SIMBA SC imeifunga Mgambo Shooting FC ya Tanga bao 1-0
kwenye mchezo wa Ligi Kuu Uwanja wa Taifa leo.
Bao hilo lilifungwa na kiungo mshambuliaji wa pembeni,
Haroun Chanongo dakika ya nane, ambaye
alitoka na mpira katikati ya Uwanja na kuanza kuwapangua mabeki wa Mgambo kabla
ya kumchambua kipa Godson Mmassa.
Baada ya bao hilo, Simba SC waliongeza kasi ya mashambulizi
langoni mwa Mgambo na Amri Kiemba alikaribia kufunga mara mbili wakati Nassor
Masoud ‘Chollo’ na Ramadhani Singano ‘Messi’ kila mmoja alikaribia kufunga mara
moja.
Kipindi cha pili, Mgambo JKT walipambana kutoruhusu mabao
zaidi, ingawa Simba SC iliendelea kutawala mchezo huo kwa pasi maridadi na soka
ya kuvutia.
Katika mchezo huo, kipa Juma Kaseja aliokoa hatari mbili tu
kipindi cha kwanza moja alipopangua shuti la juu kabla ya kudaka na kipindi cha
pili alipodaka shuti la chini, pembeni.
Ushindi huo, unaifanya Simba SC itimize pointi 45, sasa
ikizidiwa pointi tatu na Azam FC inayoshika nafasi ya pili, ambayo Jumapili itamenyana
na Mgambo kwenye Uwanja wake wa Azam Complex, Chamazi.
Mchezo huo, ulichezeshwa na mwamuzi Andrew Shamba,
aliyesaidiwa na Abdallah Rashid na Abdallah Mkomwa wote wa Pwani, huku mezani
akiwepo Israel Nkongo.
Katika mchezo wa leo, kocha Mfaransa Patrick Liewig
aliwapumzisha wachezaji kadhaa tegemeo, Mrisho Ngassa, Shomary Kapombe, Mwinyi
Kazimoto, Felix Sunzu na Mussa Mudde kuelekea mchezo dhidi ya Yanga Mei
18.
Kikosi cha Simba SC; Juma Kaseja, Nassor Masoud
‘Chollo’/Omary Salum, Haruna Shamte, Miraj Adam, Hassan Khatib, Jonas Mkude,
Edward Christopher, William Lucian ‘Gallas’/Rashid Ismail, Amri Kiemba,
Ramadhani Singano ‘Messi’/Salim Kinje na Haroun Chanongo.
JKT Mgambo; Godson Mmasa, Salum Mlima, Ramadhani Kambwili,
Bashiru Chanacha, Bakari Mtama, Salum Kipanga, Chande Magoja/Mussa Gunda, Peter
Mwalyanzi, Issa Kandulu, Fully Maganga na Nassor Gumbo.
No comments:
Post a Comment