MUHIDIN GURUMO
SHEM KARENGA
STEVEN HIZZA
MUZIKI wa dansi ulioanzishwa miaka ya 1930 katika miji ya mwambao wa Bahari ya Hindi, kama vile Tanga na Dar es Salaam, unaendelea kupendwa na kuchezwa hadi leo, ijapokuwa bendi nyingi za zamani zimekufa na zilizoko zinajikongoja.
Wakati ulipoanzishwa, muziki huu ulikuwa na vionjo vya muziki wa soukous kutoka Congo -Kinshasa. Bendi nyingi za Tanzania zilizoanzishwa wakati huo, zilikuwa zikiiga muziki wa Congo.
Hata hivyo, muziki huo ulianza kuwa na mabadiliko kadri miaka ilivyokuwa ikisonga mbele. Bendi kama NUTA Jazz, Dar es Salaam Jazz, Morogoro Jazz na Tabora Jazz zilianza kubuni mitindo yake ya muziki na kuwa na mvuto kwa mashabiki.
Mikoa ya Morogoro na Tanga ilikuwa ikiongoza kwa kuwa na bendi nyingi, ambazo hivi sasa haziko katika ulimwengu wa muziki, zikiwemo Paloma Jazz, Cuban Marimba, Les Cubano, Vina vina Orchestra, Sukari Jazz, Kilombero Jazz, Malinyi Jazz, Kwiro Jazz, Mahenge Jazz na Kilosa Jazz za Morogoro.
Bendi zilizokuwepo katika mji wa Tanga ni Atomic Jazz, Jamhuri Jazz, Tanga International, Amboni Jazz, Bandari Jazz, Watangatanga, Lucky Star na Black Star.
Mwanzoni mwa miaka ya 1970 hadi 1980, ziliibuka bendi nyingine nyingi zilizokuwa na maskani katika Jiji la Dar es Salaam. Miongoni mwa bendi hizo ni Orchestra Safari Sound, Uda Jazz, Urafiki Jazz, MCA Internatinal, Washirika Stars, Orchestra Maquis Original, Dar International, Mlimani Park Orchestra na Vijana Jazz.
Kila bendi ilikuwa na mtindo wake wa uchezaji, baadhi ya mitindo iliyovuma miaka ya 1970 hadi 1980 ni Ogelea piga mbizi wa Maquiz, Takatuka na Pambamoto ya Vijana Jazz, Msondo wa NUTA Jazz, Sikinde wa Mlimani Park, Ndekule wa OSS na Super Bomboka wa Dar International.
Hata hivyo, mitindo hii ya muziki ilikuwa ni ubunifu wa majina kwa lengo la kuziongezea umaarufu bendi.
Upigaji muziki wa bendi nyingi ulikuwa ukifanana, ndiyo sababu unaitwa muziki wa dansi na hata uchezaji wake unafanana.
Kwa kawaida, nyimbo za muziki wa dansi huanza kwa kupigwa polepole kusisitiza ujumbe kwa wasikilizaji, baadaye hatua kwa hatua hupigwa kwa haraka. Kipande hiki huitwa mchemko, kwani ngoma na magitaa huongezwa sauti.
Ushindani na kupigana vijembe kwa bendi za muziki ulikuwa mkubwa na ni muhimu kwa muziki wa dansi. Kwa mfano, Maquis Original ilikuwa na ushindani na Safari Sound, OTTU Jazz ilikuwa ikishindana na Mlimani Park, Morogoro Jazz na baadaye Super Volcano zilikuwa na ushindani na Cuban Marimba wakati Jamhuri Jazz ilikuwa ikichuana na Atomic Jazz.
Licha ya bendi nyingi za muziki wa dansi kufa, bado nyimbo za zamani zina mashabiki. Hili ni kutokana na tungo zake kuwa na ujumbe unaogusa jamii, ala za muziki kupigwa kwa mpangilio wa kuvutia na pia kuwepo vionjo vyenye mvuto, vikiwemo vya asili ya makabila ya Tanzania.
Popote zinakopigwa nyimbo za zamani, mashabiki hupatwa na hisia, iwe redioni au kwenye kumbi za burudani. Ni nyimbo zisizo chuja kuzisikiliza.
Nyimbo hizi zinapopigwa humfanya msikilizaji kukumbuka ya kale au kuhusisha mambo hayo na hali ya maisha ya sasa.
Nyimbo kama vile Dada Asha, Rosa, Chakula kwa jirani na Dada Lemi za bendi ya Tabora Jazz iliyokuwa na maskani mkoani Tabora, ni miongoni mwa ambazo ladha yake haijachuja.
