Diwani
wa Kata ya Kitanzini Manispaa ya Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu
(kushoto) akimkabidhi tisheti nahodha wa timu ya chuo Kikuu cha Ruaha,
Said Mohamed wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa
vyuo shiriki vya mashindano ya Pool kwa Vyuo vya Elimu ya Juu Mkoa wa
Iringa. Katikati Kushoto ni Mwenyekiti wa Chama cha Pool Mkoa wa
Iringa,Salumu Kisaku na Katibu wa chama hicho,Haji Kiyeyeu.
***************************
Na Mwandishi Wetu,Iringa
VYAMA
vya mchezo wa pool kuanzia wilaya hadi taifa vimetakiwa kutumia vizuri
udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kuhakikisha mchezo huo unaenea
katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Hayo
yalisemwa jana na diwani wa kata ya Kitanzini katika Manispaa ya
Iringa, Jesca Msambatavangu wakati alipokuwa mgeni rasmi wakati wa
kukabidhi vifaa vya michezo kwa vyuo vikuu vitakavyoshiriki mashindano
ya mchezo huo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ngazi ya mkoa wa Iringa ya
'Higher Learning Pool Competition 2013'.
Msambatavangu
alisema kuwa ni vema vyama vya mchezo huo vikatumia nafasi ya udhamini
huo vizuri katika kuhakikisha mchezo wa pool unapanuka zaidi ili
hatimaye uchezwe kila mkoa kwa mikoa yote ya Tanzania Bara kuanzia
kwenye klabu na vyuo vikuu.
"Nitakuwa
mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru na kuwapongeza TBL kupitia bia ya
Safari Lager kwa kuutoa mbali mchezo wa pool na hatimaye kuufikisha hapa
ulipo na pia udhamini wa kampuni yenu si katika mchezo wa pool pekee
bali ni mambo mengi mnayoyafanya kwenye jamii katika kuchangia maendeleo
ya taifa letu na serikali inalitambua hilo,"alisema Msambatavangu.
Aliongeza
kwa kuwataka vijana wengi kuendelea kujitokeza kujifunza kucheza mchezo
huo ambao kwa sasa ni ajira kwa vijana wanaoucheza.
Katika
kile kilichoonekana kuwa ni mmoja wa wadau wa mchezo huo, diwani huyo
aliahidi kutoa mbuzi mmoja mmoja kwa kila chuo kinachoshiriki mashindano
hayo.
Naye
mwenyekiti wa chama cha mchezo huo mkoa wa Iringa (IRPA), Salim Kisaku
alisema kuwa mashindano hayo yatakayoshirikisha vyuo vikuu vinne
yatafanyika kesho kwenye ukumbi wa Twisters Club.
Kisaku alivitaja vyuo vitakavyoshiriki mashindano hayo kuwa ni Ruaha, CDTI, Mkwawa na Tumaini.
Alisema
kuwa chuo kitakachobeba ubingwa wa mkoa huo ndiyo kitakachoushirikisha
katika fainali za taifa za mashindano hayo zitakazofanyika juni mosi
jijini Dar es salaam.
Meneja
wa Kampuni ya TBL mkoani hapa, Josephat Changwe alisema kuwa bingwa wa
mashindano hayo kwa upande wa timu katika mkoa huo atajinyakulia fedha
taslim Sh.500,000, mshindi wa pili Sh.300,000, mshindi wa tatu
Sh.200,000 na mshindi wa nne Sh.100,000.
Changwe
alisema kuwa kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja (wanaume) bingwa
atazawadiwa Sh.150,000 na mshindi wa pili Sh.100,000 wakati kwa upande
wa wanawake bingwa atapewa Sh.100,000 na mshindi wa pili Sh.50,000.
No comments:
Post a Comment