Na Mwandishi Wetu, Kondoa
MWENYEKITI wa Wazazi Mkoa wa Tanga, Dk. Edmund
Mndolwa, ameahidi kuinua uchumi wa Mkoa wa Tanga kupitia kilimo cha biashara
ili kuwakomboa vijana kiuchumi.
Akizungumza wakati wa kujifunza kilimo cha
biashara katika Kata ya Kwadelo, wilayani Kondoa, alisema elimu aliyoipata
ataipeleka mkoani Tanga ili vijana wa mkoa huo nao waweze kunufaika.
Mndolwa ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu
ya CCM (MNEC), aliongozana na madiwani wawili akiwamo Diwani
wa Kerenge, Shebila Iddi na Diwani wa Mnyazi, Muhidin Rajabu, ambapo
walitembelea shamba la Halima Selemani
lenye ukubwa wa ekari 60 lililokuwa limelimwa alizeti.
Mndolwa alisema licha ya kata yake kuwa na eneo
dogo la shamba yuko tayari kutafuta sehemu nyingine na kulitumia kwa kilimo cha
alizeti ili kuleta tija kwa jamii na taifa kwa ujumla.
“Kwa kweli leo nimejifunza kitu maana mafunzo
yenu yamenishangaza na ninaamini yatakuwa na manufaa makubwa kutokana na elimu
tuliyoipata,” alisema.
Diwani wa Kwadelo, Omary Kariati, alisema
wananchi wakipewa elimu juu ya matumizi ya kitu chochote chenye masilahi ya
maisha yao
huitikia kwa haraka na hatimaye maendeleo hujitokeza.
“Katika kata yangu wananchi wamejitahidi
kujitoa katika kilimo na kuhakikisha wanaondokana na tatizo la njaa kwa kila
mwaka kupitia mradi wa Kilimo Kwanza,” alisema Kariati.
No comments:
Post a Comment