Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, May 22, 2013

MAONI YA CARTHBERT KAJUNA KUHUSU TAALUMA YA UANDISHI WA HABARI NDANI YA MAGAZETI TANDO/MITANDAO YA KIJAMII

Kajunason
Watu wengi kwa sasa wameibuka na kutokea kuipenda fani ya uandishi wa habari bila kujua misingi na miiko ya uandishi wa habari. Tatizo moja ambalo limeonekana ni kubwa sana ni utandawazi ambao umekuwepo na kutokea ibuko la kila kijana kufungua gazeti tando (blog).

Hatukatai kuja kwa magazeti tando ila naomba tujiulize, yanatumika ipasavyo ama ndiyo limekuwa ni wimbi vamizi lenye kutoa ama kusambaza habari hata zile zisizokuwa na vyanzo kamili na visivyojitosheleza.Kwa sasa imezuka tabia ya wanaojiita wamiliki wa magazeti tando,wengi wao kukopi na kupaste vitu wanavyoviokota katika mitandao ya kijamii ikiwemo Twitter, facebook na mingine mingi.

Sina nia ya kumsema mtu bali napenda tuelimishane kama vijana wenzangu,ambao wametokea kuipenda fani ya uandishi wa habari, wakumbuke kuwa fani ya uandishi wa habari ina miiko na maadili yake, mfano. Katika kuandika habari za mazingira, siasa, elimu, uchumi, michezo, burudani ukiangalia habari hizi zote zina misingi na miiko yake.

 Leo hauwezi kumchukua mwandishi wa habari za michezo ukamwambia aandike habari za uchumi kwa vile hatakuwa na takwimu za uchumi na hata akiandika hiyo habari na ukiisoma utakuwa unajiuliza maswali mengi bila kupata majibu.

Vile vile ni vizuri vijana wenzangu kutambua kuwa kila kazi ina mipaka na misingi yake, juzi juzi nilisoma habari katika gazeti tando moja wapo ikisema, ‘ALIYEONGOZA MAANDAMANO YA IRINGA MHESHIMIWA MCHUNGAJI MSIGWA ASWEKWA NDANI’ nilijiuliza maswali mengi ambayo kiukweli nilikosa majibu yake, kuona huyu aliyeandika hiki kichwa cha habari kweli amepitia fani ya uandishi wa habari ama ndio ule upepo vamizi?

Maana unapoandika habari za mahakamani, polisi kuna misemo yake, hauwezi kumuhukumu mtu moja kwa moja kwa kusema fulani ni mwizi, hata hao polisi ambao huwa wanakwenda kukamata watu eneo la tukio hawawezi kusema fulani ni mwizi mpaka apelekwe mahakamani ndipo sheria ichukue mkondo wake na kumbaini huyo aliyekamatwa ni mwizi.

Naomba tufike mahali tuheshimu utu wa watu na kuepuka udhalilishaji wa bila kujua naamini baadhi ya vijana wengi walioamua kufungua magazeti hayo tando ambayo yanatoa habari, hawana taaluma ya uandishi wa habari.

Napenda kuwapongeza wale walioamua kufungua magazeti tando katika milengo yao tofauti ikiwemo kutoa habari kwa njia ya ‘kufundisha masuala ya urembo, mapishi, kuwasaidia kuwatangaza vijana katika muziki na hata wale walioamua kuandika habari zao binafsi.

Nayasema yote hayo kwa vile kumezuka wimbi la vijana wanaotaka kuichafua fani ya uandishi wa habari na ionekane si fani ya watu walioenda shule bali ni ya wahuni tu wasiojua mambo, naomba vijana tuelimike na tujifunze kwa watu wanayoyajua mambo ili tuweze kufika mbele zaidi.

Namalizia kwa kusema tusipoziba ufa tutajenga ukuta.

Asanteni sana kwa kusoma.

Imeandikwa na Cathbert A. Kajuna

www.kajunason.blogspot.com

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...