Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, March 7, 2014

OMOTOLA: MWANAUME NDIYE KIONGOZI WA NYUMBA
ACCRA, Ghana
MCHEZA filamu nyota wa Nigeria, Omotola Jalade ameamua kuvunja ukimya kwa kusema, haamini iwapo kuna kitu kinachoitwa usawa katika ndoa kama wanavyopigania wanawake.

Akihojiwa na gazeti la Punch la Nigeria wiki hii, Omotola alitaja mambo mbalimbali yanayopaswa kufanywa na wanandoa ili ndoa yao iweze kudumu kwa muda mrefu na kuwa na mafanikio.

Kwa mujibu wa Omotola, haamini kuwepo kwa usawa wa kijinsia na kwamba wanawake wanapaswa kutambua kuwa, wanaume ni viongozi wa familia.

Omotola, ambaye ndoa yake na mumewe, Matthew Ekeinde imedumu kwa miaka 18, alisema:
"Siamini usawa wa kijinsia. Siamini kwamba Mungu amemuumba mwanaume na mwanamke kuwa sawa kwa njia yoyote."

"Naamini kwamba katika kila taasisi iliyojiimarisha, siku zote yupo kiongozi na msaidizi wake. Haimaanishi kwamba mmoja anapaswa kumdharau mwenzake. Naamini kwamba, mume ndiye kiongozi wa nyumba na mke ni msaidizi,"alisema msanii huyo, ambaye pia ni mwanamuziki.

Omotola alisema inapotokea mwanamke anaanzisha mapambano ya kutaka kuwa kiongozi wa nyumba dhidi ya mwanaume, ni rahisi kwa ndoa yao kuwa na msuguano. Alisema mwanamke anapaswa kumuheshimu mwanaume kama kiongozi wa nyumba.

"Naye anapaswa kuthibitisha kwamba ni rubani msaidizi. Mwanaume anahitaji kuwa na msaidizi bora,"alisisitiza Omotola, ambaye amecheza filamu zaidi ya 50 za Kinigeria.

"Wakati mwingine, mwanaume anaweza kushindwa kuendesha nyumba. Inapotokea hivyo, unapaswa kuchukua uamuzi, lakini unatakiwa kufanya hivyo kwa nia nzuri, ambayo inaweza kumfanya mwanaume ajisikie vizuri na kukuona mtu anayestahili kukutegemea,"alisema Omotola.

"Unapokuwa na mume mwenye majivuno, mkabidhi kwa Mungu. Unapohisi maisha yako au ya watoto wako yapo hatarini, jitoe katika hali hiyo,"aliongeza.

Hata hivyo, Omotola alisisitiza umuhimu wa wanandoa kuwa karibu na kuwasiliana vyema kwa sababu mambo hayo husaidia kujenga penzi la kweli na dhati.

Alipoulizwa ni kipi kilichomvutia kwa mumewe, Omotola alisema ni kwa sababu ya mwonekano wake na uwezo wake mkubwa wa kupambanua mambo.

Wakati huo huo, Matthew Ekeinde mwishoni mwa wiki iliyopita alimwacha mkewe, Omotola Jalade, akiwa kinywa wazi baada ya kuzuka ghafla katika sherehe yake ya kuzaliwa nchini Ghana.

Omotola aliandaliwa sherehe hiyo na wafanyakazi wa ofisi yake iliyoko nchini Ghana kwa ajili ya kusherehekea kutimiza miaka 36.

Kabla ya Omotola kuanza kukata keki, alipatwa na mshtuko baada ya kumuona mumewe, Matthew, akizama ofisini na kumshika mabegani.

"Oh Mungu wangu," alitamka Omotola baada ya kugeuka nyuma na kumuona Matthew akiwa ametandwa na tabasamu mwanana.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...