Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, April 18, 2014

Manny Pacquiao Ngumi zake nyepesi kama karatasi Wachambuzi watilia shaka uwezo wake Huenda asimvutie mbabe Mayweather

Manny Pacquiao

Ngumi zake nyepesi kama karatasi

 Wachambuzi watilia shaka uwezo wake

 Huenda asimvutie mbabe Mayweather


LAS VEGAS, Marekani

BONDIA Manny Pacquiao amerejea ulingoni na kupigana kwa kiwango bora, lakini alianza kurusha makonde taratibu mithili ya mtoto anayejifunza kutembea.
Hakuwa na kasi iliyozoeleka kama ya mwaka 2008/2009, wakati alipoonyesha umahiri ulingoni mara zote kiasi cha kulinganishwa na enzi za Mike Tyson.
Pacquiao huenda asirudi katika makali hayo tena, lakini ataendelea kuwa moja ya mabondia bora duniani kutokana na kile alichofanya Jumamosi iliyopita mbele ya mashabiki 15,601 kwenye ukumbi wa MGM Grand Garden.
Alimtandika makonde ya kutosha Timothy Bradley, na kushinda kwa pointi 119 dhidi ya 109 na kutwaa taji la WBO ambalo alipoteza kwa mpinzani wake huyo mwaka 2012.
Wengi waliamini bondia huyo raia wa Ufilipino alishinda pambano hilo, lakini majaji walimnyima ushindi.
Pacquiao mwenye sifa ya kutumia vizuri pembe za ulingo wa ngumi alimfumua Bradley na kuzima mbinu zake.
Bradley alimshambulia Pacquiao, kwa kumpiga ngumi kali, na kuelekea kumaliza pambano hilo.
Katika raundi ya nne, alimchanganya Pacquiao kwa kumpiga sumbwi zito kichwani na Pacquiao akainama, lakini Mfilipino huyo aliinuka haraka.
"Nafikiri alifanya vizuri kidogo, lakini hakutarajia ile staili," alisema kocha wa Pacquiao, Freddie Roach. "Ilituogopesha kidogo, kwa sababu tulidhani ameumizwa kwa ngumi. Hatukudhani angerudi nyumbani akiwa anashangilia."
Licha ya maelezo hayo ya Roach, Pacquiao alishindwa kupigana kwa kasi yake kabla ya kuzinduka na kumdunda konde zito la kushoto Bradley, ambalo ilidhaniwa lingemdondosha na kumaliza pambano.
Bradley alisema Pacquiao alimpiga ngumi nzito sana na kuongeza kuwa, makonde mengi ya mpinzani wake hayakuwa makali kama alivyokuwa zamani.
"Ngumi zake hazikuwa za haraka," alisema Bradley, japokuwa amekubali kuwa 'muziki' wa Pacquiao ulikuwa unatisha walipozipiga katika pambano la mwaka 2012.
Lakini matokeo hayaongopi. Tangu 2010 mwanzoni, Pacquiao katika mapambano sita aliyopigana hakuna ambalo ameshinda kwa 'KO'.
Ingawa kocha Roach amesema anachofikiri yeye, "Sumu ya Manny (Pacquiao) bado haijakwisha," lakini ukweli unabaki kama ulivyo ni kwamba madhara ya ngumi zake hayafanani na ilivyokuwa miaka michache iliyopita.
Mabondia hawaugulii maumivu kama alivyokuwa akiwatandika ngumi zake nzito.
"Bado ni bondia bora, dhahiri yupo imara, lakini kwa kawaida, inashangaza ngumi zake zenye nguvu zimeenda wapi," Makamu wa Rais wa Kampuni ya Top Rank, Carl Moretti alisema.
Kilichofanya Pacquiao kuwa miongoni mwa mabondia bora na maarufu duniani ni kuamini 'miguvu' aliyokuwa nayo kipindi alipokuwa anawaangusha wababe wengi wa ngumi.
Alikuwa kamili, anapiga ngumi nzito za kudondosha mpinzani mara moja na pambano kumalizika punde.
Hakuwa bondia mwenye sifa hizo, japokuwa ni miongoni mwa wapiganaji wanaoongoza kwa ubora.
"Pacquiao alipigana vizuri usiku huu na alionyesha alivyojiandaa," alisema Bradley, ambaye aliumia kiwiko cha kulia katika raundi ya kwanza lakini baadaye aligoma kuzungumzia jeraha hilo.
"Jamaa bado anatisha. Moja ya sababu ya kumpenda sana Pacquiao hadharau mpinzani.
