MSANII wa muziki wa kizazi
kipya, Bernard Paul ‘Ben Paul’, anatarajiwa kuwasindikiza warembo wa
kinyang’anyiro cha Redd’s Miss Uni-college Temeke kitakachofanyika kesho katika
ukumbi wa Club Bilicanas, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa
habari Dar es Salaam jana, mratibu wa shindano hilo, Florence Josephat,
alisema kuwa maandalizi yote yamekamilika na kwamba kilichobaki ni shoo yenyewe
ambayo alitamba itakuwa katika ubora wa hali ya juu.
Alisema kuwa jumla ya warembo
13 wanatarajia kupanda jukwaani siku hiyo, ikiwa ni baada ya kunolewa vilivyo
kwa takribani wiki tatu na kwamba wameiva kuwapagawisha watakaofika kushuhudia
uhondo huo.
“Maandalizi yote yamekamilika
hivyo tunawaomba wapenzi wa burudani na urembo kwa ujumla kujitokeza kwa wingi
siku hiyo kwani kipenzi cha warembo, Ben Paul, atatoa burudani ya hali ya juu
itakayoambatana na shoo kutoka kwa warembo wetu kutoka vyuo vitano vilivyopo Temeke,”
alisema.
Alivitaja baadhi ya vyuo
hivyo kuwa ni Chuo Kikuu cha Uganda, TIA, Chuo cha Bandari, DUCE na Chuo cha
Utalii, huku akitamba kuwa kutokana na ubora wa warembo walionao, wana imani
mwaka huu Redd’s Miss Tanzania atatoka katika kitongoji chao hicho.
Florence ambaye alikuwa mshiriki wa fainali za Miss Tanzania
2008, aliwataka wapenzi wa urembo na burudani, hasa wanafunzi wa sekondari na
vyuo, kujitokeza kwa wingi siku ya shoo yao
ili kujionea warembo bomba, huku wakipata burudani ya aina yake.
Alitaja kiingilio cha shoo yao kuwa ni Sh 10,000 na
kwamba mbali ya kinywaji cha Redd’s ambao ndio wadhamini wakuu wa mashindano
hayo, wadhamini wengine ni Shome Decoration & Catering,
djfetty.blogspot.com na Lamada Hotel.
No comments:
Post a Comment