Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Saturday, September 21, 2013

MIKAKATI YA KUBORESHA SHULE ZA JUMUIYA YA WAZAZI YAANDALIWA


Katibu wa CCM wilaya ya muheza mkoani Tanga, Josephine Thomasi (aliyesimama) akimkaribisha Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi mkoani humo, Dk.Edmund Mndolwa, wakati wa ziara yake ya kutoa shukrani kwa kumchagua na pia kueleza uhai wa jumuia hiyo. Kikao hicho kilichofanyika katika ofisi za CCM wilayani humo, kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali ya jumuia hiyo kuanzia kata na wilaya.

Mwenyekiti wa Jumuia ya wazazi mkoa wa Tanga, Dk.  Edmund Mndolwa, wa nne kulia, akiwa na baadhi ya viongozi wa bodi ya Shule ya Sekondari Shemvua iliyoko wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, wanafunzi wa shule hiyo na viongozi wa jumuia hiyo mkoani Tanga. shule hiyo inamilikiwa na jumuia ya wazazi.
TANGA, Tanzania

MWENYEKITI wa Jumuia ya wazazi mkoani Tanga, Dk. Edmund Mndolwa, amesema kuna mikakati ya haraka ya kuboresha shule za Jumuia hiyo ili ziweze kutoa elimu bora.

Alisema shule za jumuia ya wazazi zilikuwa kimbilio la wazazi na Watanzania kwa jumla, lakini kwa sasa zinakabiliwa na soko la ushindani kutokana na shule nyingi za kata na binafsi.

Akizungumza katika ziara ya kutoa shukrani katika mkoa wa Tanga kwa kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa jumuia hiyo, Dk. Mndolwa alisema shule za wazazi zote nchini zinakabiliwa na uhaba wa walimu, vitendea kazi na vitabu.

Alieleza kuwa shule hizo zimekuwa na tatizo la mfumo wa uendeshaji wake, kitu kinachochangia kujiendesha kiholela na wakuu wa shule kuzichukulia kama zao.
“Tunatakiwa kubadilika na kuzirejesha shule zetu katika hali yake ya zamani. Kwa kufanya hivyo, tutawafanya Watanzania waendelee kuzikimbilia shule hizo ambazo zilikuwa mkombozi kwao,

“Tushirikiane kuanzia wazazi kwa kulipa ada ili walimu wapate mishahara mizuri na wakipata mishahara mizuri watafundisha kwa ari na moyo, hivyo hata watoto wetu watapata elimu nzuri,”alieleza Dk. Mndolwa.

Dk. Mndolwa alisema kuwa mkoa wa Tanga una shule za wazazi sita huku nchi nzima kukiwa na shule za wazazi 71.

Aidha, akizungumza katika wilaya za Mkinga, Muheza  na Pangani, Dk. Mndolwa aliwataka viongozi wa jumuia hiyo kuwa watumishi wa watu kwa kwenda kusikiliza kero zao katika ngazi za chini badala ya kujifungia ofsini.

Vilevile, aliwataka viongozi hao kuachana na dhuluma kwa wanachama wanapokuwa wanaomba nafasi ya uongozi, kwani kwa kuendeleza dhuluma kunachangia kupunguza nguvu ya chama.

“Unakuta mwanachama anakubalika na wananchi lakini kwa sababu ya chuki na dhuluma anapewa mtu mwingine ambaye hakuongoza kura za maoni, hali ambayo hujenga chuki kwa wanachama na kuamua kuwapigia kura wapinzania,

“Ukiangalia, nafasi nyingi tulizopoteza katika ngazi mbalimbali kuanzia wenyeviti wa serikali za mitaa, udiwani na ubunge, nafasi nyingi zimetokana na dhuluma, na waliowachagua wapinzania ni wanaCCM wenyewe kwa sababu ya kuchukizwa kwa mtu waliyempenda kutorudishwa jina lake,”alieleza.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...