"Siku zote anataka kukabiliana na mabondia bora, ambaye mmoja wao amepambana naye usiku huu. Amekuwa bora na ndiyo maana mahiri sana."
Mpaka katika raundi ya sita mabondia hao walikuwa wanakaribiana pointi, Pacquiao alikuwa na 58, mpinzani wake 56. Lakini Pacquiao alicharuka na kuibuka kidedea.
Alitumia vyema raundi ya saba, nane na tisa, 10 hadi ya 12. Licha ya kuongoza, ngumi za Pacquiao hazikuwa kama zile ambazo mashabiki wake walizoea kuziona.
Alifanya kazi yake vizuri, lakini hakuwa na kitu cha pekee kulinganisha na wakati alipopewa hadhi ya kuwa Bondia wa Muongo.
Jambo lingine alikuwa muoga kuingia kwenye mikono ya mpinzani wake kwa kuwa hakutaka kuumizwa, hasa wakati Bradley alipokuwa anarusha makonde, ameshinda lakini si kwa ngumu zenye ladha.
"Sikutaka kuwa mzembe," alisema Pacquiao, ambaye alipigwa kwa 'KO' mwaka 2012 na Juan Manuel Marquez na alipoteza fahamu kwa muda kutokana na kupigwa konde la kulia kichwani.
Kulingana na orodha ya mabondia bora, ni wazi Pacquiao yumo, lakini hamfikii hata chembe hasimu wake, Floyd Mayweather.
Kiwango kimeporomoka, japo, Pacquiao kuna wengine wanasema ni 'nusu Tyson'. Amebakisha miezi michache kufanya sherehe ya kutimiza miaka 36 na mpaka akipanda ulingoni tena inapita miaka tangu aliposhinda kwa 'knockout'.
Kwa umri wake bado ana nafasi ya kujirekebisha kwa kufanya 'tizi' gumu na kurudisha mvuto kwa mashabiki wake hata kulipa viiingilio vikubwa kwa ajili ya kuona mapambano yake.
Floyd Mayweather bondia anayetajwa kuwa ni bora wakati wote ulimwenguni katika uzani anaocheza, huenda asipigane na Pacquiao kutokana na kiwango cha kawaida kilichoonyeshwa na Mfilipino huyo.
Japokuwa Pacquiao amekaribisha ombi la bondia yeyote mwenye nia ya kupigana naye, huku akimlaumu Mayweather kwa kupiga chenga miaka mingi kuhusu pambano lao, hakupigana kiasi cha kumshawishi Mmarekani huyo atamani wazipige.
Mayweather hakuwepo ukumbini wakati wa pambano hilo hali inayotia wasiwasi kama atakubali kucheza na Pacquiao. Nafasi nyingine ipo kwa Marquez, ambaye kama atakubali kudundana na Pacquiao, itakuwa mara ya tano.
Mfilipino huyo katika pambano lake la wiki iliyopita alichanika nyama ya juu ya jicho na kushonwa nyuzi kadhaa.
HISTORIA YAKE
Pacquiao alizaliwa Desemba 17, 1978, huko Kibawe, Bukidnon, Ufilipino.
Ni mtoto wa Rosalio Pacquiao na Dionesia Dapidran-Pacquiao. Wazazi wake waliachana wakati bondia huyo alikuwa darasa la sita, baada ya mama yake kubaini mumewe alikuwa anaishi na kimada.
Mtoto wa nne kati ya sita kutoka tumboni kwa mama yake: Liza Silvestre-Onding na Domingo Silvestre (ndugu zake waliozaliwa kwa mume wa kwanza wa mama yake) na Isidra Pacquiao-Paglinawan, Alberto "Bobby" Pacquiao na Rogelio Pacquiao.
Pacquiao ni mume wa Maria Geraldine "Jinkee" Jamora, na wamezaa watoto wanne: Emmanuel Jr. "Jimuel", Michael, P

rincess, na Queen Elizabeth "Queenie."
Anaishi kwenye mjengo wake huko General Santos City, Kusini mwa Cotabato, Ufilipino.
Baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Sarangani, kwa sababu za kiofisi amehamia Kiamba, Sarangani, nyumbani kwa mke wake.
Ni muumini wa dhehebu la Kanisa Katoliki, Pacquiao ingawa katika siku za karibuni anasali katika kanisa la Waprotestant.

MAKALA HII KWA HISANI YA BURUDANI.
NA BAADHI YA DVD ZAKE ZA BONDIA HUYO PACQUAIO

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...