Ni kutokana na hilo ndiyo maana bendi kama ya Soukouss Stars ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo iliiga kibao cha Dada Asha na kukipiga upya.
Bendi nyingine iliyotikisa anga za muziki nchini ilikuwa Super Volcano ya Morogoro, iliyoongozwa na Mbaraka Mwinshehe (sasa marehemu), ambayo ilitikisa anga la muziki kwa vibao Shida, Jogoo la Shamba, Mashemeji wangapi, Dk. Kleruu na Taifa Stars.
Western Jazz, Dar Jazz, Atomic Jazz, Jamhuri Jazz na Kilwa Jazz ni miongoni mwa bendi zingine zilizotamba nchini kimuziki miaka ya 1960 hadi 1970. Hivi sasa bendi hizo hazipo.
Bendi hizi zilipotea katika anga ya muziki moja baada ya nyingine kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo za uchakavu wa vyombo.
Kufa kwa bendi nyingi za zamani kulitokana na wamiliki wake kushindwa kuziendesha kutokana na kuundwa na idadi kubwa ya wanamuziki. Kwa mfano, baadhi ya bendi zikiwemo zilizokuwa zikimilikiwa na mashirika ya umma, zilikuwa zikiundwa na wanamuziki kati ya 20 na 30.
Bendi chache zilizoko na zinazoendelea kupiga muziki wa dansi ni Mlimani Park, Msondo Ngoma, Twanga Pepeta, FM Academia, Akudo Impact, Mashujaa Band, Mapacha Watatu, Vijana Jazz na Tabora Jazz.
Licha ya kuwa na mvuto, nyimbo nyingi za zamani ni nadra kusikika zikipigwa kwenye vituo vya redio na televisheni nchini.
Vituo vingi vimekuwa vikipenda zaidi kupiga nyimbo za wasanii wa muziki wa kizazi kipya (bongo fleva) na zile za bendi zinazoundwa na baadhi ya wanamuziki kutoka nchi jirani ya DRC.
Hali hii imewafanya wanamuziki wengi wakongwe nchini wajenge hisia kwamba, baadhi ya vituo vya redio na televisheni nchini vina mpango wa kuua muziki wa dansi kwa kutopiga nyimbo hizo.
Kiongozi wa zamani wa bendi ya Kiko Kids iliyokuwa na maskani mkoani Tabora, Salum Zahoro, anasema ana hisia kuwa mpango huo umelenga kutoa nafasi kwa muziki wa kizazi kipya kupanda chati.
"Nyimbo zetu zinapendwa, lakini hazitakiwi na wamiliki wa redio na televisheni, hata hivyo, kila zinapopigwa, zinavutia zaidi kuliko nyimbo za vijana wa sasa," anasema Zahoro, ambaye kwa sasa ni kiongozi wa Shikamoo Jazz.
Zahoro anasema muziki wa dansi upo hatarini kutoweka kutokana na bendi nyingi za zamani kufa na zilizoko kusuasua.
Kwa mujibu wa Zahoro, tatizo lingine linalochangia nyimbo za zamani kutosikika redioni na kwenye televisheni ni gharama kubwa ya kurekodi nyimbo studio na kutengeneza video za muziki.
"Ukitaka kwenda studio kurekodi nyimbo, lazima uwe na si chini ya sh. 500,000 na ukitaka kutengeneza video ya wimbo mmoja, uwe na si chini ya sh. milioni 1.5. Kwetu sisi bendi za muziki si rahisi kumudu gharama hizi," anasema.
Aliyekuwa kiongozi wa Msondo Ngoma, Muhidin Gurumo, anaamini bendi zilizoko sasa zinazopiga muziki wa dansi, zitatoweka iwapo vituo vya redio na televisheni vitaendelea kutopiga nyimbo zao.
"Ukifungulia televisheni yoyote, kuanzia asubuhi hadi jioni, nyimbo zinazopigwa ni za bongo fleva tu. Huwezi kusikia nyimbo za muziki wa dansi. Hii maana yake ni kwamba, vyombo hivi vinaua muziki wetu makusudi," anasema.
Mwanamuziki mkongwe na kiongozi wa bendi ya Tabora Jazz, Shem Karenga, anasema, uamuzi wa baadhi ya vituo vya redio na televisheni nchini kutopiga nyimbo za zamani si mzuri kwa sababu umelenga kuwadhoofisha wanamuziki wakongwe.
Hata hivyo, Karenga anaamini muziki wa dansi hauwezi kufa. Anasema muziki utakaokufa na kutoweka haraka ni ule wa kizazi kipya, ambao huwekwa mipigo yake kwa kutumia kompyuta.
