Baadhi
ya wanakijiji wa kijiji cha Usoha Njiapanda, Wilaya ya Mbeya Vijijini
wakizungumza katika mkutano na mwandishi wa habari hizi juu ya
changamoto anuai za huduma za kijamii kijijini hapo.Mwenyekiti
wa Kijiji cha Usoha Njiapanda, Willson Mwamunyila (katikati) pamoja na
wanakijiji wenzake wakizungumza na mwandishi wa habari hizi. Mratibu wa Elimu Kata ya Tembela, Antony Mwaikwila akizungumza na mwandishi wa habari hizi.
WANAVIJIJI wa
vijiji vya Shibolya, Usoha Njiapanda, Simambwe, Ikhoho na Ilembo Usafwa
vyote vya wilayani Mbeya Vijijini wametupiana lawama kuhusiana na
baadhi ya wazazi na viongozi wa vijiji kuwa wakifumbia macho watu
wanaotuhumiwa kuwatia mimba wanafunzi wa msingi na sekondari na
kuwakatisha masomo.
Kauli
hiyo imetolewa juzi na baadhi ya wanakijiji walipokuwa wakifanya
mazungumzo na mwandishi wa habari hizi Wilaya ya Mbeya Vijijini kwa
vyakati tofauti alipotembelea vijiji hivyo kuangalia changamoto za
elimu.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti baadhi ya wanavijiji walisema idadi kubwa ya
wanafunzi wanaotiwa mimba na kukatishwa masomo ya shule za msingi na
sekondari wamekuwa wakirudi vijijini na kulea watoto huku kukiwa hakuna
hatua zozote za kisheria zinazochukuliwa kwa wanaotuhumiwa kuwatia
mimba.
Greyson
Ngolia wa Kijiji cha Shibolya alisema katika kijiji hicho wapo
wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao wanalea watoto wao baada
ya kutiwa mimba na kukatiswa masomo yao.
“…Hapa
kijijini tunao hadi wanafunzi wa shule za msingi ambao wametiwa mimba
na kukatishwa masomo, wanalea watoto wao nyumbani hakuna hatua zozote
zinazochukuliwa iwe kwa mzazi wala waliowatia mimba na wengine wapo hapa
hapa,” alisema Ngolia.
Eliud
Mwakilasa mkazi wa Kijiji cha Usoha Njiapanda alisema katika kijiji
hicho hakuna hatua zinazochukuliwa kwa wanafunzi wanaopata mimba kuanzia
kwa viongozi wa kijiji, wazazi na wala uongozi wa shule husika
anaposoma mtoto.
Naye
Maria Kolneri wa Kijiji cha Usoha Njiapanda alisema katika kijiji hicho
hakuna utamaduni wa kuwashtaki watu wanaotuhumiwa kuwatia mimba
wanafunzi na suala hilo linaogopwa na kila mmoja kwa kile kuhofia
kutengwa.
“…Hapa
kijijini hakuna utaratibu huo wa kuwashtaki waliowatia mimba wanafunzi
watu wanaogopa kulaumiwa kuanzia viongozi wa kijiji na hata wazazi wa
mtoto anayekuwa ametiwa mimba, kiujumla tunaogopana,” alisema Bi.
Kolneri.
Faustina
Nafasi toka Kijiji cha Simambwe alisema idadi kubwa ya wanafunzi
wanaopata mimba usababishwa na umbali wa shule wanazosoma, ambapo baadhi
yao wamelazimika kupanga kwenye vyumba karibu na shule (yaani mageto)
jambo ambalo linachangia idadi kubwa kurubuniwa kwa kukosa uangalizi wa
karibu toka kwa wazazi/walezi.
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Usoha Njiapanda, Willson Mwamunyila alikiri kuwepo na
matukio ya kesi za mimba kwa wanafunzi katika eneo lake na vijiji
vinavyomzunguka lakini alisema hali ya kushindwa kuwashughulikia
wanaowatia mimba wanafunzi huchangiwa na ushirikiano mdogo toka kwa
wazazi wa watoto.
“…Unakuta
umeletea taarifa ya mimba kwa mwanafunzi toka shuleni, ukienda kwa
mzazi anasema hajui aliyemtia mimba mwanaye na vile vile mtoto anasema
aliyempa mimba hamjui sasa mazingira kama hayo mnashindwa pa kuanzia,
maana hakuna ushirikiano…wawazi na wanafunzi binafsi ndio nawaona
kikwazo,” alisema Mwamunyila.
Kwa
upande wake Mratibu wa Elimu Kata ya Tembela, Antony Mwaikwila alikiri
uwepo wa matukio ya mimba katika shule anazozisimamia na takwimu
zimekuwa zikitofautia kila mwaka, licha ya kesi nyingi kushindwa
kushughulikiwa kwa kile kukosa ushirikiano.
Alisema
kesi nyingi hata zikifika polisi huishia kituoni maana wanafunzi wengi
wanaotiwa mimba hudai hawawajui waliowapa mimba hivyo kukosa ushahidi.
“…Mfano mwaka 2013 Shule ya Sekondari Shibolya tulipata taarifa ya mimba
tatu lakini watoto walipinga kuwa hawawajui waliowapa mimba hivyo kesi
kuishia njiani, zipo kesi zinafunguliwa lakini zinaishia njiani kwa
kukosa ushahidi.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa kushirikiana na TGNP
No comments:
Post a Comment