Kiungo wa Uholanzi, Nigel de Jong kushoto akichuana na mshambuliaji wa Ubelgiji
AMSTERDAM, Uholanzi
NAHODHA
mpya wa timu ya taifa ya Uholanzi, Wesley Sneijder, ameshindwa kujizuia
na kuwataja Nigel de Jong na Maarten kama waliochangia kufungwa mabao
4-2 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Ubelgiji kwenye Uwanja wa Roi
Baudouin.
Sneijder
aliyetangazwa siku moja kabla ya mechi na kocha Louis van Gaal kurithi
unahodha ulioachwa na Mark van Bommel aliyestaafu soka, amesema ni kweli
‘walipoteana’ kipindi cha kwanza, lakini makosa ya kizembe ya nyota hao
yaliwaponza hata waliporejea mchezoni kipindi cha pili.
“Ni kweli
hatukucheza vema kwa dakika 45 za kwanza. Lakini tulikuwa bora zaidi
dimbani katika kipindi cha pili, lakini lazima niseme kwamba tumeponzwa
na makosa binafsi ya kiungo Nigel de Jong na mlinda mlango Maarten
Stekelenburg,” Sneijder aliwaambia waandishi wa habari wa Uholanzi.
Mkali huyo
aliyecheza mechi ya 87 akiwa na jezi za taifa za Uholanzi, aliumwagia
sifa mfumo bora wa ufundishaji na upangaji kikosi wa kocha wake Louis
van Gaal, licha ya kujikuta wakiangukia pua katika mechi hiyo.
“Nadhani
mfumo mpya wa kocha umeifanya timu kuwa bora na imara kimchezo na
kimbinu (akiuzungumzia mfumo wa 4-3-3 badala ya ule wa 4-2-3-1
ulioiponza timu kwenye mashindano ya Euro 2012).
“Tulikuwa
na nafasi nyingi za kufunga ambazo hatukuzitumia, lakini kimsingi
tulicheza vema kwa muda fulani,” alihitimisha Sneijder.
Ubelgiji
waliokuwa nyumbani, walimaliza dakika 45 za kwanza wakiwa mbele kwa bao
la Christian Benteke, ambapo kipindi cha pili Uholanzi ikasawazisha kwa
bao Luciano Narsingh dakika ya 54, kabla ya Klaas-Jan Huntelaar kufunga
la uongozi kwa Oranje.
Ndipo De
Jong alipotoa ‘boko’ kwa Dries Mertens, ambaye alijivuta kwa kasi
kuingia ndani ya boksi na kufumua shuti kuisawazishia Ubelgiji, kabla ya
Romelu Lukaku kuifungia bao la tatu. Kipa wa Uholanzi, akafanya kosa
lililozaa bao la nne na kumfanya Sneijder afure kwa hasira.
No comments:
Post a Comment