"Enzi zetu tulikuwa tunatunga nyimbo na kupiga muziki kwa utaalamu kwa kuzingatia utaratibu na kanuni za upigaji muziki. Nyimbo za zamani zilipigwa kwa kutumia ala na alama za muziki, ndio sababu hazichuji," anasema Karenga.
Naye Kiongozi wa zamani wa bendi ya Atomic Jazz, Zigi Said, anasema muziki wa dansi ni ala, si kutunga mashairi, hivyo si rahisi kutoweka hata kama vituo vya redio na televisheni vitaacha kupiga nyimbo hizo.
"Muziki wa dansi utaendelea kudumu kwa miaka mingi, lakini muziki wa kizazi kipya hauna maisha marefu kwa sababu wanamuziki wake hawana ubunifu katika mipigo ya ala. Mtu anatunga mashairi, anakwenda studio, anatengenezewa mipigo, anaimba, tayari unakuwa wimbo," anasema.
Hata hivyo, Zigi anasema muziki wa kizazi kipya ni matokeo ya mabadiliko ya teknolojia duniani, ndiyo sababu unapendwa zaidi na vijana, na ndiyo walio wengi kwenye vituo vya redio na televisheni.
Mmoja wa wakurugeni wa bendi ya The Kilimanjaro, Waziri Ally, anasema muziki wa bendi bado uko hai, hususan kwenye kumbi za burudani.
Hata hivyo, anasema anashangazwa na watangazaji wa baadhi ya vituo vya redio kuwataka warekodi nyimbo zisizozidi dakika tano.
"Hili ni jambo la ajabu, haiwezekani muziki wa dansi kupigwa kwa dakika tano. Hii ni sababu mojawapo ya kuua muziki kwa kutoupa nafasi ya kutosha kwenye vituo vya redio na runinga,” anasema Waziri.
Mwanamuziki mkongwe na mchambuzi wa masuala ya muziki, John Kitime, anasema kuanzishwa kwa vituo vingi vya redio za FM kumechangia kuua muziki wa dansi kwa sababu watayarishaji wake wamekuwa wakipenda zaidi kupiga muziki kutoka nje ya nchi.
"Watangazaji wa vituo hivi wamejikita zaidi kupiga na kuutangaza muziki wa nje, wameupa kisogo muziki wa nyumbani. Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA) nacho kimeshiriki kuua muziki huu," anasema.
Kitime anasema chama hicho kilishiriki kumleta nchini mwanamuziki kutoka DRC, Awilo Longomba na kufanya maonyesho kadhaa katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza.
Kwa mujibu wa Kitime, vyombo vya habari vilipoamua kutoa kipaumbele kwa kupiga muziki wa Congo, bendi nyingi za nchini ziliamua kuiga na kupiga katika mirindimo ya nchi hiyo kwa lengo la kukabiliana na ushindani wa soko.
Kitime anasema uamuzi wa bendi hizo kuiga mitindo ya Kicongo haukuzisaidia katika kuongeza soko la muziki wao, bali kujichimbia kaburi na hadi sasa hawajui watatokaje.
“Ni sawa na kusema tumeingia kwenye shimo kubwa, hatuji tutatokaje. Hii imesababishwa na vyombo vya habari, hususan redio za FM,” anasema.
Baadhi ya mashabiki wa muziki wa zamani wanalalamikia utaratibu wa vituo vingi vya redio nchini kutopiga nyimbo za zamani.
"Mwisho mwa wiki nimejiwekea utaratibu wa kusikiliza nyimbo za zamani kupitia baadhi ya vituo vya redio vinavyoandaa vipindi maalumu vya muziki huo," anasema Aloyce Jonathan, mkazi wa Temeke, Mwembe Yanga, Dar es Salaam.
Juma Mkude (45), mkazi wa Tandika, Dar es Salaam, anasema vituo vingi vya redio vinashindwa kupiga nyimbo za zamani kwa sababu havina nyimbo hizo kwenye maktaba zake na watangazaji wake hawazijui.
"Watangazaji wengi ni vijana, ndiyo sababu wanapenda muziki wa bongo fleva wa vijana wenzao. Hawana kumbukumbu ya nyimbo za zamani," anasema.
Hassan Athumani, mkazi wa Makorola, mjini Tanga, anasema kufa kwa mashindano ya bendi za muziki wa dansi nchini (MASHIBOTA) kwa kiasi kikubwa kumechangia kuzifanya bendi nyingi zitoweke kwenye ulimwengu wa muziki.
"Angalau mashindano haya yalikuwa yakizifanya bendi ziwe na ushindani wa kuwania ubingwa, hivyo kuendelea kuziweka hai. Baada ya kufa kwake, na bendi nazo zimekufa," anasema.
