Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa
Nchini (TPBC) inamaliza mwaka 2012 na mafanikio lukuki ikiwa imeweza
kuiletea nchi ya Tanzania mapambano makubwa ya kimataifa zaidi ya
matano.
Haya ni mafanikio ambayo
yanapaswa kusifiwa na watanzania wote wapenda maendeleo kwani kutokana
na mapambano hayo nchi imeweza kujulikana kimataifa, vivutio vyake vya
utalii vimeweza kujulikana, nchi imeweza kuwatengenezea vijana ajira, na
kuweza kupunguza uhalifu kwa kuweza kuwapa vijana kazi kwani kukaa kwao
bure ni kishawishi tosha cha kutumia nguvu zao kwa shughuli ambazo sio
za maendeleo.
Katika mwaka unaoishia Desemba
31, 2012, TPBC imeweza pia kuwapeleka nje mabondia zaidi ya 15
wakiiwakilisha nchi ya Tanzania ambako waliweza kuitangaza nchi ya
Tanzania vizuri na kuwavutia wageni wakitalii na kuwekeza katika nchi
hii inayojulikana kama kisiwa cha amani katika bara la Afrika.
Aidha, TPBC imeweza kuhudhuria
mikutano mitatu mikubwa ikiwa ni pamoja na mkutano wa Bodi ya
Wakurugenzi wa Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC) katika jiji la
London, Uingereza na ule wa mwaka wa Baraza la Ngumi la Jumuiya ya
Madola uliofanyika nchini Bahamas.
Kadhalika TPBC iliwakilishwa
kwenye mkutano wa 30 wa Shirikisho la Ngumi la Kimataifa na Chana cha
Ngumi Cha Marekani (IBF/USBA) uliofanyika katika jiji la Honolulu,
jimbo la Hawaii nchini Marekani pamoja na ule wa Baraza la Ngumi la
Dunia (WBC) uliofanyika pia katika mjiji la Las Vegas, nchini Marekani.
Hapa nyumbani , TPBC iliweza
kutoa vibali na kusimamia mapambano mengi yaliyofanyika katika miji ya
Tanga, Dar-Es-Salaam, Morogoro, Songea, Mbeya, Morogoro na Arusha na
kuweza kuwapatia mabondia wengi wa kitanzania mikanda ya Kanda, Taifa
na Afrika ya Mashariki, Kati na bara la Afrika.
No comments:
Post a Comment