Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, September 27, 2013

BONGO MOVIE KUIMBA SIYO LELE MAMA



STEVE NYERERE  pichani  naye kaachia ngoma japo anasema kwamba yeye anaimba kwa hobbie na siyo kusaka mahela.
Huenda, kutokana na mafanikio ya aliyekuwa msanii wa filamu, Zuwena Mohammed ‘Shilole’, labda ndiko kumewapa mshawasha wengine kujaribu kuimba kwa lengo la kupata mafanikio.

.............

WASANII wengi hapa nchini, hususan wale wa filamu ‘Bongo Movie’ wengi wao wameibuka na kutangaza kuacha kucheza filamu na kugeukia muziki wa Bongo Fleva.

Hii ni sawa, lakini je ni kweli wana vipaji vya kuimba ama ni kutaka kuuza sura tu?

Ni jambo la kawaida na zuri, kwa kila binadamu kuamua kuiga mambo mbalimbali yaliyo mazuri, ikiwa ni njia moja katika kusaka maendeleo binafsi.

Lakini katika hili, wasanii wa bongo movie, wengi wenu kugeukia muziki hiyo si sawa, kwani inaonesha dhahiri kwamba, wengi wao wanafuata mkumbo.

Kwa kufuata mkumbo huku, sina shaka kwamba, hata nyimbo watakazoziachia hazitakuwa na mashiko kama jinsi ilivyo kwa wasanii ambao tangu awali waliamua kujikita katika muziki.

Ushauri wa safu hii ni kuwaomba wajidhatiti katika kuandaa filamu zao, ambazo kwa ukweli usiopingika, nyingi zimekuwa zina upungufu mwingi ambao unahitaji marekebisho.

Lakini, badala ya kufanya masahihisho katika filamu zao na kuondoa makandokando yaliyomo, sasa  wanageuza mwelekeo na kukimbilia muziki, ambako nako sitarajii kama watatenda miujiza.

Nadhani, laiti kama wakiamua kujikita ipasavyo katika filamu na kutuliza vichwa vyao, sambamba na kupata mafunzo mbalimbali yanayohusu fani hiyo, huenda wangefika mbali zaidi ya hapa walipo kwa sasa.

Inasikitisha kuona kwamba, msanii ambaye alikuwa anafanya vema katika filamu, kisha akageukia bongo fleva lakini anashindwa kufanya vizuri katika kuimba, hii itaweza kumshusha hata katika mauzo ya filamu zake bila ya yeye kujua.

Usanii ni pamoja na kukopi, lakini kwa kukopi kipaji cha mtu hii si sawa, kwani kila mtu amezaliwa na kipaji na uwezo wake, hivyo kwa kulazimisha kipaji ambacho siyo cha kwako, sidhani kama yupo ambaye atafanikiwa.

Huenda, kutokana na mafanikio ya aliyekuwa msanii wa filamu, Zuwena Mohammed ‘Shilole’, labda ndiko kumewapa mshawasha wengine kujaribu kuimba kwa lengo la kupata mafanikio.

Kwa upande wa Shilole, Mungu alimuumba na kumpa vipaji, kwani yeye alipotangaza kuwa muimbaji wa Bongo Fleva, alitoka na Aboubakar Katwila ‘Q- Chillah’ na wimbo wa ‘Sitaki Lawama’ akaonekana kama kabebwa, lakini  kwa kuwa ule ulikuwa ndiyo mwanzo, wengi wakasema acha tumpe nafasi.

Akaja akaachia ngoma nyingine ‘Paka wa Baa’, hapo kila mtu akamkubali na sasa anatamba na kibao cha ‘Nakomaa na Jiji’.

Hivi sasa, Shilole ameweza kupata mialiko mingi na kufanya maonesho kwenye matamasha mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Jina la Shilole, limekuwa kubwa na kazi yake inatambulika hata kama wapo ambao watasema amebebwa, lakini ukweli ni kwamba, uwezo wake unaonekana dhahiri.

Cha kushangaza kwa sasa ni hawa wasanii wengine wa filamu, kupanga mstari na kutangaza nia ya kuingia katika bongo fleva.

Sawa, tangazeni nia siyo vibaya, ila je mtaweza kumudu au mnadhani kuna mteremko huko?

Muziki siyo lele mama, lazima uwe na uhalisia na siyo mchezo wa maigizo kama jinsi mlivyozoea huku wakati mwingine ‘mkikopi’ kazi za watu na kuziweka sokoni.

Safu ya Busati, inawatahadharisha bila kificho, ingieni katika muziki lakini mje mkiwa kamili.

Baadhi ya wasanii ambao wametangaza kuimba ni pamoja na Wema Sepetu, Jokate Mwegelo, Aunt Ezekiel, Rashida Wanjara, Mzee Magari, Rose Ndauka na wengineo wengi, lakini hadi sasa hakuna kipaji chochote kimeonekana na kufanya vizuri.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...