Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA), Jerome Valcke atawasili nchini Mei 1 mwaka huu ambapo atafungua
semina ya mawasiliano itakayoshirikisha viongozi wa vyama wanachama wa Baraza
la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Akizungumza Dar es Salaam leo (Aprili 14 mwaka
huu), Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema
Valcke ambaye hii ni mara yake ya kwanza kuja Tanzania atafuatana na maofisa
wengine wa saba wa FIFA.
Amesema semina hiyo iliyoandaliwa na FIFA itafanyika
kwa siku mbili (Mei 1 na 2 mwaka huu) ambapo vilevile Valcke atapata fursa ya
kuzungumza na waandishi wa habari wa ndani na wa kimataifa.
Rais Malinzi amesema washiriki wa semina hiyo ni
marais, makatibu wakuu na wakuu wa mawasiliano wa wanachama 12 wa CECAFA ambao
ni Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somali, Sudan, Sudan
Kusini, Tanzania na Uganda.
Naye Mwenyekiti wa CECAFA, Leodegar Tenga ambaye
alifuatana na Katibu Mkuu wake Nicholas Musonye amemshukuru Rais wa TFF kwa
kukubali kuwa mwenyeji wa semina hiyo kwani itasaidia katika maendeleo ya mpira
wa miguu katika ukanda huu.
RAMBIRAMBI MSIBA WA JOSEPHAT MAGAZI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea
kwa masikitiko kifo cha Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu
(FRAT) Mkoa wa Singida, Josephat Magazi kilichotokea jana mkoani Kilimanjaro.
Magazi
ambaye pia aliwahi kuwa mwamuzi na kamishna wa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom
(VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) alikuwa amelazwa katika Hospitali ya KCMC.
Mazishi yatafanyika kesho (Aprili 15 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwao Ushirombo
mkoani Shinyanga.
Msiba
huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Magazi
alishirikiana na TFF na wadau wengine wa mpira wa miguu katika masuala ya
uamuzi na uongozi, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF
tunatoa pole kwa familia ya marehemu Magazi, FRAT na Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Singida (SHIREFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika
kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Bwana
alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment