lakini njia pekee ya kutatua changamoto hizo ni
kushirikiana na kutetea maslahi ya nchi zao na Afrika kwa ujumla.
Maalim
Seif ametoa changamoto hiyo katika hoteli ya Serena jijini Dar es
Salaam leo, alipokutana na Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja
wa Mataifa balozi Tuvako Manongi na msaidizi wake Mhe. Ramadhan Muombwa
Mwinyi walioteuliwa hivi karibuni kushika nyadhifa hizo.
Amesema
licha ya kuwa wana kazi kubwa ya kufanya kutokana na changamoto nyingi
zilizopo, lakini wanaweza kufanikisha majukumu yao vizuri iwapo
watashirikiana vyema na wawakilishi wengine kutoka nchi zinazoendelea.
“Nchi
zinazoendelea ni nyingi mno, nazo zina wawakilishi wao katika Umoja wa
Mataifa, iwapo mtashirikiana vyema na wenzenu hawa wan chi nyingine,
mtaweza kutatua kero zilizopo kwa urahisi”, alinasihi Maalim Seif.
Amesema
nchi zinazoendelea zinakabiliwa na matatizo yanayofanana, na kwamba
masuala yanayopaswa kupewa kipaumbele kwa sasa ni pamoja na mapambano
dhidi ya janga la UKIMWI pamoja na mabadiliko ya tabia nchi.
Amewatakia
kheri wawakilishi hao wa Umoja wa Mataifa, na kuahidi kutoa ushirikiano
unaohitajika wakati wowote katika kusogeza mbele maendeleo ya
Tanzania kwenye Umoja huo.
Kwa
upande wake balozi Manongi amesewa watatumia uzoefu walionao katika
kufanikisha majukumu waliyopewa, na kuomba ushirikiano wa karibu kutoka
kwa viongozi wa nchi.
Nae
Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja huo Mhe. Ramadhan
Muombwa Mwinyi amepongeza kitendo cha kukutana na viongozi mbali mbali
wakiwemo Makamu wa Kwanza na Makamu wa Pili wa Rais, na kwamba mawazo
waliyoyapata kutoka kwao yatakuwa ni dira ya utekelezaji wa majukumu
yao.
Wawakilishi
hao wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa walionana na Makamu wa Kwanza
wa Rais kwa ajili ya kuagana nae wakati wakijiandaa kuelekea katika
kituo chao kipya cha kazi mjini New York, Marekani mwishoni mwa mwezi
huu.
Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais ametoa wito kwa waislamu kuungana na kuwa kitu kimoja ili kuipa nguvu zaidi dini hiyo.
Amesema
ni jambo la kusikitisha kuona waislamu nchini wamekosa mshikamano,
umoja na upendo, na hatimaye kushabikia mifarakano isiyokuwa na manufaa
yoyote kwa waislamu.
Maalim
Seif ametoa kauli hiyo, wakati akiwasalimia waislamu baada ya sala ya
Ijumaa huko msikiti wa Mtoro mtaa wa Mahiwa, Kariakoo jijini Dar es
Salaam.
Amesema
wakati umefika kwa Waislamu kushikamana, na kutoa wito kwa Masheikh
kuwaunganisha wafuasi wao, ili kuwa kitu kimoja kwa lengo la kuongeza
nguvu katika kuuendeleza Uislamu.
Pia
Makamu wa Kwanza wa Rais amewataka waislamu kuitumia fursa iliyopo ya
kutoa maoni katika tume ya mabadiliko ya katiba, ili kuelezea kero
zinazowakabili na kupelekea kupatikana kwa katiba itakayojali matakwa
yao.
Amesema
katika kufikia matarajio hayo, viongozi wa dini wana wajibu wa
kuwaandaa wafuasi wao katika kutoa maoni ya katiba, kwa vile wengi wao
hawaifahamu katiba ya sasa na changamoto zilizopo.
Katika
hotuba yake Imamu wa Msikiti huo Sheikh Zubeir Yahya amesema kuna haja
kwa viongozi wa kiislamu kukaa pamoja na kutoa msimamo wa pamoja juu ya
masuala mbali mbali ya kijamii likiwemo la sense, ili kuepuka
kuwapotosha wananchi kwa kutolewa misimamo tofauti ya viongozi wa dini
moja.
Aidha
Sheikh Zubeir amewatanabahisha waislamu kujipanga ili kuanzisha vyuo
vikuu vya kiislamu nchini pamoja na vyuo vya taaluma mbali mbali, ili
kuwaandaa vijana wa kiislamu kuifahamu dini yao na kuwawekea misingi
imara ya kuiendeleza.
No comments:
Post a Comment