MMILIKI wa timu ya African Lyon,Rahim Kangezi ametamba kwamba kikosi chake kipo imara na itaifundisha soka timu ya Yanga katika mchezo utakao fanyika Jumapili kwenye uwanja wa Taifa,Dar es Salaam.
Kangezi ameeleza hayo jana wakati akizungumza na gazeti hili kwamba kikosi chao kipo imara baada ya kukamilika zoezi la usajili na kupatikana kwa kocha mpya.
Alisema kwamba baada ya kuanza mazoezi ya nguvu,wapo tayari kwa ajili ya kupambana na Yanga siku hiyo ambapo wamepania kufanya kweli huku wakipanga kuwatumia baadhi ya nyota waliowasajili.
"Tuna wachezaji watatu kutoka nje ya nchi,wakiwemo wa Kenya na Uganda,Pablo Velez ameanza kufanya vitu vyake na siku hiyo tutamtangaza Mkurugenzi wetu mwingine mpya ambaye ni mwanamke,"alisema Kangezi.
Ametamba kuwa wao wamefanikiwa zaidi baada ya kuwasajili wachezaji wengi kinda ambao ana uhakika wataweza kufanya vizuri katika mchezo huo dhidi ya Yanga.
Mmiliki huyo amevitaja viingilio kwenye mchezo huo ni shilingi 15,000 VIP A wakati VIP B ni shilingi 10,000 huku upande wa viti vya rangi ya machungwa ni shilingi 5,000 na mzunguko shilingi 3,000 na kuwataka mashabiki wa soka kufika kwa wingi ili kuona jinsi kikosi chao kitakachotoa dozi kwa Yanga.
No comments:
Post a Comment