Kwa upande wake, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), linatajwa kuwa mstari wa mbele katika kuhifadhi nyimbo za zamani kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Mmoja wa watangazaji wa vipindi vya muziki wa zamani wa TBC FM, Mbazigwa Hassan, anasema shirika hilo lina utaratibu mzuri wa kuhifadhi nyimbo hizo, hivyo haziwezi kutoweka.
Mbazigwa anasema nyimbo hizo, ambazo baadhi zipo kwenye santuri na kanda za kaseti, zimekuwa zikihifadhiwa kwa kutumia teknolojia maalumu ili kuzifanya zisiharibike na pia ziweze kutumika kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa Mbazigwa, TBC ina utaratibu wa kupiga nyimbo za zamani kupitia vipindi vyake mbalimbali, vikiwemo vipindi maalumu vya muziki huo, kama vile Zilipendwa na Pachanga.
Kutokana na maombi ya mashabiki wa muziki wa zamani, Mbazigwa anasema TBC imeanzisha utaratibu wa kuuza nyimbo hizo katika ofisi zake zilizoko Barabara ya Nyerere na Zanaki, mjini Dar es Salaam.
Hata hivyo, Mbazigwa anasema kutokana na utaratibu wa sasa wa wasanii kurekodi nyimbo holela katika studio mbalimbali, si rahisi nyimbo hizo kutunzwa na kudumu kwa muda mrefu.
"Labda kama mmiliki wa studio ana utaratibu maalumu wa kuhifadhi nyimbo za wasanii wote wanaokwenda kurekodi kwake. Vinginevyo, nyimbo za vijana hazitaweza kudumu kwa muda mrefu," anasema.
Justine Limonga, mtangazaji wa kituo cha redio cha Uhuru FM, anasema vituo vya redio havikusudii kutopiga nyimbo za zamani, isipokuwa vingi havina programu za nyimbo hizo.
"Redio zinazopiga nyimbo za zamani ni chache na zimeweka muda maalumu wa kufanya hivyo kupitia vipindi vyake, ikiwemo Uhuru FM," anasema.
Limonga anasema watangazaji wengi wa redio ni vijana ndiyo sababu mapenzi yao yako kwenye muziki wa kizazi kipya, kwa kuwa hawaufahamu vyema muziki wa zamani.
"Huwezi kuwa mtangazaji wa nyimbo za zamani kama huzipendi. Lazima uzipende, uzijue na uzitafute. Mimi nazifahamu na ninazitafuta kwa ajili ya kuzipiga," anasema.
Modest Msangi, mtangazaji wa Redio Tumaini na kituo cha televisheni cha Tumaini anasema vipo baadhi ya vituo vya redio, ambavyo watangazaji wake wamejiwekea utaratibu wa kuomba chochote kutoka kwa wasanii ili wawapigie nyimbo zao.
"Wakati mwingine, mtangazaji akipelekewa wimbo, anamuuliza msanii, nani kautengeneza? Umerokodiwa studio gani? Lengo lake ni kutaka amtafute mmiliki wa studio ili amuombe chochote aweze kupiga wimbo alioutengeneza kwa lengo la kumtangaza kibiashara," anasema.
Kwa mujibu wa Msangi, baadhi ya watangazaji wanalaumiwa kwa kukusanya nyimbo za wasanii mmoja mmoja na kutengeneza albamu bila ya ridhaa yao.
Msangi anasema kwa vituo vya televisheni, ni vigumu kupiga nyimbo za zamani kwa sababu hazikuwahi kurekodiwa kwenye video.
Anasema nyimbo za zamani zinazopigwa na vituo hivyo ni zile zilizorekodiwa kuanzia miaka ya 1990 baada ya kuanzishwa kwa teknolojia hiyo.
Ally Kashushu, mtangazaji wa kituo cha redio cha Capital anasema, si kweli kwamba nyimbo za zamani hazipigwa kwa kukusudia, bali watangazaji wengi hawaujui muziki wa zamani.
"Kama wapo wanaoujua, basi ni kwa kuusikiliza, hawawezi kuuelezea kwa kina kuhusu historia za wanamuziki wake, nani alipiga ala fulani na nani aliimba. Kwa jumla redio nyingi zilizoko sasa ni za kizazi kipya," anasema.
Kashushu anasema kukosekana kwa waandaaji wa vipindi vya muziki wa zamani, ndiko kunakosababisha vituo vingi vya redio visiwe na vipindi hivyo kwa ajili ya wasikilizaji.
No comments:
Post a Comment