1. Jeshi la Polisi Nchini,
linawakumbusha wananchi wote kuwa, tunapoelekea kipindi hiki cha sikukuu
za Christmas na Mwaka Mpya itakayoadhimishwa kati ya tarehe 24-26
Disemba, 2012 na tarehe 01 Januari, 2013 wanatakiwa kusherehekea sikukuu
hizo kwa amani na utulivu pasipo vitendo ama viashiria vyovyote vya
uvunjifu wa sheria. Wananchi wote wachukue tahadhali kwa kushirikiana na
Jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa vitendo vyote vya uhalifu na wahalifu
kwenye maeneo mbalimbali vinadhibitiwa.
2. Ikumbukwe kuwa, wananchi wenye imani ya Kikristo na hata
madhehebu mengine hutumia muda huo kwenda kuabudu pamoja na muendelezo
wa sherehe hizo kwenye maeneo mbalimbali ya starehe, uzoefu unaonyesha
kuwa baadhi ya watu hutumia kipindi hicho cha sikukuu kufanya matukio ya
uhalifu kutokana na mikusanyiko hiyo ya watu.
3. Jeshi la Polisi limejipanga
kikamilifu kuhakikisha kwamba wananchi kote nchini wanasherekea sikukuu
hizo kwa amani na utulivu, ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote ya
kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine yote
ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.
4. Aidha, tunawatahadharisha wale
wote ambao watakuwa wakitumia barabara, kuwa makini kwa kuzingatia
sheria za usalama barabarani, madereva kuepuka kwenda mwendo kasi na
kutumia vilevi wawapo kazini.
5. Katika kuhakikisha usalama
kwenye kumbi za starehe, wamiliki wa kumbi hizo wazingatie uhalali na
matumizi ya kumbi zao katika uingizaji wa watu kulingana na uwezo wa
kumbi hizo, badala ya kuendekeza tamaa ya fedha kwa kujaza watu kupita
kiasi. Vilevile, wazazi wawe makini na watoto wao na hasa disko toto na
kutokuwaacha kutembea peke yao, ili kuepuka ajali na matukio mengine
yanayoweza kusababisha madhara juu ya watoto hao.
6. Wananchi wote wanakumbushwa
kwamba, watokapo kwenye makazi yao wasiache nyumba wazi ama bila mtu na
endapo kuna ulazima wa kufanya hivyo watoe taarifa kwa majirani zao, na
pale wanapowatilia mashaka watu wasiowafahamu wasikae kimya bali watoe
taarifa kwa Jeshi la Polisi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa haraka
kwa wahusika kupitia namba simu 0754 785557 ama namba za viongozi wa
polisi zilizokwishatolewa hapo awali.
7. Jeshi la Polisi linatoa wito
kwa taasisi mbalimbali za serikali, madhehebu ya dini, asasi za kiraia,
vyama vya siasa, vyombo vya habari, makampuni binafsi ya ulinzi na
wananchi kwa ujumla, kuendelea kutoa ushirikiano na hasa katika kipindi
cha mwisho wa mwaka, ili kuhakikisha usalama wa nchi yetu unadumishwa na
raia wote wema wanaishi kwa amani na utulivu bila hofu ya uhalifu.
8. Mwisho, nawahakikishia
wananchi kwamba, Jeshi la Polisi linatekeleza majukumu yake kwa
kuzingatia sheria za nchi na hivyo halitawajibika kumwonea huruma ama
upendeleo mtu yeyote atakayeenda kinyume na sheria.
NAWATAKIENI WATANZANIA WOTE KHERI YA CHRISTMAS NA MWAKA MPYA.
Advera Senso-ASP
Msemaji wa Jeshi la Polisi (T)
POLISI MAKAO MAKUU.
Msemaji wa Jeshi la Polisi (T)
POLISI MAKAO MAKUU.
No comments:
Post a Comment