Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Monday, September 16, 2013

BALOZI IDDI ASHIKIA BANGO ZOEZI LA UFUFUAJI WA KITUO CHA UPANDISHIAJI NG'OMBE ZANZIBAR


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiushauri  Uongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwa na kara kana ya kisasa ya vyombo vya moto  wakati alipoitembelea kara kana ya wizara hiyo iliyopo Maruhubi. Kulia kwa Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mh. Mohd Said Dimwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikagua hatua zinazoendelea kuchukuliwa na  Wizara ya Mifugo na Uvuvi Zanzibar ya kukifufua upya kituo cha upandishiaji Ng’ombe kiliopo eneo la Maruhubi . Kushoto kwa Balozi Seif ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi hiyo  Dr. Kassim Gharib . Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
********************************
Wizara ya Mifugo na Uvuvi Zanzibar  iko katika harakati za kukifufua  upya Kituo cha kupandishia Ngombe  kilichopo katika eneo la Maruhubi  nje kidogo ya Mji wa Zanzibar ili kirejee katika utaratibu wake wa kutoa huduma bora kwa wafugaji wa Ngo’mbe wa kisasa hapa Nchini.
Kituo hichoanzishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  mwanzoni mwa miaka ya 70 na kusitisha huduma zake  kutokana na mabadiliko ya sera ya ufugaji kwa kuachiliwa  suala hilo kuendeshwa na wananchi moja kwa moja.
Katibu Mkuu  Wizara ya Mifugo na Uvuvi Zanzibar Dr. Kassim Gharib alieleza hayo wakati wa ziara fupi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika katika eneo hilo  kukagua juhudi zinazochukuliwa na Wizara hiyo katika kukifufua tena kituo hicho.
Dr. Kassim alimueleza Balozi Seif kwamba Wizara hiyo imeanza na hatua ya kuzunguusha ukuta eneo hilo ili kuzuia uvamizi wa ujenzi  holela wa nyumba pamoja na uchimbwaji ovyo wa mchanga uliokuwa ukitishia uchafuzi wa mazingira.
Alisema hatua hiyo itakapokamilika itatoa fursa kwa wafanyakazi wa Mifugo kuendelea na hatua ya pili ya upandaji majani kwa ajili ya malisho ya madume ya ng’ombe watakaotumiwa kutoa mbegu na kuendelea kusambazwa kwa wafugaji kwenye maeneo mbali mbali nchini.
Dr. Kassim alifahamisha kwamba licha ya matatizo na changamoto mbali mbali zilizokuwa zikikikabili  kituo hicho lakini bado kinaendelea kutoa huduma za upandishiaji ng’ombe kikiwa na Madume Sita bora  ya kisasa hivi sasa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif pia alipata fursa ya kukagua kara kana inayohudumia matengenezo ya dharura ya vyombo vya moto vya Wizara hiyo ya Mifugo na Uvuvi iliyopo jirani na kituo hicho.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...